March 22, 2017MSUVA-YANGA


Wafunga bora watatu kati ya watano wa juu kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara, wamekuwa wakivaa viatu vya kampuni ya Nike, hali inayoonyesha kuwa viatu hivyo ni bora zaidi kwa ufungaji.

Kwenye chati ya wafungaji Tanzania Bara, mshambuliaji wa Yanga Simon Msuva ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao 12, huku akifuatiwa kwa karibu na Shiza Kichuya wa Simba mweney mabao 11, ambao wote hawa wanavaa viatu vya kampuni hiyo.

Nike ambayo pia inatumiwa na mshambuliaji hatari wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, imekosa nafasi ya tatu kwa ufungaji huo ambayo imechukuliwa na Mbaraka Yusuf wa Kagera Sugar ambaye ameshapachika mabao kumi kwenye ligi hiyo yeye akiwa anavaa kiatu cha kampuni ya Adidas.

Pia ikapinduliwa kwenye nafasi ya nne ambayo ipo kwa mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe ambaye naye anavaa Adidas, huku Nike ikirudi kwenye nafasi ya tano ambayo yupo John Bocco wa Azam mwenye mabao nane kwenye ligi.

Hii ni sawa na kusema kuwa Nike ndiyo imewazawadia wachezaji hao watatu kati ya watano kwenye chati hiyo mabao hayo, lakini ikiipiga bao Adidas.

BOCCO-AZAM FC

Hali hii inaonyesha kuwa kwenye mabao 50, ambayo yamefungwa na wachezaji watano wa juu kwenye chati hiyo ya Ufungaji hadi sasa, Nike imechukua mabao 31, huku 19 yakizolewa na Adidas ambayo inavaliwa na staa wa Barcelona Lionel Messi.

Mbali na hao pia mshambuliaji wa Simba, Laudit Mavugo mwenye mabao saba, ambaye aliwafungia bao pekee kwenye ushindi wa dhidi ya Madini kwenye mchezo wa Kombe la FA, wikiendi iliyopita naye anavaa kiatu cha kampuni ya Nike.

MAVUGO -SIMBA

Tofauti na klabu kubwa za Ulaya, wachezaji wetu wenyewe wanavaa viatu hivi kwa mapenzi yao wenyewe na hakuna anayelipwa chochote na kuna uwezekano hata kampuni hizo hazijui kama mfungaji bora wa Tanzania anavaa kiatu chao.


Wachezaji wote wa ligi kubwa Ulaya wamekuwa wakipewa viatu hivyo na makampuni husika, lakini mbali na kupewa wamekuwa pia wakilipwa mabilioni ya fedha kutokana na kuvivaa.

“Mimi tangu mwanzo nilijikuta tu napenda kuvaa Nike sikuwahi hata siku moja kushawishiwa na hadi leo naendelea kutumia viatu vya kampuni hiyo,” aliwahi kusema mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva.

Mbali na wafungaji, Nike imeteka pia kwenye idara nyingi nyeti kwenye vikosi vya Simba, Yanga na Azam, kwenye kikosi cha Azam kilichoanza dhidi ya Mbambane, wachezaji zaidi ya sita walikuwa wamevaa Nike.


Kwenye mchezo wa Simba na Yanga uliopita wachezaji wa Simba zaidi ya sita pia walikuwa wamevaa Nike huku wa Yanga napo ikiwemo idadi kubwa kama hiyo.

1 COMMENTS:

  1. Ukikosa habari zenye akili bora utulie acha kuandika blaablaa zinachosha sana akili za wanaokufuatilia mimi mmoja wao.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV