September 20, 2017




Na Saleh Ally, aliyekuwa London
NAKUMBUKA ilikuwa ni siku chache kabla ya Arsenal kuivaa Bournemouth kwenye Uwanja wa Emirates jijini London.

Mimi na rafiki yangu mmoja tulikuwa tumesimama mbele ya uwanja huo karibu na duka kubwa la kuuza vifaa mbalimbali vya Arsenal, mara kuna gari lililobeba watu wawili likasimama.

Baada ya gari lile kusimama, mmoja wao ambaye alikuwa abiria alisimama na kuanza kutoa maneno machafu akimtusi kila aliyekuwa amesimama mbele ya duka la Arsenal huku akitumia neno “shetani” au “wasaliti”. Kama hiyo haitoshi, shabiki huyo aligeuka na kuvua akatuonyesha makalio yake, halafu akaimba wimbo wa kuisifia Tottenham Hotspurs na kurejea kwenye gari, likaondoka kwa mwendo wa mbwembwe!

Nilibaki nimepigwa butwaa, nilimgeukia rafiki yangu na kumuuliza kuhusiana na tukio hilo. Lilinishangaza na nilitaka kujua sababu ya mtu yule kuvurumisha matusi ya mwendo kasi kwa watu bila kosa.



Alinieleza jamaa ni mmoja wa mashabiki wa kufa wa Totteham, kazi yake ni fundi ujenzi na wakati huo alikuwa katika kazi zake za kawaida na moja ya starehe zake ni kuitukana Arsenal kwa matusi makali. Baada ya hapo, nikataka kujua kuhusiana na upinzani wa timu hizo mbili za Kaskazini mwa jiji kubwa zaidi katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) la London.

Hili ndilo lilinivutia kuandika makala kuzizungumzia timu hizi mbili hasa ile ishu ya “North London Derby”. Mechi ambayo kwa mashabiki wa soka nchini Tanzania wanaweza kuiona ni ya kawaida lakini ndiyo mechi inayolitikisa zaidi Jiji la London kuliko hata Arsenal wanapokutana na Manchester United.

Ukubwa wa Manchester United na ule wa Arsenal, unaifanya mechi yao kuwa kubwa sana. Lakini kwa London, mechi kubwa zaidi ni hiyo inayozikutanisha Arsenal dhidi ya Tottenham, mechi ambayo inasababisha jeshi la polisi na vyombo vya ulinzi kufanya kazi ya ziada.



Chama cha Soka cha England (FA), kimepitisha kwamba; kinapopanga ratiba, haitatokea Arsenal na Tottenham zote zikacheza London, labda tu zinapokutana zenyewe. Kama ni mechi ya ligi Arsenal ipo Emirates, basi Tottenham haiwezi kucheza White Hart Lane (imebomolewa), sasa wanatumia Wembley.

Hii ni kwa sababu za kiusalama, kwani mashabiki wa Arsenal wangekuwa wanakwenda Emirates kuona timu yao inacheza dhidi ya Bournemouth wakakutana na wale wa Spurs wanaokwenda White Hart Lake kuangalia timu yao ikicheza dhidi ya Manchester City, basi wote wanaweza wasifike uwanjani maana wataishia kuchapana.

Mashabiki wa timu hizo mbili hawapendani na hii ni historia na chuki yao imeendelea kutambaa vizazi hadi vizazi. Wazazi wanawafundisha vijana wao kuonyesha chuki ya wazi dhidi ya timu nyingine.

Jeshi la Polisi London ndilo lililoitaka FA kuhakikisha timu hizo hazichezi London kwa siku moja kutokana na ugumu wa ulinzi wa kuzidhibiti. Lakini hata siku ya mechi yao iwe ni Islington au Haringey, polisi hujipanga hasa kwa kuwa wanajua mashabiki hao watatumia usafiri wa treni na mabasi kabla ya kufika uwanjani. Hivyo ulinzi mkali katika Jiji la London kila sehemu, kuhakikisha mambo yanaanza na kuisha salama.



Inaonekana chuki ya Spurs iko juu zaidi kwa kuwa eneo la Islington waliopo Arsenal, wanasema ni mali yao na kwa maana ya historia inaonyesha ni kweli kwa kuwa Arsenal ni wageni walihamia hapo. Uwanja wa White Hart Lane ambao sasa unajengwa, uko umbali wa takriban dakika 24 kwa gari binafsi, dakika 42 kwa usafi wa basi hadi eneo la Haringey.

Haringey na Isilington ni maneno yaliyo karibu kabisa. Tottenham ambao kiasili ndiyo wanatokea eneo hilo walianza kukerwa na ujio wa wageni Arsenal na baadaye wakawa na mafanikio makubwa na kuanza kujulikana huku wakitaka kuonyesha wao “ndiyo wenye London”.

Timu hizo zilikutana kwa mara ya kwanza Desemba 9, 1909 na Tottenham wakalala kwa bao 1-0. Kuanzia hapo Arsenal wakaanza kutamba wao ndiyo wenye mji, hilo lilichangia kuanzisha vita kubwa ya klabu hizo mbili.

Hadi sasa, Mwafrika, Emmanuel Adebayor raia wa Togo ndiye anayeongoza kwa kupachika mabao katika North London Derby baada ya kufunga jumla ya mabao 10, akiwa Arsenal na Tottenham. Jumla tangu mwaka 1909, timu hizo zimekutana mara 183, sare ni 51, Arsenal imeshinda mara 80 na Spurs imeshinda 62.



Baada ya kuwa nimeshuhudia lile tukio la fundi, niliwaona mashabiki watatu wa Arsenal katika eneo la Fisbury Park karibu na sehemu niliyokuwa nikiishi wakimvurumishia matusi shabiki wa Tottenham, kisa tu alipita karibu yao. Kitu kizuri hakuna aliyempiga mwenzake, lakini maneno makali ilikuwa balaa.


Hali hiyo imesababisha hata aina ya ukaaji wa maeneo hayo, mfano mashabiki wengi wa Tottenham wasingependa kuishi katika eneo la Islington na mara nyingi, kama ni zile nyumba za serikali ambazo hugawiwa kwa utaratibu maalum, mtu anaweza kutoa sababu ya ushabiki wake kwa Tottenham na asipelekwe Islington ikachukuliwa ni sababu ya msingi au wa Arsenal akakataa kuishi eneo la Haringey kwa sababu hizohizo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic