Beki wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Erasto Nyoni amesema kuwa leo lazima timu ipambane mpaka tone la mwisho kupata matokeo dhidi ya Lesotho.
Stars leo wana kibarua cha kuandika historia endapo watafanikiwa kushinda katika mchezo wa Kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) yatakayofanyika mwakani nchini Cameroon.
"Tunajua kwamba taifa linatuombea nasi pia tutaonesha juhudi kufa na kupona uwanjani ili kuweza kupata matokeo na hicho ndicho wachezaji tunafikiria, Mungu yupo pamoja nasi, mashabiki watuombee tufanye vizuri," alisema.
Endapo Stars watashinda leo dhidi ya Lesotho itafuzu moja kwa moja michuano hii mikubwa Afrika ikiwa ni baada ya miaka 38 kupita kwa kuwa wakishinda leo watafikisha pointi 8.
Katika kundi L ambalo Stars ipo Uganda imefuzu baada ya kufikisha pointi 13, hivyo Stars wakishinda leo watafikisha pointi 8 ambazo hazitafikiwa na timu ya Cape Verde yenye pointi 4 na Lesotho yenye 2 zikiwa zimebakiwa na mchezo mmoja mkononi.
0 COMMENTS:
Post a Comment