October 15, 2017



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amempongeza Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Ligi Kuu, Clement Andrew Sanga wa Young Africans kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa TPLB baada ya kupata kura 10 kati ya 16.

Katika  katika uchaguzi uliofanyika leo Oktoba 15, 2017 kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Mpinzani wa Sanga, Hamad Yahya Juma wa Mtibwa Sugar alipata kura sita kati ya 16 za Klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Wakati Sanga akichaguliwa kuwa Mwenyekiti, Shani Christoms Mligo wa Azam FC alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa TPLB. Shani aliyekuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo alipata kura 15 kati ya 16 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Nafasi tatu za kuwakilisha klabu za Ligi Kuu kwenye Kamati ya Uongozi zilivutia wagombea wawili; Hamisi Mshuda Madaki (Kagera Sugar) na Ramadhani Marco Mahano (Lipuli) ambao wote wameshinda. Madaki alipata kura 12 na Mahano 13.
Almasi Jumapili Kasongo kutoka Ashanti United FC ni mgombea pekee aliyejitokeza kuwania nafasi ya uwakilishi wa klabu za Ligi Daraja la Kwanza. Alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 35 kati ya 40 zilizopigwa.

Edgar William Chibura kutoka Abajalo FC alishinda nafasi ya Ujumbe kutoka Klabu za Ligi Daraja la Pili ambako zina nafasi moja kwenye Kamati ya Uongozi ya TPLB. Chibura alipata kura 35 kati ya 40.

“Natuma salamu zangu za pongezi kwa wote walioshinda. Nina imani nao kwamba tutashirikiana vema, kufanya kazi katika sekta ya mpira wa miguu, najua wanajua changamoto za ligi yetu hivyo naamini wataweza,” amesema Rais Karia mara baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Revocatus Kuuli kutangaza matokeo.

Mapema kabisa leo asubuhi, Rais Karia aliahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati mpya ya Uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) waliochaguliwa leo Oktoba 15, 2017.

Rais Karia aliyeambatana na Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura pamoja na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred alitoa ahadi hiyo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Baraza la TPLB uliofanyika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
“Tupo kwenye kikao hiki ambacho pia kitachagua viongozi wakaoongoza miaka minne ijayo, viongozi watakaochaguliwa leo kwa nia njema wataongoza Bodi kwa miaka minne…

“Bahati nzuri nilikuwa mmoja wa viongozi wa kwanza wa Bodi ya Ligi. Kwa hiyo najua changamoto tangu uundwaji wake. Hivyo nakifahamu chombo hiki vema, najua kwa undani malengo ya chombo hiki, lazima tuyafikie.
“…Lakini niwahakikishie tu kwamba hatutafika kama tutaendesha shughuli zetu bila uwazi, uadilifu na uwajibikaji,” amesema Rais Karia.

“Naahidi kuona kamba chombo hiki kipo huru. TFF itakuwa ikifanya monitoring. Tukiona mambo hayaendi sawa, hatutasita kukaa nanyi watu wa Bodi ili tushirikiane kuweka mambo sawa,  mvumiliane huku mkifuata taratibu,” amesema.

Rais Karia amesema kwamba uadilifu, uwazi na uwajibikaji upo zaidi kwa lengo la mpira wa miguu kuchezwa kwa weledi ili tupate mabingwa wa kweli  katika mashindano yanayosimamiwa na kuendeshwa na TFF.
Rais Karia aliasa viongozi wa klabu kubadilika na hasa kutoa ushirikiano kwa viongozi wa TPLB, “Nami nitatoa ushirikiano kwenu.”
Awali kabisa Mwenyekiti wa TPLB, Hamad Yahya akimkaribisha Rais Karia, aliwakaribisha viongozi wote waliohudhuria huku akiwapa pole kwa safari ndefu hadi kuja kwenye mkutano.
Baada ya matokeo, Yahya alirudi tena kuzungumza na Wajumbe ambako aliwashukuru kwa ushirikiano waliompa wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa TPLB na kuahidi, “Nipo bado kwenye mpira tutaendelea kushirikiana. Uchaguzi umekwisha, hakuna makundi.”

Kwa upande wake, Sanga alimshukuru Mungu na wajumbe wote kwa uchaguzi wa amani na utulivu, ishara inayompa nguvu kutekeleza vema majukumu yake mapya.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic