POGBA, NACHO, WALCOTT, BALOTELLI: TETESI KUBWA ZA SOKA ULAYA LEO JUMATANO
Juventus watajaribu kumnunua tena nyota wa Ufaransa anayeichezea Manchester United Paul Pogba mwenye miaka 25 mwezi Agosti mwaka ujao. Mabingwa hao wa Italia pia wanataka kumnunua beki wa Brazil, Marcelo, mwenye miaka 30 ambaye kwa sasa huwachezea Real Madrid (Tuttosport)
Barcelona wanajiandaa kuwanunua mabeki kamili wa Uhispania Nacho Monreal, 32, na Alberto Moreno, 26, ambao huchezea Arsenal na Liverpool mtawalia. (Mundo Deportivo)
Kiungo wa kati wa Ujerumani anayechezea Manchester City Ilkay Gundogan, 27, yuko radhi kuwakataa Barcelona ambao wanataka kumnunua mwezi Januari na badala yake kuanzisha mazungumzo kuhusu mkataba mpya katika klabu hiyo ya Etihad. (Sun)
Mkabaji wa Arsenal na Uswizi Stephan Lichtsteiner, 34, amepuuzilia mbali taarifa kwamba anapanga kustaafu. Amedai kwamba anahisi mwili wake ni kama wa kijana wa miaka 28. Lichtsteiner amechezeshwa mara moja pekee kama nguvu mpya na Gunners tangu ajiunge nao kutoka Juventus mwezi Juni. (Daily Mail)
Mkurugenzi wa michezo wa Atletico Madrid Andrea Berta anaongoza miongoni mwa wanaotarajiwa kujaza nafasi mpya ya mkurugenzi wa uchezaji soka katika klabu ya Manchester United. (London Evening Standard)
Uwezekano wa John Terry kuhamia Spartak Moscow umeingia mashaka. Beki huyo wa zamani wa Chelsea na England mwenye miaka 37 alikuwa ameafikiana masharti ya mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo, ambapo angekuwa analipwa £1.8m, kukiwa na uwezekano wake kuongezewa mwaka wa pili.
Lakini sasa vyombo vya habari Urusi vinaripoti kwamba mpango wake umesimamishwa kwa muda huku familia yake ikiwa na wasiwasi kuhusu kuhamia Moscow. Kwa muda sasa kumekuwa na uhasama kati ya Urusi na Uingereza (Mirror)
Klabu ya Fenerbahce ya Uturuki inataka kumteua meneja wa zamani wa Sheffield Wednesday ya Uingereza Carlos Carvalhal kuchukua nafasi ya Mholanzi Phillipe Cocu, 47, ambaye amewaongoza kwa mechi tisa pekee. Mreno Carvalhal , 52, hajapata kazi tangu alipoondoka Swansea City baada yao kushushwa daraja kutoka Ligi ya Premia mwezi Mei. (Sky Sports)
Mshambuliaji wa zamani wa Manchester City na Liverpool Mario Balotelli, 28, alikuwa na uzani wa kilo 100 alipofika kwa mazoezi ya kujiandaa kwa msimu mpya katika klabu ya Nice ya Ufaransa. Uzani huo ni kilo 12 zaidi ya uzani wake rasmi. (L'Equipe)
Kutoka BBC
0 COMMENTS:
Post a Comment