July 4, 2017





Na Saleh Ally
NIMEJIFUNZA sana kwamba wakati mwingine usajili umekuwa ukifanywa kwa maana ya kufurahisha watu au mashabiki wa klabu na si kitaalamu sana.

Nilikuwa najiuliza kwa nini Simba imekuwa “busy” kufanya mazungumzo na Donald Ngoma wakati ina John Bocco na Laudit Mavugo? Nilianza kuamini huenda ilitaka kuwanyima kabisa raha Yanga na mwisho kuwafurahisha mashabiki wake.

Achana na hadithi za pembeni, Ngoma na Simba walifikia pazuri kabisa. Na kama uongozi wa Yanga usingejitutumua kutuma wanachama kumpokea uwanja wa ndege na kuhakikisha unajichanga na kumsajili, basi alikuwa amebakiza kusaini tu Simba.

Usajili wa Ngoma, kama angekwenda Simba basi Mavugo au Bocco mmoja asingetakiwa kuwepo. Hivyo Simba hawakupaswa hata kupambana kutaka kumsajili Ngoma kutokana na kikosi chao kilivyo.

Hilo tuachane nalo, zaidi nataka kuzungumzia mazugumzo ya soka. Ninapokuwa mitandaoni au mitaani, mashabiki wengi wamekuwa wakiniuliza au kunielezea mambo mawili ambayo nimeamua kuyazungumzia.

Mashabiki wa Yanga na Simba, wamekaa katika mikao miwili tofauti. Upande mmoja una hofu kuu na mwingine unaonekana ni wenye faraja hata kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Bara.

Simba tayari wanaamini ni mabingwa, hii ni kutokana na usajili wao mpya wa wachezaji kama watano sita hivi; angalia Haruna Niyonzima ambaye taarifa zinaeleza Simba wana hofu ya kutangaza kwa kuwa mkataba wake na Yanga haujaisha.

Wana Shomari Kapombe, Aishi Manula na John Bocco lakini usisahau wameshamalizana na Emmanuel Okwi ambaye ni mchezaji halali wa Simba. Hivyo mashabiki wanaona hakuna wa kuwazuia kubeba ubingwa.

Yanga wao ni hofu, kwamba hawaoni kama kuna usajili mkubwa. Hakuna mchezaji hata mmoja mpya ambaye ameshuka Jangwani anayeweza kuonekana ni hatari sana.

Ibrahim Ajibu kutoka Simba, ndiyo kiasi fulani hawana uhakika na matumaini yameamka zaidi baada ya uongozi wa Yanga kumnasua Ngoma kwenye mdomo wa Simba.

Huenda kuondoka kwa Niyonzima kumetengeneza hofu zaidi. Lakini unashangazwa na mashabiki wa Yanga wanavyoweza kuwa wasahaulifu mapema sana.

Kwamba bado ni timu mbili pekee zenye kikosi bora zaidi katika Ligi Kuu Bara. Yanga wamo na ndiyo wa kwanza kwa kuwa ni mabingwa na wanafuatiwa na Simba ambao wanaonekana hawana tofauti kwa kuwa walimaliza ligi kila upande una pointi 68.

Simba kweli wamejiimarisha lakini Yanga wamefanya hivyo kwa kiwango cha kati, wameimarisha difensi yao kwa kumsajili Abdallah Haji Shaibu ‘Ninja’ lakini bado muda unawaruhusu kufanya usajili.

Ingawa kama mashabiki watakuwa wanaweza kuangalia kwa jicho la mbali zaidi wataona Yanga haikuwa ikihitaji usajili mkubwa zaidi kwa kuwa ina wachezaji wengi wenye uwezo wa kucheza na kufanya vema.

Yanga wanaweza kuwa na hofu ya Niyonzima wakiwa na Thabani Kamusoko? Nani asiyemjua na wote wanaelewa kazi yake ilivyo. Ukweli ni hivi, lazima kuwe na juhudi kuu katika nafasi ya kiungo mkabaji na hapo ndiyo Yanga wanapaswa kupatupia jicho.

Kiungo mkabaji mpya wa uhakika, akitua Jangwani, Kamusoko atasogea mbele na unaweza kusema “hakuna matata”.

Lakini ukizungumzia ulinzi, una Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Juma Abdul au Ramadhani Kessy na pia Haji Mwinyi. Wachezaji hawa wote ni wa kiwango cha kimataifa.
Kama ni katika ushambulizi hata kama Simon Msuva afanikiwa kuondoka na kujiunga na timu ya Morocco inayomuwania, wako wachezaji kama Emmanuel Martin au Juma Mahadhi wanaweza kufanya vizuri katika nafasi yake.

Achana na hao, Yanga mbele ndiyo imekamilika zaidi na kila mmoja anajua. Hasa unapomuona Ngoma, Obrey Chirwa ambaye hakika ni mmoja wa washambulizi hatari zaidi na msimu ujao, kama atatulia basi atakuwa gumzo.

 Chirwa alifunga mabao 12, Msuva alifunga 14, Ngoma alifunga nane na Amissi Tambwe akatumbukia wavuni mara 11 na amekuwa mfungaji mwenye mwendo sahihi kwa misimu minne mfululizo.

Hivi, hofu ya hao wanachama ni nini? Au walitaka usajili wa mbwembwe ili kupata nafasi ya kujidai? Simba hawana hofu kwa kuwa wameona mabadiliko wakiongeza wachezaji wapya lakini bado hawatakiwi kujiamini kwa asilimia mia maana soka, lina mambo yake.

Ushauri wangu kwa viongozi wa kila upande, hasa unapofikia wakati wa usajili, inakuwa vizuri sana kufanya mambo kitaalamu badala ya furaha ya mashabiki ambao sahihi wanatakiwa kufurahia wakati wa ligi au michuano ya kimataifa.

Kama usajili utakuwa wa mbwembwe halafu ukashindwa kuwa na tija, basi hakutakuwa na tija na furaha haitakuwa ile iliyo na tija.






1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic