July 20, 2017





Ni wiki sasa imekatika tangu Everton waweke historia ya kuwa klabu ya kwanza inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uingereza kucheza mechi kwenye ardhi ya Tanzania na Afrika Mshariki kwa ujumla.

Pamoja na mechi dhidi ya Gor Mahia ambayo waliibuka na ushindi wa mabao 2-1, lakini pia Everton walipata kutembelea sehemu mbalimbali nchini ikiwemo shule ya viziwi na vipofu ya Uhuru Machanganyiko, Albino United, Hospitali ya Pugu, na sehemu nyingine kadha wa kadha.

Everton walikuja nchini na ujumbe wao wa Together Inspired “Kwa pamoja tumehamasika” ukiwa ni ujumbe ulioambatana na kampeni ya uzinduzi wa jezi yao mpya ya ugenini ambayo waliitumia kwa mara ya kwanza kwenye mchezo dhidi ya Gor Mahia katika ardhi ya Tanzania.

Katika sehemu ambayo ujumbe huo wa Everton ilileta uhalisia ni pale ambapo baadhi ya wachezaji wa Everton walitembelea uwanja wa Uhuru siku ya Jumatano ya Julai 12 ambapo walikutana na timu ya watu wenye Ulemavu wa ngozi ya Albino United.

Albino United walikuwa ni sehemu ya ujio huo wa Everton ambapo walitembelewa na wachezaji watatu wa Everton, Michael Keane, Mohamed Besic na Tom Davies ambapo waliwakuta wakifanya mazoezi uwanjani hapo chini ya kocha wao Alex kashasha.

Sambamba na kufanya nao mazoezi, lakini pia wachezaji hao waliongoza zoezi la kugawa zawadi kwa wachezaji wa Albino United ambapo waliwapa shin guards, mipira, jezi, Kamba za kuruka, pampu za kujazia mipira pamoja na vifaa vingine vingi vya kimichezo.

Wachezaji Michael Keane pamoja na Tom Davies walipata fursa ya kuongea na waandishi wa habari waliokuwepo uwanjani pale ambapo walieleza hisia zao baada ya kuweza kukutana na timu hiyo.

Maneno ya Tom Davies
Kwa Tom Davies ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza ya chini ya miaka 19 alisema ni mara yake ya kwanza kukutana na timu ya mpira wa miguu iliyoundwa na watu wenye ulemavu ili kufikisha ujumbe kwa jamii.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kuona timu kama hii lakini nimeona umoja kati yao na inaleta picha nzuri ukiwa hapa. Wote ni marafiki na nina Imani kocha ataweza kuwasaidia sana, kwakweli nina furaha sana kuwepo hapa.”

Mbali na kuwa ni mara yake ya kwanza, lakini pia Davies alisema kuwa mpira wa miguu ni mchezo unaoleta watu pamoja na anawashauri Albino United kuendelea kufurahia kucheza pamoja.

“Ni vizuri kuwa hapa kuona timu inavyocheza na kufurahia wanachokifanya na hiyo ndio maana halisi ya soka na michezo kwa ujumla ya kuwaleta watu pamoja. Ninachopenda kuwaambia ni kuwa waendelee kufurahia kwani ndio kitu kizuri kufanya na nina Imani kuwa kocha atawasaidia”, alisema Michael Keane.

Michael Keane
Naye beki wa kati wa Everton, Michael Keane alieleza hisia zake baada ya kuja kukutana na wachezaji hao.
“Ni ngumu sana kwao na nimekuwa nikisikia kuwa wanapitiahali ngumu sana kwahiyo kwa wao kuja pamoja na kufurahia ni jambo zuri sana.

 “Ni vigumu kuona timu kama ya Albino United kwa Uingereza kwani huwa wanachukuliwa kama watu wasiokuwa na mchango kwenye jamii hivyo kuona watu wanapata shida sio jambo rahisi hata kidogo.

Keane alimalizia kwa kusema kuwa wana kila sababu ya kuendelea kufurahia kile wanachokifanya na wacheze kwa bidiI.

“Ningependa kuwaambia kuwa waendelee kufurahia katika kile wanachokifanya na nina furaha kuwa hapa kuwaona walivyo na umoja ni jambo zuri”, alimalizia Michael Keane.
Ni jambo zuri kuona wachezaji wa Everton wakija na kutoa mchango wao kwa watu wenye uhitaji maalumu na pia wakieleza uzoefu wao katika hilo.

Kweli kama ambavyo wamesema kwenye kauli mbiu ya kampeni yao ya Together Inspired (Kuhamasika kwa pamoja) basi bila shaka wameweza kutoa hamaa kubwa sana kwa wachezaji wa timu hii ya Albino United ambayo imeamua kutumia mpira wa miguu kama sehemu ya kufikisha ujumbe wao kwa jamii.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic