NA SALEH ALLY
Katika dini, kwenda peponi ni sehemu sahihi ambayo kila mwanadamu angependa kufika. Tatizo kwetu ni kwamba lazima ufe ili kwenda peponi.
Wanadamu hawataki kufa lakini wanatamani kwenda peponi kutokana na sifa ya huko tuliyoipata kwenye vitabu vya dini.
Kwa leo, Taifa Stars inaweza kwenda “Peponi”. Peponi ya Taifa Stars si ile ya kwenye dini lakini furaha yake, utaweza ukaipa jina hilo.
Jiulize leo, Taifa Stars kama itafanikiwa kufuzu kucheza Afcon, utajisikiaje hasa kama wewe ni mpenda soka?
Si vibaya kusema Stars imekaribia kwenda “peponi” na matendo mema leo dhidi ya Lesotho pale mjini Maseru, yataifa Stars nafasi ya kufanya vema na kupita katika eneo hilo.
Stars inatakiwa kushinda, inatakiwa kupata pointi tatu tu zitakazoiwezesha kufikisha pointi nane ambazo hazitafikiwa na Cape Verde au Lesotho kama wataifunga leo.
Hakika ni kazi ngumu, ngumu kwelikweli lakini inawezekana kabisa. Vijana wetu wanaweza na sapoti yetu inahitajiwa.
Waliosafiri hadi Maseru kwa basi au usafiri mwingine ni mashujaa. Wamekwenda kuiunga mkono timu yetu, wanastahili pongezi na waifanye kazi yao sahihi.
Watanzania wote wapenda soka wangependa kuona hilo linatokea. Tokea 1980, hii si mchezo. Sasa miaka 28 bila ya kushiriki Afcon, umri wa mtu mzima mwenye familia bila ya kuiona timu ya Tanzania katika michuano hiyo. Leo iwe mwisho na Stars ipae hadi “peponi.
Mwandishi. Unapajua peponi? Mbona unawatakia mabaya.
ReplyDelete