Kiungo wa zamani wa klabu ya Yanga, Abdi Kassim 'Babi' amesaini mkataba wa kuitumikia timu ya Mawenzi Market inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza mkoani Morogoro.
Babi ambaye anakumbukwa kwa kuandika rekodi ya kufunga bao lake la kwanza katika Uwanja mpya wa taifa wakati Taifa Stars ilipomenyana na Uganda, amefikia makubaliano na Mawenzi ili kuipandisha Ligi Kuu.
Kwa muda mrefu sasa Morogoro imekuwa na timu moja pekee ambayo ni Mtibwa Sugar ingawa miaka kadhaa nyuma kulikuwa na Moro United ambayo ilishuka daraja.
Babi ambaye aliwahi kutamba na kikosi cha Yanga mwaka 2007 alipojiunga nacho akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, amekabidhiwa majukumu ya kuipandisha ligi kuu Mawenzi ili iweze kuungana na Mtibwa kwa ajili ya kuongeza hamasa ndani ya mkoa huo.
Wakati Babi akikabidhiwa majukumu hayo, kikosi chake cha Mawenzi Market kitakutana na Yanga Agosti 12 katika mchezo maalum wa kumuaga beki mkongwe wa Yanga, Nadr haroub 'Cannavaro' ambaye amestaafu kucheza soka na sasa amekabidhiwa majukumu ya Umeneja wa Timu.
Hapo mmemdharau Canavaro kuagwa na kitimu ambacho hakina jina wala umaarufu wowote
ReplyDelete