June 16, 2017Na Saleh Ally
JUMA Said maarufu kama Nyosso, amerejea Ligi Kuu Bara.
Nyosso ataonekana katika ligi hiyo katika kikosi cha Kagera Sugar chini ya Kocha Mecky Maxime ambaye ameiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya tatu baada ya kwisha kwa Ligi Kuu Bara.

Kagera Sugar ina wachezaji kadhaa walioonekana hawana kiwango kizuri au walihofiwa lakini sasa wanafanya vizuri.
Wachezaji wanne wanaweza kuwa mfano mzuri. Edward Christopher ambaye alichemsha kabisa Simba baada ya kuwa amefanya vizuri katika timu ya vijana ya klabu hiyo.


Mbaraka Yusuf ambaye alipelekwa kwa mkopo kutokana na kiwango chake kuonekana bado kwa Klabu ya Simba. Kweli lengo lilitimia, chini ya Maxime ameondoka Kagera Sugar akiwa shujaa baada ya kugombewa na Yanga, Simba na Azam FC ambao wameonekana kuwa na kisu kikali, mwisho wamekula nyama.

Mohamed Fakhi, huyu ni beki wa kati. Alichukuliwa na Kagera Sugar baada ya kuonekana hana namba Simba, lakini akiwa Kagera amekuwa shujaa na unaona mwisho timu yao imeshika nafasi ya tatu.

Kawaida nafasi tatu za juu kwa zaidi ya misimu mitano imeonekana ni mali ya timu za Dar es Salaam, yaani Yanga, Simba na Azam FC.

Mchezaji mwingine ni kipa, Juma Kaseja ambaye ni mahiri lakini amegeuzwa kuwa mshindani wa wasio na juhudi. Wengi wanachukizwa na yeye kucheza tu, mfano alipokuwa Simba.

Hakuna aliyekuwa anapima ndani ya Kaseja kuna nini. Kwamba anacheza tu kwa kuwa anapewa zawadi na kocha au anajituma na kupata nafasi?

Maxime amemchukua na alisema ukweli, iliwahi kuonekana kuwa Kaseja anahongwa na akawa anaonywa. Mwisho akawaambia hawamjui Kaseja, ndiyo maana yeye akamuajiri na amewaonyesha wale waliokuwa wanafikiria tofauti.

Hivyo, Nyosso ametua katika mikono sahihi, sehemu ambayo anaweza kurudisha heshima yake baada ya kuwa imeingia katika walakini kutokana na mienendo yake kuonekana hailengi ushindani sahihi au ule wa Fair Play unaohimizwa sana na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Nyosso alionyesha vitendo ambavyo havikuwa vya kiungwana baada ya kumtomasa makalio Elius Maguri ambaye alikuwa mshambulizi wa Simba wakati huo.

Ikaonekana ni kama jambo la bahati mbaya na kadhalika na wapo waliojitokeza kumtetea. Miezi michache baadaye, Nyosso akarudia jambo hilo, safari hii akimfanyia John Bocco nahodha wa Azam FC wakati huo, sasa ni mshambulizi wa Simba.

Hakika yalikuwa ni mambo ya hovyo na yaliyopaswa kulaaniwa. Lililowaudhi wengi ni lile la marudio, lilionyesha Nyosso si mtu aliyekuwa tayari kujifunza na hasira zilisababisha watu wengi na hasa mitandaoni kuandika mambo mabaya kuhusiana na Nyosso.

Hayo yamepita na hatuwezi kuacha kuyasema kwa lengo la kuweka mambo sawa kwa sasa.

Nyosso ni mtu anayeweza kuzungumza na mtu yeyote kiungwana. Matendo yake ndiyo yaliyoleta hisia mbaya dhidi yake kutoka kwa jamii inayomzunguka.

Waliokasirika walikuwa na haki, lakini kama unakumbuka Nyosso aliomba radhi licha ya kwamba alifungiwa. Kikubwa wakati namkaribisha leo, nilitaka kuwakumbusha wadau, wapenda soka na wanajamii ya wapenda michezo kwa jumla, kwamba tumkaribishe kwa msamaha na kumpa nafasi tena.

Neno zuri la tahadhari kwa Kingereza ni precaution. Ndiyo maana ningependa kumkaribisha Nyosso kwa “Welcome with precaution”. Yaani karibu kwa tahadhari.

Ninasema tahadhari kwa kuwa kila upande utakuwa na jicho tofauti la utazamaji wa mambo na utendaji wenyewe. Watakaotazama hivyo wana haki kutokana na yaliyotokea nyuma, lakini hawapaswi kuhukumu badala yake watoe nafasi kwa Nyosso.

Huenda Nyosso akawa na hofu katika utekelezaji wa mambo yake kwa hofu ya watu kusema. Anapaswa kuchukua tahadhari lakini kikubwa ni usahihi wa mambo na aepuke tahadhari isiharibu malengo yake.

Kikubwa ni kuepuka vitendo vya kihuni alivyokuwa akifanya. Kwani kama atarudia, nafikiri adhabu yake inapaswa kuwa itakayotikisa dunia kama sehemu ya kumbukumbu.

Nyosso wakati tunamkaribisha na amerejea, tukubali binadamu ana nafasi zaidi ya moja kujirekebisha. Alirudia kosa moja mara mbili, hivyo tusiamini anaweza kurudia wakati hajafanya.

Tusimhukumu, waamuzi wasijenge chuki dhidi yake, kosa dogo likawa kubwa. Wachezaji wasimjengee mazingira ya kukosea kwa kuwa anajulikana ni mkosaji badala yake, apewe nafasi iliyo wazi, iwe kazi kwake kujaza akionyesha amebadilika au ameshindwa!0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV