TUACHE KUIBEZA TAIFA STARS, VIJANA WAMEFANYA KWELI
Ligi Kuu Bara bado haijashika sana kasi, lakini kwa namna ilivyoanza, inatoa matumaini kwamba hapo baadaye ushindani utakuwa mkubwa sana kutokana na hivi mwanzo tu timu kutokubali kupoteza mechi kirahisi.
Ingawa kuna changamoto ya kukosekana kwa mdhamini mkuu, lakini timu zinapambana. Hofu yangu ni kwamba, hapo baadaye wachezaji wanaweza kushuka morali kutokana na kukumbwa na ukata kwenye timu zao na ile hali ya kupambana ikapotea. Ligi ikakosa msisimko.
Ni vema juhudi zikaendelea kufanyika kwa kasi kubwa ili mdhamini mkuu apatikane kuja kuokoa jahazi hili ambalo binafsi naona siku si nyingi linaweza kuzama.
Mwishoni mwa wiki hii ligi hiyo itaendelea, hiyo ni baada ya kusimama kwa muda kidogo kupisha michezo ya kimataifa ambayo ipo kwenye Kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Katika kalenda hiyo, kwa timu za Afrika zilikuwa zikicheza mechi za kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) ambapo Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, yenyewe ilicheza dhidi ya Uganda na kutoka suluhu.
Suluhu hiyo ya ugenini si mbaya kwetu kwa sababu timu nyingi ambazo zimekuwa zikipambana na Uganda kwenye uwanja wao wa nyumbani, sare imeonekana ni kama ndio ushindi kwa wengi, lakini zingine zinaambulia kipigo.
Vijana wetu walifanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha wanaambulia pointi wakiwa ugenini, kweli wakafanikiwa kufanya hivyo na wamerudi wakionekana ni mashujaa ingawa hawakuweza kupata pointi zote tatu na badala yake wakaipata moja.
Jitihada za wachezaji wetu tumeziona hasa katika kuhakikisha kwamba wanafanikiwa kupata ushindi, lakini haikuwa hivyo.
Kwa hatua ambayo wameweza kufikia ilihali ikiwa ni kikosi kilichoongozwa na kocha mpya, Emmanuel Amunike, kwa kweli kazi kubwa ilifanyika licha ya awali baadhi ya mashabiki kuonekana kuikacha kuipa sapoti timu hiyo.
Kwa wale ambao walikuwa wanadhani kwamba mwalimu atapotea basi sasa ni muda wa kurudi kwenye mstari na kuendelea kumpa sapoti ili aweze kufanya yale ambayo ana imani nayo yataweza kusaidia timu.
Hivyo kwa kuunga mkono juhudi zake itasaidia kuleta chachu ya ushindani hasa kwa timu yetu ambayo bado ina safari ndefu ya kuweza kufanya vizuri kimataifa, hivi sasa kazi ndiyo kwanza imeanza.
Napenda kuwapa rai wachezaji wa kikosi hicho kwamba siri ya mafanikio imefichwa sehemu ambayo hauwezi kuifikiria kwa haraka, hivyo ni jukumu lenu kuhakikisha kwamba mnazingatia kile ambacho mnaambiwa cha kufanya wakati husika.
Mnapaswa muumize vichwa katika kupambana kwa ajili ya maslahi ya taifa na kwa kufanya hivyo itasaidia kuweza kupata ushindi kwa kila mpinzani ambaye tutakutana naye kwa kuwa tumeonyesha kwamba nasi tunaweza.
Nidhamu ni kitu cha msingi sana kwa wachezaji wetu hasa wa ndani ambao wana safari ndefu kuhakikisha wanafikia yale malengo ambayo wanayahitaji hasa kwa wakati huu ambao mpira ni zaidi ya ajira kwa vijana wengi.
Wengi sana wamefanikiwa kupitia mpira kwa kuwa walikuwa na nidhamu na waliamini katika kutumia uwezo walionao hasa kupambana kwa hali na mali bila kujali matatizo ambayo wanapitia, hivyo kikubwa ni kuwa na nia na kutazama kule ambako unataka kwenda.
Imani yangu ni kwamba yale matatizo ambayo yalitokea wakati uliopita kwa sasa hatutayaona tena kwa kuwa somo litakuwa limewapata vilivyo wachezaji na maumivu ya kutoitumikia timu yao wameyapata.
Nikimalizia na ligi kuu, rai yangu kubwa timu zijiandae kisaikolojia kuhakikisha kwamba ugumu ambao wanapitia usiwafanye wakalegeza kama na kuanza kupata matokeo mabaya ambayo hayaleti tija.
Pia matokeo yakiwa mabaya kwa timu nyingi yanaua ile ladha ya ushindani ambayo ilianza kuonekana kwenye ligi hiyo ambayo wengi wanaifuatilia kwa hapa nyumbani.
Matokeo ya uwanjani yanategemea maandalizi mazuri mkiwa nje ya uwanja kwa muda sahihi na wachezaji kutambua kwamba wapo kwenye ushindani na sio kuleta utani na kazi zao wanazofanya.
0 COMMENTS:
Post a Comment