February 13, 2017




Na Saleh Ally
JUNI 18, 1971 Rais wa Marekani wakati huo, Richard Nixon alitangaza rasmi kuwa madawa ya kulevya ndiyo adui namba moja wa taifa hilo. Akisisitiza vita imeanza na adui huyo ni lazima apigwe na kuangushwa.

Nixon alitangaza hilo mbele ya waandishi wa habari baada ya kuwa amezungumza na viongozi wa nchi.

Vita hiyo haijawahi kusimama na sasa imefikia Marekani inatumia hadi dola bilioni 51 (Sh trilioni 112) kwa mwaka kwa ajili ya vita ya madawa ya kulevya.

Hapa nyumbani, mkuu wa mkoa wa jiji kubwa zaidi nchini, Dar es Salaam, Paul Makonda, ameanzisha vita ya kupambana na madawa ya kulevya na tayari watuhumiwa wamekuwa wakitajwa na kufika kwenye Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam maarufu kama sentro kuhojiwa na wengine wamefikishwa mahakamani.

Vita ya Makonda dhidi ya madawa ya kulevya si yake kwa kuwa anawapigania Watanzania na nguvu kazi ya taifa letu ambayo inaonekana kuingia kwenye “fasheni” ya matumizi ya madawa hayo inayoanzisha mambo mengi mabaya kwa ajili ya taifa.

Kitu kibaya zaidi, madawa hayana faida zaidi ya wachache wanaoingiza fedha huku nguvu kazi ya nchi yetu ikiteketea.

Hasara za madawa ya kulevya au unga kama ilivyo maarufu ni kuua nguvu kazi ya taifa kwa njia nyingi kama vijana kushindwa tena kufikiri kiushindani, kutokuwa wabunifu, kusambazwa kwa kasi kwa virusi vya Ukimwi na hata kusambazwa kwa tabia za kishoga.

Kama itatotea mtu akampinga katika vita hiyo, nitasema akapimwe kwa kuwa athari zinapozidi kuwa juu basi kila mmoja zitamkuta. Ndiyo maana nchi kama Marekani imeamua kutumia mabilioni ya dola kuhakikisha inaikomesha, lakini ajabu kabisa, haijawahi kukoma.
Ukitaka kujua vita ya madawa si ya leo, Marekani walianzisha sheria mwaka 1931 kupambana nayo. Sasa wanapeleka hadi dola milioni 500 nchini Colombia pekee kuhakikisha wanaidhibiti kwa kuwa huko ndiyo matatizo makubwa. Na inaelezwa imefikia hadi watu 50,000 hupoteza maisha katika vita dhidi ya madawa.

Hii ni vita ya dunia nzima, lakini Marekani wamekuwa waathirika wakubwa kwa kuwa soko kuu liko nchini humo ndiyo maana nilianza kutolea mfano.

Vita inayoendeshwa na Makonda ni ya sisi sote lakini binafsi nimekuwa nikiona haiendi katika njia sahihi inayoweza kutoa picha kwamba kweli imelenga hasa kuwakamata wauzaji au wasambazaji sahihi.

Tumeona wasanii mbalimbali kama akina Wema Sepetu, Khaleed Mohammed ‘TID’,  Hamidu Chambuso ‘Dogo Hamidu au Nyandu Toz’, Anna Kimario, ‘Tunda’, Winifrida Josephat ‘Recho’ na wengine wakiitwa sentro na kufikishwa mahakamani na baadaye wakaachiwa kwa dhamana kwamba watakuwa chini ya uangalizi kwa mmoja na miwili.

Tumeona watu wengine maarufu zaidi kama Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji na mfanyabiashara mkubwa pia kiongozi wa dini, Askofu Josephat Gwajima, pia wakiitwa kama sehemu ya watuhumiwa.

Mbunge wa zamani wa Kinondoni (CCM), Iddi Azzan na mwenyekiti wa chama namba moja cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe akiitwa pia, hata hivyo aligoma kwenda.

Wengi wameitwa kwa tuhuma au lengo la kusaidia. Kwa maelezo kwamba wanatuhumiwa kutumia au kusambaza lakini lengo ni kuisaidia polisi. Hii imezua mazungumzo mengi pembeni wengi wakiamini si sahihi.

Mimi naungana na wale wanaoamini kuna makosa mengi katika njia ya upambanaji huu. Hasa unapoona watu wanatangazwa siku mbili kabla, baada ya hapo wanafika kituoni wakiingia na kupigwa picha, baada ya hapo wanachukuliwa kwenda kupekuliwa nyumbani kwao na ofisini.

Ninaanza kuwaza tofauti kama kweli hii ni vita sahihi ya madawa ya kulevya au ina nia nyingine? Kama haina, basi ninaamini wahusika wanaikosea na huenda wamekosa angalau wa kuwapa ushauri tu wa wazi kwa nia njema.

Mbaya zaidi, walioanzisha mjadala pembeni wamekuwa waoga kwa kuwa inaonekana ukimwambia Makonda umekosea basi utakuwa matatizoni. Hili ni jambo baya kabisa kwa nchi kama yetu, watu kuwa na hofu hata ya kusema ukweli kwa lengo la kujenga kwamba “utashughulikiwa”, siamini hilo.

Hata vyombo vya habari navyo vimeshindwa kuwa huru na kusema kweli kwa nia ya kujenga. Waandishi nao wana hofu ya “kushughulikiwa?” Acha mimi niwe wa kwanza.

Wanaoshindwa kusema, wanazidi kuivuruga hii vita, badala ya kulenga kuwaokoa ndugu zetu na kuwakomesha wanaofaidika nayo kwa kuliumiza taifa letu, wapo walioigeuza kuwa ya ushabiki wa Yanga na Simba au kama ile ya zile timu za mtandaoni, “Team Diamond”, “Team Kiba”. Hii si sahihi hata kidogo.

Hatuwezi kuwa na taifa la watu waoga, wasioweza kusema au kuchangia jambo kwa nia nzuri eti unaogopa kushughulikiwa au kukamatwa. Tanzania ni yetu sote, si ya Makonda pekee na kwa kuwa vita aliyoianzisha ina nia njema kama alivyoeleza basi tuichangie na kuingiza mawazo chanya ili kuisaidia ifanikiwe.

Lakini bado ninaona, katika vita hiyo kuna haja ya kuheshimu na kuthamini utu wa watu na kuepusha kuifanya ionekane ni ya kisiasa au ya visasi. Tuhuma kwenda hadharani bila ya uhakika hata kidogo, si sahihi. Tukumbuke wahusika wana biashara zao, familia zao, watu wanaoawaamini. Lazima ubinadamu wao uthaminiwe.

Jeshi letu la polisi lina wataalamu wengi wenye ujuzi wa juu kabisa. Huenda linaweza likafanya mambo yake kwa uhakika zaidi kuliko mfumo unaotumika wa watu kwenda polisi kama wanakwenda kwenye mkutano wa kampeni.

Kama Marekani wanapambana na vita hiyo miaka nenda rudi tena kwa njia rundo za kitaalamu na hadi leo mtandao wa madawa unaendelea kuwasumbua, basi lazima tujue hii haiwezi kuwa vita ya shoo na ikafanikiwa.

Tangu mwaka 1971, Rais Nixon alipotangaza rasmi madawa ya kulevya ni adui namba moja wa Marekani, zimeshaandikwa ripoti zaidi ya 50 zikionyesha namna walivyofeli katika kupambana na madawa ya kulevya na zimetumika kuboresha njia za vita hiyo inayoonekana kutokuwa na mwisho.

Kumekuwa na kila aina ya njia za kupambana kwa kuwa wauza unga ni kama kinyonga, wanabadilika kulingana na mazingira, mtandao wao mkubwa pia ni watu wenye nguvu kubwa. Siamini kwa mwendo huu wa kutaja majina kwa matangazo, watu wakaenda na kupokelewa na vyombo vya habari ndiyo vita sahihi pekee.

Mwaka 2000, Marekani walifikia bajeti ya dola bilioni 18.4 kupambana na madawa huku Jiji la New York likitumia 17% ya bajeti yake katika suala la madawa pekee. Kiasi hicho kilitumika katika masuala la tiba, ushawishi wa kuepuka madawa hayo haramu lakini pia uchunguzi wa kina yaani research, nini cha kufanya, wapi sehemu zilizoathirika, nini kifanyike na wapi pa kushikilia.

Sisi hatujafanya research ya kutosha, hakuwezi kuwa na research ya wiki au mwezi kuhusiana na suala hili halafu tukasema imeanza kufanyiwa kazi. Tutakuwa tumekurupuka, lazima kuwe na utulivu na wataalamu washirikishwe hasa huku wakipewa nafasi.

Tumeona wanaokamatwa asilimia 85 ni watu maarufu. Nani anataka kunithibitishia hakuna wasio maarufu wameathirika? Hakuna maarufu wanaotumia au kuuza? Sasa kwa nini wale maarufu tu? Vipi hatujaona hata mmoja ambaye hatukumtarajia?

Nani anaamini wanaotumia ni wasanii wa Bongo Movie na Bongo Fleva pekee? Ndiyo maana nasisitiza, kuna shida katika mwenendo wa vita aliyoianzisha Makonda na huu ndiyo mchango wangu kwamba vizuri ikaenda kuwa vita iliyolenga kweli kulimaliza tatizo hili ambalo si dogo na si rahisi kulimaliza kama tunavyoona.

Kuhofia kumueleza Makonda ni kuendelea kuifanya vita hiyo kuwa ngumu zaidi na kuendelea kupoteza muda wote kwa mashabiki wa Simba kuwabeza wa Yanga kwa kuwa kiongozi wao katajwa, huku Yanga nao wakisema hata wao kiongozi wao katajwa pia.

Lengo si kuonyesha kina nani wamekosea au kina nani si wasafi. Lengo ni kupambana na madawa ya kulevya kuokoa nguvu kazi.

Wabunge walipoibuka na kupinga mambo kadhaa ya kampeni hiyo ya Makonda walikuwa sawa kukosoa. Huenda naye hakufurahishwa akatoa kauli ambayo pia haikuwa sahihi.

Kweli Bunge ni mhimili unaojitegemea, ndiyo unaotunga sheria za nchi na una haki ya kuzisimamia. Naamini bila ya kukosea hakuna aliye juu ya sheria. Huenda ‘approach’ ya uzungumzaji ya wabunge ilimkera Makonda, lakini huwezi kulizuia bunge kusema.

Unaona sasa, mjadala umegeuka, umekuwa ni Makonda kuhojiwa na kamati ya bunge. Hii naona ni sehemu nyingine itakayopunguza vita hiyo ya madawa ya kulevya na kusababisha ndani ya vita hiyo kuwa na vita nyingine ya Makonda na wabunge na mwisho itawapa ahueni wasambazaji, wauzaji na hata watumiaji kuendelea na mambo yao kama kawaida.

Mwenendo sahihi ndiyo utafanya vita hii iwe sahihi. La sivyo, itakuwa ni vita ya muda mfupi na baada ya hapo mambo yataendelea kama kawaida, huku wako wakiwa wamechafuliwa kimakosa au kuonewa kwa kuwa hawakuwa na nguvu ya kujitetea.

Katika ripoti ya mwaka 2012 ya Umoja wa Mataifa (UN) ya madawa ya kulevya, imeeleza takribani watu 200,000 kila mwaka hupoteza maisha kutokana na madawa hayo haramu kwa maana ya afya pekee.

Dunia hutumia hadi dola bilioni 250 (zaidi ya Sh trilioni 547) kwa mwaka ili kuwasaidia waathirika kwa njia sahihi.

Ripoti hiyo imeeleza watu milioni 230 au asilimia 5 ya watu duniani kote wameathirika na madawa hayo haramu na wanawake wanaonekana kuwa waathirika wakubwa zaidi.

Hii si vita ndogo wala fupi. Tumuunge mkono Makonda na Rais John Pombe Magufuli ambaye ameeleza nia yake ya kupambana. Watu wawe huru na kuchangia kwa maoni chanya ya kujenga ikiwezekana kulisaidia Jeshi la Polisi kwa kulionyesha njia za wahusika.

Isiwe kutajana kwa visasi na wivu unaolenga kukomoana, pia Makonda awe tayari kupokea maoni kwa kuwa hawezi kuwa sahihi katika kila kitu.

Nisisitize hatuwezi kuwa taifa la hofu tupu tukafanikiwa, lakini hatuwezi kuwa sahihi kwa kutaka kukosoa kwa kuharibu au kukatisha tamaa.

Mimi nawaasa, tusiifanye vita hii ni ya siasa au Usimba na Yanga au Udiamond na Ualikiba. Watu muwe huru, tuendelee kuifanya Tanzania kuwa Free Land, Land of Democracy na tuichangie vita hii tukiamini inatuokoa sisi, familia zetu na vizazi vyetu vijavyo.

MUNGU IBARIKI TANZANIA

1 COMMENTS:

  1. Umeeleweka,lkn nawe umeeleza kwa uoga pia,hukufunguka wamekosea wapi na kwa nini iwe wamekosea,funguka nyinyi ndio tunawategemeeni,funguka kaka mimi nakuamini

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic