March 3, 2018



WAKATI kikosi cha Simba kikijiandaa kucheza na timu ya Al Masry ya katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, klabu hiyo imempoteza mmoja wa wachezaji wake waliotamba huko nyuma.

Mchezaji huyo ni Arthur Mambeta aliyefariki Jumatano wiki hii, ambaye alipata kutamba na timu hiyo mwanzoni mwa miaka ya 1960 wakati ilipokuwa ikijulikana kwa jina la Sunderland mpaka katikati ya miaka ya 1970, ikiwa tayari imebadilishwa jina na kuitwa Simba.

Kwa wapenzi wa soka wa miaka ya 1960-1974, jina la Mambeta siyo geni masikioni mwao, wengi watakuwa wamelisikia lakini pia wale wa sasa nao watakuwa wanalijua.

Mambeta alikuwa ni kati ya viungo washambuliaji mahiri waliowahi kutokea katika timu ya Simba na Taifa Stars, waliokuwa na uwezo wa kipekee wa kutandaza soka.

Aliitumikia Simba kwa moyo wa kipekee na kufanikiwa kuiandika rekodi mbalimbali timu hiyo ambayo kwa sasa inashika nafasi ya kwanza katika Ligi Kuu Bara.

Rekodi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara 18, ambayo Simba inaishika hivi sasa, Mambeta ni mmoja kati ya wachezaji aliojitoa kwa nguvu zao kufanikisha hilo kabla ya kustaafu mwaka 1974.

Ubingwa ambao Simba iliupata mwaka 1965, 1966 na 1973, Mambeta ni kati ya wachezaji walioiwezesha timu hiyo kunyakua ubingwa huo.


ALICHEZEA TIMU YA AFRIKA MASHARIKI
Lakini ukiachana na Simba, Mambeta ambaye alizaliwa Oktoba 23, 1943 huko Ludewa mkoani Njombe, alifanya mambo makubwa akiwa na Taifa Stars ambapo mwaka 1969 alichaguliwa kuwa miongoni mwa wachezaji wachache kutoka Tanzania kwa ajili ya kuunda timu ya Afrika Mashariki iliyokuwa ikishiriki michuano mbalimbali ya kimataifa.

Akiwa na kikosi hicho cha Afrika Mashariki alikuwa ni mmoja kati ya wachezaji wa  kikosi cha kwanza cha timu hiyo akicheza nafasi ya mshambuliaji mwenza.

AKATWA MIGUU YOTE
Hata hivyo, pamoja na yote hayo, leo hii nyota huyo ambaye alikuwa alama na nembo kubwa ya klabu ya Simba na Taifa hili hayupo nasi tena baada kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Temeke.

Mpaka mauti yamfika, Mambeta hakuwa na miguu yake yote miwili ambayo alikuwa akiitumia kwa ajili ya kuijengea heshima Simba na taifa la Tanzania.


CHAMPIONI LILIWAHI KUMTEMBELEA
Kabla ya kufikwa na mauti Jumatano wiki hii, Gazeti la Championi liliwahi kumtembelea nyumbani kwake Kigamboni, Kibugumo jijini Dar es Salaam kumjulia hali baada ya kupata taarifa zake za kupoteza miguu yake yote miwili.

Mambeta yule ambaye aliyekuwa na umbo lenye miraba minne na aliyekuwa akiongea kwa kujiamini kwa kutumia Lugha ya Kiswahili na Kingereza, alikuwa akiongea kwa huzuni na mara kwa mara machozi yakimtoka.

KILICHOMUUA HIKI HAPA
Kabla ya mauti kumfika, Mambeta aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba, alianza kuhisi maumivu katika mguu wake kushoto na baadaye ukaanza kuota vitu kama fangasi kwenye vidole.

Alisema alipokuwa akivikuna alihisi maumivu makali hivyo ilimbidi aende Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Baada ya kufika huko na kufanyiwa uchunguzi aliambiwa kuwa ana Ugonjwa wa Gangrene na ulikuwa tayari umeshamshambulia sana kwani madakitari walimwambia kuwa tayari mguu ulikuwa umeshaoza ndani kwa ndani.

Wakamshauri mguu ukatwe kama anataka kuendelea kuishi vinginevyo angekufa, bila ya wasiwasi wowote alikubaliana nao kwani bado alikuwa anapenda kuishi.

Alikatwa mguu huo na baada ya wiki mbili aliruhusiwa kurudi nyumbani kuendelea na maisha yake lakini baada ya mwaka mmoja tatizo hilo lilijitokeza pia katika mguu wake pili.

Mdogo wake aliyekuwa akiishi naye akampeleka tena Muhimbili ambako alikatwa mguu huo kwani ulikuwa unampa mateso makubwa hasa nyakati za usiku.

Hata hivyo, wakati alipokuwa Muhimbili madaktari walimweleza mara nyingi ugonjwa huo huwapata wanamichezo kwani wakati wanafanya mazoezi mwili huwa na uwezo mkubwa wa kutengeneza damu nyingi, ambapo mishipa ya mwili nayo hutanuka na kuruhusu damu kupita kwa wingi.

Sasa wanapochacha mazoezi, mishipa husinyaa lakini uwezo wa mwili kutengeneza damu nyingi unabakia palepale.

Kutokana na hali hiyo uwezo wa mshipa kupitisha damu kama zamani hupungua jambo ambalo husababisha damu kusimama sehemu moja kisha hutengeneza usaa na sehemu hiyo kuoza.

USHAURI WAKE KWA WANASOKA KABLA YA KIFO 
Aliwataka wanasoka kupendana na kusaidiana wakati wa shida na raha kwani yeye ni kama vile walikuwa wamemtenga, kwa hiyo hakupenda kitu kama hicho kitokee kwa mtu mwingine.

Pia aliwataka wanasoka kuwa na tabia ya kufanya uchunguzi wa afya zao kila wakati ili kuepukana na matatizo ambayo hapo baadaye yanaweza kuwasababishia mateso makubwa kama ilivyokuwa kwake. 

Mambeta anatarajiwa kuzikwa leo jijini Dar es Salaam. 

SOURCE: CHAMPIONI


1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic