NA SALEH ALLY
KLABU ya Simba imefanikiwa kuchagua watu wa Bodi ya Wakurugenzi ambao watakuwa wanatokea katika upande wa Klabu ya Simba na ule wa mwekezaji.
Upande kwa maana ya utambuzi na malengo ya mafanikio kimaslahi wa mwekezaji na klabu yenyewe, lakini lengo namba moja ni mafanikio kwa klabu.
Simba inaweza kufanikiwa zaidi kama wajumbe, bodi hiyo ya wakurugenzi watasikilizana wakiwa na nia au lengo moja la kupatikana kwa mafanikio.
Kupishana lazima kutakuwepo lakini suala la lengo na kusikilizana linatakiwa kupewa kipaumbele kama ambavyo mara kadhaa tumekuwa tukiwashauri kuhusiana na hilo.
Katika wajumbe hao 16, mjumbe pekee mwanamke au mwanamama ni Asha Ramadhani Baraka. Huyu si mtu mgeni na hasa utakapozungumzia suala la burudani hapa nchini.
Asha Baraka ndiye mmiliki wa bendi maarufu ya dansi la kisasa nchini hasa kwa mitindo ya Kitanzania ya African Stars maarufu kama Twanga Pepeta.
Lakini amewahi kumiliki bendi nyingi kadhaa maarufu, hivyo Asha Baraka ni mtu wa burudani hasa na anajua mengi linapofikia suala la kuongoza watu kwa kuwa amekuwa mmiliki, kiongozi na mzazi.
Kuna sehemu fulani suala la timu au bendi katika uongozi linakuwa linafanana na hasa unapozungumzia mahitaji na gharama za uendeshaji. Maana yake akiutumia uzoefu wake atakuwa na faida na Simba.
Pamoja na hivyo, Asha Baraka bado ana nafasi kubwa ya kuisaidia Simba kupita njia nyingine ambayo haikuwahi kufika na ikaenda katika mafanikio.
Nakukumbusha kuwa Simba ni Sports Club, kwa maana ina uwezo wa kushirikisha michezo mingine zaidi ya soka. Tofauti na sasa, Simba wamekuwa wanajikita katika soka pekee.
Asha ni mtu aliyetokea katika michezo kabla hata ya burudani, huenda hili wengi hawalijui. Alikuwa mmoja wa wachezaji mahiri wa timu ya netiboli Bima enzi zake.
Alikuwa maarufu kutokana na umahiri wake katika mchezo huo na hili linathibitisha kweli yeye ni mwanamichezo hasa. Hapa ndipo ninataka kuanzia kuhusiana na yeye.
Simba inahitaji kujiimarisha na ndoto ni kufanya vizuri katika soka na kuwa tishio Afrika. Lakini kama Sports Club inatakiwa kutanua wigo na kwenda ikikuza michezo au timu za michezo mingine na kama ni soka pia upande mwingine.
Katika soka upande mwingine, basi ni timu za watoto, vijana na wanawake ambazo zinaweza kuijengea Simba msingi bora na pia kuitangaza katika nyanja tofauti.
Hakuna timu za soka zenye mafanikio makubwa bila ya kuwa na timu bora za watoto na vijana. Hili ni lazima na ndilo limekuwa msingi wa mafanikio ya klabu nyingi Afrika, Ulaya na duniani kote.
Bado Asha ana kila sababu ya kuweka ushawishi mkubwa kwa maendeleo ya timu ya wanawake ya Simba ambayo bado ina nafasi ya kuitangaza na kuiingizia faida klabu hiyo kama itafikia mafanikio makubwa nyumbani na kimataifa.
Kama mwanamichezo na mwanamama, anapaswa kuweka ushawishi, mipango na ushauri kuhakikisha timu hiyo inasimama na kufanya vema.
Upande wa michezo mingine, mfano netiboli, Simba inaweza kushiriki kwa kuwa na timu yake ambayo itaangaliwa kwa upande mwingine ikiwa imetafutiwa wadhamini.
Mwanzo unaweza kuwa mgumu kama ilivyo kawaida, lakini kama jambo limepangwa hakuna ambalo linakuwa linashindikana kama wahusika watakuwa wamepiga hesabu na wana uhakika wanataka kufanya jambo ambalo litakuwa na maendeleo hata kama ni baadaye.
Asha ni mzoefu na amepita milima na mabonde, asikae akakubali kusikiliza tu bila ya kuwa tayari kuonyesha uthubutu kwa kuwasilisha hoja zenye lengo la kuchangia mabadiliko au kuanzisha vipya vitakavyokuwa na msaada kwa Simba.









0 COMMENTS:
Post a Comment