May 18, 2018






NA SALEH ALLY
LIGI Kuu Tanzania Bara ndiyo inakwenda ukiongoni, kama ni vita basi ni ile inayofanana na Ligi Kuu England.

Kabla ya mechi kwisha, Ligi Kuu England maarufu kama EPL ilikuwa imeishapata ubingwa. Suala la kugombea nafasi likabaki katika nafasi ya nne na zile timu zitakazoteremka daraja.

Hivyo kila mmoja alikuwa akimjua bingwa ni yupi, lakini likabaki suala la timu nne za juu na timu tatu zinazoshuka daraja.

Kwa Ligi Kuu Bara, bingwa akiwa amejulikana kama ya mechi tatu kabla lakini ukweli unaonyesha hivi; kuna timu zinazopambana kujiokoa kuepuka kuteremka daraja.


Kila timu inapambana kuhakikisha inabaki ligi kuu kwa kuwa kuna umuhimu na faida zake na kumbuka kuna timu zinapambana kuipata nafasi hiyo.


Wakati timu hizo zikiwa zinapambana, ligi ndiyo inaisha hivyo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapaswa kujiuliza na ikiwezekana kushirikiana na uongozi wa waamuzi kwamba kiwango cha waamuzi kilikuwa vipi.


Lazima TFF ilifanyie kazi suala la waamuzi, lazima kuwe na ukaguzi na kiwango kikubwa kupitia wataalamu wa waamuzi.

Kumekuwa na malalamiko mengi na yanayochosha kuhusiana na waamuzi. Inawezekana ikawa ni kelele za wale wanaoshindwa na wakaona hawana wakilalamika watapoza machungu yao.


Lakini kuna ukweli kuhusiana na waamuzi kuwa na kiwango duni na tumeona katika Ligi Kuu Bara kaitka mechi nyingi ambazo waamuzi waliboronga na kusababisha lawama za mfululizo.

Si sahihi kuzipuuza lawama hizo wala si jambo jema kulichukulia suala hilo ni kama la watu tu walioamua kulalamika.


Kusikiliza ni moja ya jambo muhimu sana, inawezekana watu wanajua mambo mengi zaidi na wanaweza kuwa msaada kama wataona umekuwa ukiwasikiliza.


Suala la kutoajiamini, umakini mdogo na ushirikiano duni kati yao lakini inawezekana hata vishawishi pia kwa kuwa wao ni wanadamu, inawezekana ikawa ni sehemu ya mambo yanayochangia mambo kwenda mlama.

Lakini kama kutakuwa na mafunzo zaidi, mipango sahihi na kuendelea kukemea yasiyo sahihi kama waamuzi kujali ushabiki, inawezekana kabisa ikaisaidia tena nafasi ya waamuzi kuendelea kuwa muhimu badala ya kuendeshwa na hisia au matakwa yao.

Waamuzi ni muhimu na wanategemewa, waamuzi ni watu wasipokuwa makini wanaharibu vitu na wanaweza hata kusababisha maafa.



Muongozo wa waamuzi ni sheria ambazo si jambo geni, lakini wako wamekuwa wakipotea na kuzifanya kama sheria 17 za soka hazina maana.

Kwa maana ya ukombozi, basi hakuna anayeweza kuusaidia mpira wa Tanzania katika suala la haki kama waamuzi.


Lakini kwa kuwa wao watakuwa wameshindwa na suala hilo, linaendelea kuonekana ni sugu, basi TFF wanatakiwa kuweka nguvu yao na kuhakikisha tunakuwa na waamuzi bora ambao hawatabaki nyumbani tu badala yake wafanikiwe kimataifa.

Rwanda walioanza kucheza mpira juzi, leo wanasifika kwa kuwa na waamuzi bora na wanaopata nafasi nyingi za kucheza michuano ya kimataifa chini ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na lile la Afrika (Caf).

Faida wanazozipata ni kuendelea kuukuza mpira wao, pia kujitangaza kwa ubora na uhakika wa weledi.


Kuna sababu ya kuona wivu wa maendeleo na wewe kujifunza na ikiwezekana kufanya vizuri kama wale wanaofanya vema.

Pia si sahihi kwa nchi kama Rwanda kuwa mfano katika suala la soka ambalo Tanzania imekuwa mbele miaka nenda rudi.

Waamuzi wanatakiwa pia kuwa ni watu wenye wivu wa kimashindano, wanaotamani kufanya vizuri na pia kuhakikisha wanaepuka vishawishi na kuangalia matokeo ya mwisho ya kazi zao ambayo wakifanya vizuri, faida inakuwa yao binafsi na taifa letu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic