August 10, 2017



USAJILI ndiyo jambo gumzo zaidi katika kipindi hiki hata baada ya kufungwa kwa dirisha lenyewe la usajili.

Kila upande ukianzia mashabiki, wanachama na hata viongozi wa timu wamekuwa wakijiuliza kama wako sahihi au la.
 Ukiangalia kwa sasa, pamoja na kujiuliza kila upande unaweza ukawa na majigambo ya awali ambayo uthibitisho wake ni hadi hapo itakapoanza ligi wikiendi ijayo. Baada ya mechi kadhaa, utaanza kupata majibu akina nani walipatia mapema au akina nani ili wapatie wanatakiwa kuanza kurekebisha mambo mapema au wakati wa dirisha dogo.

 Binafsi ningependa kuuzungumzia usajili wa Yanga kwa kipande kimoja tu cha ushambulizi. Kwangu naona pamoja na wengi kuamini Yanga hawako vizuri sana, lakini kwa takwimu na watu walionao inaonyesha bado wana nafasi ya kuwa tishio au hatari kwa safu nyingi za ulinzi watakazokutana nazo.

 Yanga ilicheza Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu mfululizo na kufunga mechi dhidi ya timu zote ilizokutana nazo bila ya kujali ilipoteza au kushinda.

 Kama hiyo haitoshi, utaona wachezaji wake wote ni wale waliokuwepo misimu minne, mitatu au miwili iliyopita na wanaweza kuungana na kufanya vizuri zaidi kwa msimu unaofuata.

Katika safu ya ushambulizi ya Yanga, Donald Ngoma alifunga mabao nane, Amissi Tambwe akafunga 11 na Obrey Chirwa akapachika 12, angalia wachezaji hawa walivyo na uzoefu na ambavyo wameonyesha kuwa wanaweza kuifanya kazi yao kwa uhakika.

 Ngoma alikosekana mwishoni kutokana na majeruhi, lakini Chirwa akageuka kuwa shujaa na tegemeo na Tambwe akaendelea kufunga mabao muhimu katika kipindi yanayotakiwa kufanyika. Hii ni sehemu ya kuiangalia safu ya ushambulizi ya Yanga kwa jicho la pili.


 Mtu wanayemkosa hapa ni Simon Msuva ambaye amekwenda Morocco kucheza soka la kulipwa. Bado wana mtu kama Emmanuel Martin ambaye atapata msaada mkubwa kutoka kwa kinda Baruan Akilimali ambaye ni mpya lakini bado kinda Yusuph Mhilu pia ana nafasi ya kuwa msaada mkubwa.

 Kama utafuatilia kwa mtu mpya ambaye unaweza kusema wamemuongeza ni Ibrahim Ajibu kutoka Simba. Unategemea kumuona naye anaongeza nguvu kwa kiasi kikubwa. Ndiyo maana baada ya Simba kumalizana na Ngoma na wakisubiri kumsainisha, Yanga walilitambua hilo litawaangusha, wakafanya juu chini na kumbakisha.

 Katika usajili mpya utagundua ukiachana na Ajibu, Yanga hawakutaka kupeleka nguvu nyingi katika ushambulizi maana Kocha George Lwandamina anajua watu alionao ni wale wanaoeleweka na wenye uhakika.

Badala yake akashuka nguvu nyingi katika kiungo hasa baada ya kuondoka kwa Haruna Niyonzima lakini katika safu ya ulinzi kwa kuwa anajua baadhi ya wachezaji wake ni wazoefu lakini taratibu umri unawatupa mkono.

 Kwa misimu minne mfululizo, safu ya ulinzi ya Yanga ndiyo iliyofunga mabao mengi zaidi kuliko safu ya nyingine zote, jambo ambalo hata msimu huu linaweza kuendelea kwa kuwa uchezaji wa Lwandamina zaidi ni kushambulia kwa nguvu.



Yanga wanajilinda kwa kushambulia, wakitumia mfumo wa kisasa wa “ulinzi kwa kuhifadhi mpira”. Huu ni mfumo unaoilazimu timu inayoshambuliwa ishindwe kuchukua mpira kwenda kushambulia badala yake inawekeza akili zake katika ulinzi zaidi na kufanya isiwe na madhara katika lango la timu pinzani.

Mambo mawili pekee yanaweza kuiangusha safu hiyo ya ushambulizi ya Yanga kufanya vizuri kama ilivyokuwa kwa misimu miwili iliyopita.

 Kwanza ni majeruhi. Kama itatokea majeruhi mfululizo, inaweza kuwa na shida. Hili Yanga wanatakiwa kuomba kwa kuwa safu yao ya ushambulizi ina ‘advantage’ ya wachezaji wazoefu ambao wanaweza kuisaidia sana kama nilivyoelezea.

 Lakini wazoefu maana yake “wamekula chumvi”, umri wa kuanzia miaka 30 au zaidi ya 25. Wengi wao kama watapata jeraha kubwa, mara nyingi wanachelewa kupona ukilinganisha na vijana wengi kama ambavyo sayansi ya mwili inavyoeleza.

Jambo la pili ni uongozi; hili ni muhimu zaidi. Maana timu inaweza kuwa na kikosi kizuri, chenye washambulizi wakali na wasiwe majeruhi, lakini uongozi ukawavunja moyo na mwisho wakashindwa kupambana.


 Suala la uendeshaji ni muhimu sana. Lazima uongozi uwe makini katika kuhakikisha unawahisha mishahara, uwe karibu na wachezaji na kuwapa morali kabla na baada ya mechi. Kama utashindwa, utageuka kuwa tatizo na huenda washambulizi hao watashindwa kuonyesha walichonacho.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic