October 13, 2018


DAR ES SALAAM: Mwanamuziki Mbaraka Mwishehe (marehemu) amewahi kuimba: “Kwanza jiulize kwa nini hupendeki siku hizi mamaaa, bembeleza bwanako muishi pamoja usitumie dawaaa!”  

Ujumbe wa wimbo huo ni mzuri kwa wanawake na wanaume lakini wengi wamekuwa wakiupuuza na kujikuta eti wanakwenda kwa waganga kutafuta dawa ya mapenzi kama mrembo mmoja alivyonaswa hivi karibuni akiwa kwa mganga akimroga mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ili amuoe.

Mahali alikonaswa na Amani ni Magomeni jijini Dar ambako mganga huyo anayetajwa kuwarekebishia mambo yao mastaa wengi wa Kibongo ndipo anapofanyia kazi zake. Pamoja na Mbaraka kuimba hakuna dawa kabisa ya mapenzi duniani, lakini ukifika kwa mganga huyo utashangaa kuwaona warembo mbalimbali wanavyoingia na kutoka kwa mganga; kinachowapeleka hapo kinatajwa kuwa ni mambo ya kung’arisha nyota za kupendwa.

“Huyu mganga bwana anakula vichwa sana, mastaa kibao hasa hawa wa kike wanafika sana kumuona, inasemekana anatoa dawa za mapenzi, mnaweza kufuatilia,” kilisema chanzo.

OFM YAFUATILIA

Mara baada ya kupata ubuyu huo, makachero wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) walianza kuichimba habari hiyo kwa kufika hadi kwenye nyumba hiyo ya mganga na kujionea warembo mbalimbali wakiingia na kutoka kwa mganga huyo.

TIPU YA MREMBO YATOLEWA

“Kuna dada mmoja mimi nafahamiana naye, alimleta rafiki yake siku moja wakashindwa kuonana na mganga, akapangiwa siku nyingine. “Yeye alisema amemleta mwenzake anaitwa Aisha ili aje amroge Diamond kwa sababu anampenda na kwamba anataka amkamate kimapenzi.

“Huyo dada aliyeniambia mnaweza kumcheki atawapa tu mkanda mzima wa rafiki yake kwa sababu yeye haamini sana mambo ya waganga na amekuwa akimuona rafiki yake kama anapoteza muda na fedha. “Nawapa namba mumpigie,” chanzo kilisema na kushirikiana kwa kila hatua na OFM ili kumpata rafiki wa mrembo aliyekwenda kumroga Diamond jambo ambalo baadaye lilifanikiwa.

SHOGA AFUNGUKA

Baada ya kupewa namba, OFM walimvutia waya shoga huyo na kumchota kwa maneno ya kishawishi ikiwepo ahadi ya kupewa fedha ili kufanikisha kumnasa mrembo mshirikina.

“Sawa, sasa siku hiyo tulikwenda hatukufanikiwa kumuona mganga tukapangiwa siku nyingine ambayo ni kesho-kutwa.

“Kama mnataka kumtoa kwenye gazeti kesho tutakapokuwa tunaenda nitawaambia mje mpige picha na kuchukua matukio mengine,” rafiki wa mrembo huyo alirahisisha kazi ya OFM na kuiweka katika mazingira mazuri ya kukamilika.

OFM ‘WATINGA’ KWA MGANGA

Siku ya tukio, OFM walifanikiwa kumpandikiza ‘mgonjwa hewa’ ambaye aliweza kuzama ndani kwa mganga huyo na kushuhudia yanayoendelea. Mgonjwa huyo akiwa kwenye foleni ndani ya nyumba ya mganga, alifanikiwa kumnasa ‘live’ Aisha ambaye alisikika akieleza kuwa amehangaika ‘kumtengeneza’ Diamond kwa muda mrefu lakini hajafanikiwa kumnasa.

“Kwa wewe huoni wanaume wengine, si utafute anayekupenda?” mganga alijaribu kumshauri Aisha ambaye alikataa kwa madai kuwa anampenda Diamond na hataki kumkosa. Wakati mazungumzo hayo kati ya Aisha na mganga yakiendelea OFM walikuwa wakichukua matukio ya video pamoja na picha za mnato kwa ujanja mkubwa.

“Kwa hiyo unataka tumfanye nini?” mganga aliuliza lakini kabla mrembo hajaeleza cha kumfanya msanii huyo anayetamba kwa ngoma kali alitoa ombi: “Kwani huwezi kuwatoa wateja wengine nje ili tuongee kwa uhuru zaidi?” Aisha alimweleza mganga ambaye alikubali ombi lake na wateja wengine wawili waliokuwepo ndani akiwepo mgonjwa feki walitolewa nje na msaidizi wa mganga huyo.

Yaliyoendelea ndani baada ya OFM kutolewa hayakurekodiwa lakini maelezo kutoka kwa rafiki wa mrembo huyo yaliyopatikana baadaye yalisema kuwa mganga huyo alimhakikishia rafiki yake kuwa atafanya ndumba na Diamond atalegea.

MGANGA ATAKA LAKI TATU

Inaelezwa kuwa mganga alimtaka Aisha alipie gharama za dawa ambazo ni takriban shilingi laki tatu ili aweze kufanyiwa dawa ya kumpata Diamond. “Aisha hakuwa na kiasi hicho aliomba aende akatafute kwanza, akipata ndipo aende kutengenezewa dawa. Na kwamba alimpa namba ya simu ili akizipata fedha wawasiliane haraka,” alisema rafiki huyo.

Baada ya Aisha kubadilishana namba na mganga kisha kutoka, siku mbili baadaye OFM iliwasiliana tena na rafiki wa Aisha ili kujua kinachoendelea. “Yaani anahaha na hii leo huwezi amini nimemsikia anaongea naye mganga amemuomba apeleke nusu kwanza nyingine atamalizia akianza kupata matumaini,” rafiki wa mrembo alisema.

Kwa mujibu wake aliliambia Amani kuwa aliomba mganga ampatie kwanza shilingi laki moja na nusu na kwamba nyingine Diamond akishaingia mtegoni atamuomba fedha za matumizi naye atakwenda kumalizia deni la dawa, jambo ambalo mganga alilikubali.

TUJIKUMBUSHE YA HAMISA

Hivi karibuni tukio la mwanamitindo Hamisa Mobeto ambaye ni mzazi mwenzie na Diamond kudaiwa kuwasiliana na mganga kwa lengo la kumroga Diamond ili kumkoleza kimahaba lilizua gumzo mitandaoni.

Itakumbuka kuwa ‘klipu’ inayodaiwa kuwa ni sauti ya Mobeto akiwasiliana na mganga wake ilienea, jambo ambalo liliibua familia nzima ya Diamond na kumtuhumu Hamisa kuwa mchawi. Kwa kuwa hakuna marefu yasiyokuwa na ncha, skendo hiyo ilififia na kuacha ujumbe nyuma kwamba: “Kumbe kuna watu katika kizazi hiki bado wanaendelea kutukuza mambo ya kishirikina.”

Kuthibitisha hilo ni tukio la mrembo huyo kunaswa akienda kumroga Diamond kwa mambo ya kimapenzi ambayo ukweli sayansi haitambui na kwamba wanaotumia mbinu hizo wengine wamekuwa wakipoteza fedha na kuambulia patupu.

MHARIRI


Nawashauri wapenzi, wanandoa kuacha tabia ya kwenda kwa waganga kwa sababu hakujawahi kuwa na uthibitisho mwema kwamba dawa za mapenzi zinaweza kufanya maajabu tofauti na mtu kujua misingi ya mapenzi na kuifuata.

1 COMMENTS:

  1. Ukichunguza maduka ya dawa za asili wateja wakubwa wanawake wanaotafuta wanaume waolewe au wale waliokwisha olewa amfanye mumewe zuzu. Hivyo haishangazi

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic