October 16, 2017




NA SALEH ALLY
HATIMAYE kile kilichokuwa kinasubiriwa na wadau wengi wa soka kimetimia baada ya Kaimu Mwenyekiti wa Yanga kushinda uchaguzi wa Bodi ya Ligi.

Sanga amemshinda Yahaya Mohammed aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo akipata kura 10 na mpinzani wake akabeba kura sita na kuangukia pua.

Hata kabla ya uchaguzi huo wa Bodi ya Ligi, ilionekana wazi Yahaya alikuwa akimhofia mpinzani wake na hii ilionyesha wazi kwamba alijua hakuwa amefanya mambo yake vizuri.
Bodi ya Ligi chini ya Yahaya haikuwa na ubora uliostahili hasa wakati lilipofikia suala la kuikosoa TFF au kufanya mambo kwa usahihi.

Bodi ya Ligi chini ya Yahaya ilionekana wazi haikuwa na uwezo hata wa kukosoa jambo lolote kuhusiana na ambacho walikuwa wakifanya TFF wakati huo rais akiwa Jamal Malinzi ambaye wakati wa uongozi wake alionyesha wazi kutofurahia kabisa masuala ya bodi ya ligi.

 Kawaida, Bodi ya Ligi inapaswa ijitegemee na kufanya mambo ya uhakika kuhusiana na kile ambacho kinapaswa kuifanya ligi kuwa bora na yenye hadhi inayopanda.

Wakati wa Malinzi, Bodi ya Ligi ilionekana ni kama tawi tu la TFF na ilifanya kile ambacho TFF ilitaka na wakati wa kufanya mambo kuyumba kwa kuwa TFF haikuwa na wa kuikosoa kutokana na kukosa kiongozi imara katika bodi hiyo.

Mimi niliamini Yahaya hakuwa imara kuhakikisha bodi hiyo inakuwa huru na imara kufanya mambo kwa ajili ya maendeleo ya soka nchini. Badala yake bodi ikaendelea kuwa chini ya TFF hivyo kuondoa umuhimu wa kuwepo kwa bodi hiyo.

Binafsi nimeona muda umepita lakini hakuna kikubwa ambacho bodi hiyo ilifanya kuonyesha kuwa ipo na imeleta jambo ambalo awali halikuwepo.

Kuingia kwa Sanga ni matumaini mapya, binafsi pia nilitamani kumuona anashinda na nilitamani kuona anaiongoza bodi hiyo ili kuleta changamoto mpya na kuisaidia kubadili mambo.

Huu ndiyo wakati mwafaka kwa kuwa Sanga amepata nafasi hiyo ambayo wapenda soka na hasa maendeleo wanaonekana kufurahia ushindi wake.

Lakini hata wapiga kura wanaonyesha walitaka Sanga ashinde, walitaka achukue nafasi hiyo ili kuleta maendeleo na mabadiliko ambayo chagizo litakuwa uongozi bora wa bodi hiyo uliopania kubadili mambo.

Kuna changamoto nyingi ambazo Sanga anapaswa kuanza kuzishughulikia na suala la viwanja vya kuchezea ni muhimu sana kwa kuwa limekuwa kikwazo cha kupiga hatua katika mpira wetu.

Waamuzi wamekuwa tatizo pia na miongoni mwao si waaminifu na inawezekana iko haja ya kuangalia mambo mengi kwa wale wasio waaminifu lakini maslahi yao ni jambo muhimu.

Yako mengi, lakini najua Sanga ni kati ya viongozi walioonyesha katika suala la uadilifu na uchapakazi akiwa Yanga. Hivyo huu ni wakati mwafaka wa kuhamishia suala hilo katika maendeleo ya mpira.

Sina hofu na Sanga katika suala la ushabiki, kwamba anaweza kupendelea Yanga. Ila nawaasa Wanayanga kuwa makini kwa kuwa ikifika hatapendelea wasimuite msaliti kwa kuwa anapenda kufanya kazi kwa uadilifu.

Kwa TFF inapaswa kumpokea Sanga kwa mikono miwili na kuyakubali mabadiliko ya Bodi ya Ligi na kumpa ushirikiano wa kuunda timu inayoweza kushirikiana kufanya makubwa kuleta maendeleo.

Ninaamini kwa uongozi wa Karia ambaye anaonekana amepania kuleta mabadiliko na Sanga ambaye anaonekana ni mchapakazi, huu ni wakati mwafaka kwa soka la Tanzania kuendelea.

Unganeni, leteni maendeleo na ikiwezekana kwenye makosa mpakubali na kupafanyia kazi. Tumechoka kudanganywa hivyo huu ni wakati sahihi wa mabadiliko. Namkabidhi Sanga kwa Karia.








0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic