October 12, 2018


DAR ES SALAAM: Aidan Magawa ambaye ni kaka wa mtayarishaji Yoshua Mwisho ‘Pancho Latino’ aliyefariki juzi wakati akiogelea, amesema mdogo wake alikutwa na umauti akiwa katika kazi zake kisiwani Mbudya.

Akizungumza na Ijumaa, alisema mdogo wake amekuwa akifanya kazi za sanaa kwa muda mrefu na alikuwa kisiwani hapo katika moja ya mihangaiko yake.Magawa alisema familia yake imesikitishwa na walioripoti kuwa ndugu yao alifikwa na umauti akiwa ‘anakula bata’ kwani ukweli ni kwamba alienda kwenye kikao cha kazi na baada ya kumaliza aliamua kuogelea.

“Si sahihi kumuongelea vibaya marehemu wakati ukweli hawaufahamu, mdogo wangu alikwenda kwenye kazi zake na baada ya hapo akaamua kuogelea, lakini kwa kuwa siku yake ilifika akafariki, nawaomba Watanzania wamuombee badala ya kumzungumzia mambo mabaya,” alisema Magawa.

Naye baba wa marehemu, Mchungaji Simon Magawa, alisema alipokea taarifa hizo za msiba juzi majira ya saa mbili usiku kupitia mitandao ya kijamii. “Nilipoona kwenye mitandao, nikampigia kaka yake aliyepo huko Dar, Aidan akaniambia ni kweli,” alisema.

Alisema mara ya mwisho aliwasiliana na marehemu siku moja kabla ya kutokea kwa tukio hilo na walizungumza mambo ya kawaida hadi pale alipokuja kupata taarifa za kifo siku iliyofuata. Alisema marehemu mara ya mwisho kufika kijijini kwao Msingisi, Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, ilikuwa ni miezi miwili iliyopita.

Kuhusu maziko ya mtayarishaji huyo aliyetengeneza nyimbo maarufu kama Dar es Salaam Stand Up wa Chid Benz na Closer wa Vannesa Mdee, Aidan alisema mwili wa mdogo wake utasafirishwa leo kwenda kwao Gairo mkoani Morogoro kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika kesho.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic