September 12, 2018


Mwaka 1994, ndipo rasmi mashindano ya Miss Tanzania yalianza Bongo na mshindi wa kinyang’anyiro hicho alikuwa ni Aina Maeda.  Miaka 14 sasa imekwishakatika tangu mashindano hayo yaanze nchini na tumeshuhudia kinyang’anyiro hicho kikizalisha mastaa kibao.

Baadhi yao wanaofahamika kwa sasa ni Millen Magese, Faraja Kotta Nyalandu, Nancy Sumari, Wema Sepetu, Jokate Mwegelo, na Diana Edward Lukumai ambaye juzi (usiku wa kuamkia Jumapili) alikabidhi taji hilo kwa mshindi wa kinyan-g’anyiro hicho mwaka 2018, Queen Elizabeth Makune.

Lakini mashindano ya mwaka huu yameandika rekodi mpya kadhaa, kwanza tangu kuanza kwake kwa mara ya kwanza yameratibiwa na aliyewahi kushiriki mashindano haya, Basilla Mwanukuzi ambaye pia ni mshindi wa Miss Tanzania 1998, akitokea Kinondoni.

Rekodi nyingine ambayo imeandikwa kwenye mashindano haya ni kwamba Mwanukuzi akiratibu mashindano haya akiwa Miss Tanzania aliyetokea Kinondoni, mshindi wa mwaka huu, Queen Elizabeth katokea Kinondoni. Umeona mambo hayo!

Sasa tukirudi kwa Diana ameshikilia taji la Miss Tanzania kwa miaka mitatu, tangu mwaka 2016 mpaka 2018 kwa sababu mwaka jana mashindano haya hayakufanyika. Baada ya kukabidhi taji kwa mshindi wa mwaka huu, Risasi Vibes, liliamua kupiga naye stori mbili-tatu ili kuweza kufahamu ‘experience’ yake akiwa na taji hilo na kusikia maoni yake kwenye mashindano ya mwaka huu na nini anamshauri Queen Elizabeth!

Risasi Vibes: Diana nini maoni yako katika mashindano ya mwaka huu?

Diana: Binafsi ni mashindano bora na nimeyafurahia kiukweli. Ninampongeza mratibu Basilla Mwanukuzi, nina uhakika kutokana na muitikio wa mashindano kwa mwaka huu atakuwa amejifunza nini cha kuboresha.

Risasi Vibes: Wengi wanaponda kuhusu zawadi ya mshindi (gari aina ya Daihatsu Terios), wewe maoni yako ni yapi?

Diana: Zawadi ni zawadi na sioni tatizo kwenye hilo. Kikubwa ni heshima unayopewa, kuwa mrembo wa Tanzania, ni ndoto mtu unakuwa nayo. Unapoifikia unahisi amani ya moyo na una kila kitu kuliko hata zawadi unayopewa.

Risasi Vibes: Umekabidhi taji lako kwa mshindi, nini ushauri wako kwake?


Diana: Ninamshauri ‘afocus’. Changamoto zitakuwa nyingi. Watu watamtukana na mambo mengine mengi, kikubwa anatakiwa kufahamu kwamba yeye ndiye mshindi na ndiye anastahili. Anaweza kujifunza mfano hata kutoka kwangu. Nilitukanwa sana, kwa kipindi cha miaka mitatu lakini nilichozingatia ilikuwa ni kwamba mimi ndiye mshindi na ndiye ninastahili, basi.

Risasi Vibes: Mbali na kutukanwa kipi hutakisahau baada ya kutangazwa mshindi wa Miss Tanzania?

Diana: Nafikiri hilo ndilo kubwa kwa upande wa changamoto. Lakini pia nilikuwa nina furaha isiyopimika.

Risasi Vibes: Nini umefanya kwa ajili ya jamii wakati unashikilia taji hilo?

Diana: Nimeendesha kampeni ya HGM Dondosha Wembe. Ni kampeni iliyofanyika kaskazini na inahusu ukeketaji. Yapo pia mambo mengine mengi tu tumefanya kwa ajili ya jamii.

Risasi Vibes: Tangu uwe Miss nini kimebadilika kwenye maisha yako?

Diana: Kwanza nimepata heshima kubwa. Nimepata madili mengi, pesa na mambo mengine ni changamoto. Kwa mfano kwa sasa mimi ni mwanafunzi, shuleni kila mtu anakushangaa, ukifanya kitu, utasikia kafanya yule Miss Tanzania na hata kwenye jamii. Kila unachofanya vyombo vya habari vinakumulika kwa sababu ni Miss Tanzania.

Risasi Vibes: Unasoma chuo gani?

Diana: Nasoma IFM.

Risasi Vibes: Unasomea nini?

Diana: Nasomea masuala ya kodi.

Risasi: Vipi kuhusu uhusiano, naona una pete ya uchumba, umechumbiwa tayari?

Diana: Hapana, ni hali ya kuweka tu vikwazo, si unajua tuna mambo mengi ya kufanya. Bila hivi kila mtu atakufuata awe na wewe.

Risasi Vibes: Una kipi cha kumalizia?


Diana: Mashindano ya mamiss ni yetu sote kama taifa. Kunapokuwa na changamoto ‘tuzi-adress’ kama changamoto lakini isiwe jambo la kuponda na kumkatisha tamaa mtu au watu wanaokuwa wanaratibu. Ikumbukwe kuwa mashindano haya yanaipeperusha bendera ya taifa hadi kimataifa.

CHANZO: RISASI VIBES

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic