Imefahamika kuwa sherehe ya kumvalisha pete mchumba wake ndiyo imemzuia kiungo mshambuliaji wa Singida United, Deus Kaseke kusaini mkataba Yanga.
Mshambuliaji huyo, alitakiwa asaini mkataba huo Jumamosi iliyopita baada ya pande mbili Singida na Yanga kufikia muafaka wa kumsainisha kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kukaba na kushambulia.
Kaseke alijiunga na Singida msimu uliopita kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Yanga baada ya mkataba wake kumalizika.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, kiungo huyo anatarajiwa kusaini mkataba huo kuanzia leo baada ya kukamilisha zoezi hilo.
“Kaseke na Yanga wamefikia makubaliano mazuri ya kiungo huyo kusaini mkataba, kikubwa kilichozuia ni sherehe ya kumvalisha pete mchumba wake ambayo ilifanyika wikiendi iliyopita.
“Hivyo, Kaseke wakati wowote kuanzia kesho (leo) atasaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea Yanga baada ya kufikia makubaliano mazuri,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Kaseke kuzungumzia hilo alisema: “Ni kweli nipo kwenye mazungumzo mazuri na Yanga kwa ajili ya kusaini mkataba lakini ilishindikana kusaini kutokana na sherehe yangu ya kumvalisha pete mchumba wangu.
“Hivyo, wakati wowote nitasaini mkataba wa kuichezea Yanga na nimepanga kufunga ndoa Mei, mwakani baada ya ligi kumalizika,” alisema Kaseke.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment