Na Saleh Ally
BEKI Abdi Banda ndiye beki tegemeo katika kikosi cha Simba sasa hivi katika utakuwa unazungumzia mlinzi wa kati namba nne.
Banda anacheza na beki mkongwe wa Simba, Method Mwanjale raia wa Zimbabwe. Banda anachukua nafasi hiyo baada ya kuonekana ana uwezo wa juu zaidi kuliko Novalty Lufunga ambaye ameporomoka kama tone la maji kutoka juu ya bati baada ya mvua kukatika.
Naamini niliwahi kuandika, kwamba Abdi Banda ni beki anayestahili kucheza nafasi ya mlinzi wa katikati kuliko pembeni ambako alikuwa akiichezea Coastal Union.
Vigezo vyangu vilikuwa vinne. Kwanza ni umbo lake, pili uwezo wa kupiga vichwa, tatu nguvu ambayo nilishauri aongeze kidogo mwili na mwisho ni namna ambavyo anajiamini kutokana na kuwa na uwezo mzuri au mkubwa wa kumiliki mpira.
Wakati Banda amemtoa Lufunga, inajulikana hivi; ataendelea kucheza katika nafasi hiyo hadi hapo beki Mganda, Juuko Murshid atakaporejea nchini atakapotoka katika michuano ya Afcon ambako amekwenda kushiriki nchini Gabon.
Tayari Uganda wametolewa na matarajio kwamba Juuko atarejea hivi karibuni. Lakini najiuliza kwa nini Banda akubali Juuko arejee na kumtoa tu wakati tayari ameonyesha anaweza na kinachotakiwa ni kuongeza ubora.
Kama binadamu, siku moja Banda anaweza kukosea lakini hadi sasa hakuna anayeweza kubisha kuwa safu ya ulinzi ya Simba ni kati ya zile zilizo imara na kufungwa mabao machache.
Ukiangalia kati ya wachezaji waliopiga vichwa vingi zaidi katika Ligi Kuu Bara, Banda ni mmojawapo. Hii inaonyesha ni beki imara.
Simba wanaweza kumtegemea sana Juuko lakini kwangu naona ni kupoteza muda tu. Kwani hata kabla ya michuano ya Afcon alianza kuwadengulia na uongozi wa Simba unajua.
Kabla ya hapo, aliwahi kugoma kupanda basi na wachezaji wenzake akidai ni safari ndefu, akalipiwa nauli ya ndege. Unakumbuka mwishoni mwa msimu uliopita aliweka mgomo pamoja na wachezaji wengine kwenda kucheza Songea eti mshahara umecheleweshwa.
Katika hali ya kawaida, Simba haina nafasi kubwa ya kumtegemea Juuko ambaye ninaamini baada ya Afcon, kwa kuwa wakala wake ni kocha wake, basi hakuna shaka atakuwa kashaanza kumtafutia timu na mkataba wake Simba unaisha, hivyo atakuwa akivizia aondoke akiwa mchezaji huru na kuingiza mamilioni zaidi.
Kwa sasa, Simba inapaswa kuendelea kumjenga na kumuamini Banda ambaye ana faida nyingi zaidi. Kama kijana wa Kitanzania ambaye anaweza kuwa na faida hata kwa timu ya taifa na ikiwezekana kuipatia Simba faida.
Lazima niendelee kuwa mkweli, kwamba Banda amekuwa kati ya wachezaji wasiojitambua. Hakuwa makini, hakuwa akifanya mazoezi kwa juhudi, badala yake alikuwa na mipango mingi bila ya juhudi.
Niliwahi kuandika aliyekuwa Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa aliyeamua kumuonya na kumueleza wazi kwamba kama itakuwa anakamatwa na msuli wa paja kila wanapoanza mazoezi ya Taifa Stars basi mara nyingine asingemuita tena kwa kuwa ugonjwa huo mara nyingi unatokana na uvivu wa mazoezi au kutokuwa fiti.
Mkwasa alimueleza Banda maneno hayo tukiwa Kartepe nchini Uturuki ambako Stars ilikuwa imeweka kambi. Kweli baada ya hapo hadi anaondoka Stars hakuwa amemuita na kweli Banda hakuwa amebadilika.
Kwa sasa, kumuacha Banda Stars si rahisi kwani ukiachana na utendaji bora ameanza kuonyesha yuko makini, hataki utani. Juzi baada ya Simba kumaliza mazoezi ya pamoja, yeye akaondoka anakimbia pembeni ya barabarani wakati wenzake walikuwa kwenye magari.
Hii inaonyesha kuwa kweli Banda amebadilika na vizuri akaungwa mkono na kama alikosea hapo awali, ichukuliwe kama sehemu ya ujio wake mpya hivyo aungwe mkono badala ya kuadhibiwa kwa kumbukumbu au yaliyopita.
Mimi ninaimani kama atakuwa makini na kuendelea kuongeza juhudi kama alivyoanza. Nina imani hakuna wa kumzuia Banda kumfutilia mbali Juuko na kuendelea kuijenga hazina ya Tanzania ambayo imejificha ndani ya mchezaji huyo kinda ambaye ninasisitiza, akiendelea kuwa makini, kucheza nje ya Tanzania au Ulaya wala haliwezi kuwa jambo gumu kwake.
0 COMMENTS:
Post a Comment