December 5, 2016




Wakati fulani niliwahi kuandika kuhusiana na maandalizi ya ligi za vijana na wanawake ambazo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limezianzisha.

Nilieleza kwamba ni jambo zuri ambalo tulilisubiri kwa muda mwingi kwa kuwa kutokana na rundo la wadhamini na misaada lukuki ambayo TFF ilikuwa ikipata, ingeweza kuzianzisha mapema.

Lakini hazikupewa kipaumbele na huenda lilionekana ni jambo la kawaida tu. Mfano fedha zilizomwagwa kwenye Taifa Stars Maboresho zingeweza kuanzisha ligi ya vijana na leo kungekuwa na majibu.

TFF iliyojaa wajuaji, haikuwahi kusikiliza maoni. Ilipenda kufanya mambo kwa kile wanachotaka wao. Wakaanzisha Taifa Stars Maboresho na leo hii, wale waliojiita washauri wa TFF, hakuna hata mmoja anataka kuizungumzia.

Lakini hata viongozi wenyewe wa TFF anzia ngazi ya chini, katikati na juu, nao hawataki kuizungumzia wala kuisikia.


Leo Tanzania inalia na msiba wa kinda wa Mbao FC ya Mwanza, Ismail Mrisho Khalfan ambaye amefariki dunia uwanjani katika mechi dhidi ya Kagera Sugar.

Mechi hiyo ya michuano ya Ligi ya Vijana U20 ilikuwa inapigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba jana, mauti yamemkuta kinda huyo.

Kamwe sitaki kulaumu, sitaki kumuonyesha mtu kidole na ninaweza kusema kifo cha Khaflan ni mipango ya Mungu.

Ukiangalia namns alivyokuwa anawania mpira na mchezaji wa Mwadui FC, halafu ukaambiwa aliumia hadi kupoteza uhai. Hakika utakubali tu kwamba ni kazi yake Mola.

Wakati tunalikubali hilo, pia tunaweza kujifunza. Hasa pale unapoona mwili wa Khalfan ukipakiwa kwenye gazei la Zimamoti kumplekeka hospitali.

Gari la Zimamoto, kazi yake inajulikana na si kumbeba mgonjwa. Tena kwenda kumbeba mgonjwa kwenye uwanja wa soka kama Kaitaba.

Nilisema TFF imeandaa ligi hiyo ya vijana kama sehemu ya kampeni kwa uongozi uliopo madarakani. Uchaguzi ni mwakani na wanataka kuitumia kama sehemu ya kupigia debe.

Maandalizi yao, yalikuwa ya kulipua, ilimradi walitaka kuonyesha wana mambo mengi na wako busy. Lakini ukweli hawakuwa wamejipanga vizuri na Khalfan kupakiwa kwenye gari hilo la Zimamoto ni sehemu ya kudhihirisha kwamba hawakujipanga na haikuwa sawasawa.

Vifo Mwenyezi Mungu anapanga, lakini kama wanadamu lazima tuwe sahihi kwenye mambo yanayoeleweka. Gari la wagonjwa haliwezi kukosa katika michuano kama hiyo, tena ya vijana. Si sahihi hata kidogo.


Ninaweza kuanika makosa rundo kutokana na ukurupukaji huo wa TFF wakiwaza watafanyaje uchaguzi ujao kuliko wataendelezaje soka lenyewe.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic