May 4, 2017


Mdau mkubwa wa soka nchini, Nassor Bin Slum amesema klabu kongwe nchini za Yanga na Simba, zinachangia kuzorotesha maendeleo ya soka nchini.

Bin Slum amesema pamoja na umaarufu wa timu hizo nyingi, masuala mengi ya soka nchini yamekuwa yakifanyika kishabiki na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha maendeleo ya mchezo huo.

“Utaona kama kuna jambo viongozi wanashindwa kufanywa kwa kuwa huku kuna Simba, kule kuna Yanga na mwingine anashabikia timu hii na mwingine ile,” alisema Bin Slum katika mahojiano maalum na kipindi cha SPOTI HAUSI ambacho hurushwa moja kwa moja na runinga ya mtandaoni ya Global tv online.

“Hii inaleta tatizo, inasababisha kuzorotesha mambo katika soka. Mfano angalia hili suala la rufaa ya Kagera limekuwa kubwa sana kwa kuwa upande mmoja wapo Simba na mwingine Yanga ambao walipoingia, wamekuwa wakisema wazi hawataki hili au lile lifanyika.

“Sitaki kuingia sana kwa kuwa ukiwakosoa Yanga hata kama kuna ukweli watasema wewe ni Simba, hali kadhalika upande wa Simba watakuambia wewe ni Yanga. Ingawa niwe mkweli, sina hofu hata kidogo kusema ukweli, kwanza mimi si Simba wala Yanga.”

Bin Slum ambaye ni mmiliki wa kampuni maarufu ya uuzaji matairi ya magari ya Bin Slum Tyres Ltd, ni shabiki mkubwa wa klabu ya Coastal Union ya Tanga ambayo sasa iko ligi daraja la kwanza.

Kampuni yake ya Bin Slum Tyres Ltd imekuwa msitari wa mbele katika udhamini wa michezo na hasa soka kwa kuwa sasa inaendelea kuidhamini klabu ya Mbeya City kupitia bidhaa zake za betri za magari za RB.

Kabla alizidhamini Stand United na Ndanda FC kupitia matairi maarufu ya Vee Rubber na Double Star.

Pia kampuni hiyo imewahi kuzidhamini timu za Coastal Union na African Sports. Bin Slum amekuwa akifafanua kuhusiana na Coasta Union kwamba hakuwa mdhamini hasa lakini alisaidia kutokana na mapenzi yake kwa klabu hiyo.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic