Uwezekano wa kiungo mkabaji wa Simba, Said Ndemla kuichezea timu hiyo ni mdogo. Ni baada ya kupata ofa ya kwenda kufanya majaribio Ulaya.
Kiungo huyo, hivi sasa anavutana na timu yake hiyo katika kuongeza mkataba mpya wa kuichezea ambao ulimalizika mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Awali, kiungo huyo alikuwa anavutana na Simba katika dau la usajili ambalo aliwekewa shilingi milioni 50 huku mwenyewe akitaka milioni 70 kabla ya baadaye kuleta hoja nyingine ya kuomba mkataba wake uboreshwe kwa kutaka acheze mechi.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, kiungo huyo ameomba asaini mkataba wa awali ‘pre contract’ na hatma ya kusaini mkataba wenyewe kamili itajulikana katika matokeo ya majaribio yake.
Mtoa taarifa huyo alisema, taarifa za klabu ipi anakwenda kuichezea inafanywa siri na uongozi wa Simba inayopambana kuhakikisha wanambakisha kiungo huyo.
Aliongeza kuwa, Simba wamepanga kumsainisha mkataba huo wa awali leo Jumatatu baada ya pande mbili kukubaliana kwa maana ya uongozi na mchezaji mwenyewe.
“Ndemla alitakiwa asaini mkataba juzi (Ijumaa) lakini ikashindikana ni baada ya kupishana viongozi na mchezaji mwenyewe na kikubwa lilikuwa ni suala la muda pekee.
“Alitakiwa asaini mkataba wa awali ambao ameandaliwa na uongozi na atasaini mkataba huo kesho Jumatatu kabla ya kwenda Ulaya ndani ya wiki hii kwenye majaribio,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye alipoulizwa atakwenda nchi gani Ulaya akasema hana uhakika. “Nadhani ni kati ya Ufaransa na Sweden,” alisema.
“Hatma ya kusaini mkataba wenyewe kamili Simba tofauti na huo wa awali itajulikana baada ya majibu ya majaribio yake atakayoyafanya.
“Na uongozi ungeweza kumuachia kwenda kwenye majaribio hayo bila kumsainisha mkataba huo wa awali lakini wanahofia kumruhusu Ndemla kwenda huko bila ya kumpa mkataba kwa kuihofia Yanga,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Ndemla ambaye alikuwa ameshamaliza mkataba wake Simba, kuzungumzia hilo alisema “Bado sijasaini mkataba Simba, hivi sasa tupo kwenye mazungumzo ya mwisho kabla ya kusaini mkataba huo.
“Kuhusiana na taarifa za kwenda kwenye majaribio Ulaya ni kweli ninatarajia kwenda kwenye majaribio nje ya nchi na klabu nitakayokwenda ni mapema kuweka wazi hivi sasa,” alisema Ndemla.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment