June 19, 2017



Na Saleh Ally
WIKI iliyopita tulimkaribisha Ibrahim Akilimali kwa ajili ya mahojiano katika kipindi cha Spoti Hausi ambacho hurushwa na runinga maarufu ya mtandaoni ya Global TV Online kila Alhamisi kuanzia saa 10:00 jioni.

Yalikuwa mahojiano mazuri yaliyowavutia watu wengi sana. Huenda ilitokana na uwazi alionao mzee Akilimali ambaye ni Katibu wa Baraza la Wazee la Klabu ya Yanga.

Kwanza, nianze kwa kuwapuuza watu wachache ambao upeo wao na masuala ya mpira ni mdogo na huenda wanapenda kuropoka ili kuonekana wanajua.

Wako waliolaumu kwamba kualikwa kwa mzee Akilimali ni kuivuruga Yanga. Huu ni upuuzi wa kupindukia, Yanga haiwezi kuvurugwa na mtu kutoa maoni yake. Tena maoni yake, yanaweza kuonyesha msimamo au ni mtu anayetaka nini.

Kipindi cha Spoti Hausi, Gazeti la Championi au Saleh Ally hawana upande. Hivyo tutaendelea kuwahoji watu tunaowahitaji kulingana na tunavyowapata bila ya kujali nani anafurahi au kukasirishwa eti kwa kuwa anayehojiwa hampendi.

Nikirejea kwa mzee Akilimali, ni mzee wetu na mahojiano yake na kipindi hicho cha Global TV Online, yamenifanya nipate wazo la kuandika makala haya.

Mzee Akilimali amesema alitua jijini Dar es Salaam mwaka 1971 akitokea kwao Kigoma. Alisisitiza amekuwa akiipenda Yanga na amechangia maendeleo yake tangu wakati huo.
Ndiyo maana ninasema hivi, ana haki ya kuwa na uchungu na klabu hiyo kwa kuwa kaiona au alikuwa nayo kabla ya wengi sana hasa sisi hatujazaliwa.

Nani anaweza kusema mzee Akilimali atafurahia Yanga ifeli, hasa kwa kulingana na historia yake na klabu hiyo? Hakika hakuna.

Lakini maneno anayoyazungumza, utagundua mengi yangekuwa bora sana mwaka 1978 au 1988, au 1998 na si leo kwa kuwa mambo yanakwenda kwa kasi kubwa.

Mfumo wa uendeshaji umebadilika sana, ukimsikia mzee Akilimali bado anazungumzia enzi za Abbas Gulamali au Abbas Tarimba ambaye ninaamini kama atarejea leo, ataongoza kwa mfumo tofauti sana.

Mzee Akilimali alielekeza lawama zake kwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga ambaye kwa kipindi hiki ndiyo kiongozi mkuu wa klabu hiyo baada ya Yusuf Manji kujiuzulu. Mfano mmoja alisema hivi: “Sanga aliwaambia wadhamini SportPesa wasitupe basi ambalo wanatakiwa kutupa na badala yake watujengee uwanja wa mazoezi, sasa huo si upigaji?”

Nilipomuambia kuwa Yanga tayari wana basi, bora kuwa na uwanja, akaonekana kubabaika kuelezea akitoa mfano hata zamani walikuwa na mabasi mengi!

Utaona namna hesabu za Sanga zilivyokuwa sahihi lakini mzee Akilimali bado anawaza enzi hizo walivyomiliki mabasi zaidi ya moja. Jiulize mabasi mawili au basi moja na uwanja wa mazoezi kipi ni bora?

Sanga ni mfanyabiashara ambaye ataangalia uendeshaji kwa mfumo wa sasa na nini kilicho sahihi kutokana na kipindi husika.

Hakuna asiyejua Sanga ni kati ya viongozi bora kabisa Yanga wamewahi kupata. Hakubali unafiki wala upindishwaji wa mambo. Hivyo wasimuadhibu kwa yeye kuwa mkweli na kutaka mambo yaliyonyooka.

Ndiyo maana nimeona nisisitize kwamba, ninaamini mzee Akilimali ana uchungu na Klabu ya Yanga kwa kuwa ametoka nayo mbali. Lakini anaweza kutoa nafasi kwa wenye mawazo chanya kulingana na wakati waongoze klabu hiyo.
Wako wazee wengi wa klabu wamekuwa wakizikwamisha klabu hizi kongwe kupiga hatua kwa kuwa wanataka yale ya zamani yaaminike zaidi katika kipindi hiki.

Lakini wako ambao wamekuwa wakifaidika na migogoro kama ambavyo unakumbuka mzee Akilimali alikuwa mtetezi mkubwa wa uongozi wa Yanga chini ya Manji na Sanga na taarifa zinaeleza alinyimwa posho ya kamati ya ufundi tokea hapo, akaamua kuchukua upande wake.
Katika hilo, baada ya kumuuliza, mzee Akilimali alilifafanua kwa kusema: “Akutukanaye hakuchagulii tusi.”

Hakutaka kuendelea kulifafanua, jambo ambalo bado sikuridhika nalo. Ndiyo maana nasisitiza, kama ni kweli ni jambo baya, kama si kweli ni jambo baya pia maana si vizuri kumsingizia mzee.

Lakini tukubali wako wanaofaidika na migogoro ndani ya klabu hizo kwa visingizio vingi lakini namba moja ni “tunaipenda Yanga”. Hii si sawa, acheni mapenzi yenu yaendelee halafu fanyeni kazi kutafuta fedha nje ya klabu hizo.

Yanga ya sasa haiwezi kuendeshwa kama Yanga ya mwaka 1980. Lazima mkubali, mwenendo wa mchezo wa soka unabadilika na ndiyo maana kunaweza kuwa na mdhamini anayekubali kutoa hadi Sh bilioni moja kwa msimu mmoja tu kwa klabu kama Yanga.

Kumbukeni wakati huo hakukuwa na hata wadhamini wa Sh laki moja kwa msimu. Badala yake ni wafadhili wanaojitolea tu.

Sasa kama ni wadhamini, basi lazima mambo yafuate makubaliano ndani ya mikataba na kadhalika.
Wazee wawe sehemu kuu ya washauri lakini nao wakubali kwamba kuna mambo yanayotokea sasa wanapaswa kujifunza.

Mwisho nisisitize, si vema kuwafanya viongozi watumwa wa wazee. Kwamba kiongozi ambaye ana mipango bora na anaonekana kutosikiliza kila “wanachotaka” wazee, basi aonekane hafai, hii si sawa. Vizuri viongozi wakawa sehemu ya chachu ya msukumo wa maendeleo badala ya kugeuka breki ya maendeleo.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic