SIMBA WAJIANGALIE KABLA YA HAYA KUTOKEA
Na John Joseph
Simba imesajili kikosi cha bei ghali, Simba ina kocha mkali kutoka Ubelgiji, Simba ina mastaa wengi, Simba ni kama timu ya taifa, Simba kuna neema kutokana na uwepo wa Mo Dewji, Simba ndiyo mabingwa watetezi, Simba wana Ofisa Habari anayejua kuongea…
Kuna sifa nyingi ambazo unaweza kuzitoa kwa Simba hii ya sasa na kweli kwa kiasi fulani wanastahili kwa lengo ya soka letu la Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla.
Ushiriki wao uwanjani katika michuano ya kimataifa haukuwa mzuri sana lakini hata walivyotolewa siyo kwa aibu au kama timu ambayo haikuwa na maandalizi bali ni matokeo ya kuzidiwa kidogo na wapinzani wao.
Ni kweli kama klabu imekuwa na neema nzuri kuliko ilivyokuwa kwa majirani zao ambao ni wapinzani wao wa jadi, Yanga. Hilo lipo wazi na halina ubishi lakini naitazama hali hii ambayo naweza kusema ni kama ‘ufalme’ wa Simba katika jicho la tatu na kuona kama kukokosekana umakini kuna tatizo kubwa linaweza kutokea hapo mbeleleni.
Pale juu katika aya ya kwanza niliweka nukta tatu nikimaanisha kuna sifa nyingi ambazo zinaendelea wanastahili kupewa, lakini tayari kuna uchaguzi unakuja, upande wa pili ushindani huwa uwanjani nao umeanza kuonekana kuwa mkali.
Simba walipata suluhu dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara, ni matokeo ambayo hayakutegemewa na Wanasimba wengi hasa ikizingatiwa kuwa kikosi chao kiliingia kikiwa kamili, hakukuwa na kisingizio chochote, upande mwingine kocha wao msaidizi, Masoud Djuma ambaye imekuwa ikisema yupo kwenye ‘kaa la moto’ la kutimuliwa, naye alibaki Dar wakati mchezo ukichezwa Mtwara.
Baad aya matokeo hayo kumekuwa na lawama kadhaa kuhusu ubora wa kocha, japo ni mapema sana hilo kutokea lakini hiyo ndiyo kawaida ya mashabiki wa soka popote duniani hasa Tanzania, huwa ni lazima watafute ‘wakufa’ naye.
Safari hii Simba wapo Mwanza, Djuma kabaki tena Dar, wao wanasema ni sehemu ya mipango yao, lakini hii inatokea Tanzania pekee, kocha mkuu anasafiri na timu kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu kisha msaidizi wake anabaki kusimamia mazoezi ya wale ambao hawajasafiri na timu.
Ukiliweka hilo pembeni, tayari kuna vuta nikuvute juu ya uchaguzi wao mkuu ambao mamlaka ya juu ya soka imeshaingilia na kuchukua hatua ya kuusimamisha.
Shirikitisho la Soka la Tanzania (TFF) limedai kuna kanuni zimekiukwa hasa katika masuala ya ada ya fomu kwa wagombea, unajiuliza katika akili ya kawaida hao wasimamizi wa uchaguzi hawakujua kiwango cha ada stahiki au walifanya makusudi! Unajiuliza pia jinsi wagombea walivyokuwa wakisuasua kuchukua fomu kwa klabu yenye hadhi kubwa kama Simba!
Wakati hayo yakitokea kuna taarifa ambazo siyo rasmi kuwa kumekuwa na mvutano wa chinichini wa kiutawala kuhusu uchaguzi huo, japokuwa hazina uthibitisho lakini kama kweli zipo dalili siyo nzuri.
Kwa picha ninavyoiona kipindi hiki, ikitokea timu yao ikapoteza mchezo au kushindwa kupata ushindi huku upande wa pili yaani Yanga wakashinda, haitakuwa ajabu kuona kukiibuka mvutano mkubwa zaidi na wa wazi.
Hivyo, kuepuka yote hayo ni vema Wanasimba wenyewe wakatambua kuwa, kama ni kikosi wanacho kizuri, usajili ulifanyika vizuri na walipata muda mzuri wa kuweka kambini hivyo upepo mchafu wa muda mfupi hautakiwi kuwapotezea dira, watambue imewachukua miaka mingi kurejea kwenye mstari waliopo sasa hivi.
Michuano ya Afrika ilikuwa ni ndoto kwa miaka kadhaa ya hivi karibuni, Simba watashiriki tena msimu ujao katika michuano ya kimataifa, hivyo wanatakiwa kuwa na kikosi imara ambacho ili kiwe bora ni vema uongozi wa klabu nao ukawa imara.
Imara sio kuweka nguvu tuu.. Bila kutumia akili utafeli
ReplyDelete