November 14, 2018








Na Saleh Ally
UKIISHI kwa kusikiliza na kuamini mambo ya mitaani bila angalau kuyachuja na kufanya jambo fulani ili kupata uhakika basi utakwama mapema.


Wengi sana wana akili lakini ni wavivu, hawataki kuzishughulisha akili zao angalau kufikiria kidogo tu kwa kile wanachokiona au kuhadithiwa.

Mara nyingi napenda kuwa tofauti na kujaribu kutafakari au kubungua bongo. Kutafakari au kulifanyia kazi jambo fulani ambalo nakuwa nimeambiwa au kuliona.


Wakati mwingine ni raha kukiamini kile ambacho unakuwa umejiridhisha nacho kwa kuwa moyo unatulia na unaamini sahihi baada ya kukifanyia tathmini na baadaye majibu.

Kwa mashabiki wa soka au wale wa Simba, kwa sasa wengi sana wanaamini kwamba kiungo Haruna Niyonzima hana nafasi tena Simba kwa kuwa ameisha kabisa.

Wengi wanaona huu si wakati tena wa Niyonzima na anapaswa kuondoka zake kwa kuwa hafai kabisa. Wengi wanaona hana nafasi ya kung’ara tena kwa neno hilohilo amekwisha.

Wengi wanaokubaliana na  hivi, hakuna hata mmoja wao alijaribu kuhoji au kutaka kujifunza jambo. Kutaka kuangalia au kudadavua kwamba kwanini imekuwa hivyo na haraka sana.

Mchezaji kama Niyonzima aliyebeba makombe hadi matatu ya Ligi Kuu Bara, akacheza nane bora ya Kombe la Shirikisho akiwa nyota na tegemeo. Nyota kama Athumani Iddi ‘Chuji’ alikuwa pacha wake lakini baada ya hapo nyota wengine kadhaa wakaungana naye kama vile Thabani Kamusoko lakini yeye akaendelea kung’ara na kuwa kiongozi na mpishi wa mafanikio ya Yanga.

Vipi Simba hata nusu msimu hakung’ara. Tena mpira wa Simba unafanana kwa kiasi kikubwa na aina yake ya uchezaji. Maana yake ana nafasi ya kufanya vizuri zaidi na zaidi?

Ukiambiwa Niyonzima kaisha, kama unakubuka umemuona wapi, mechi ngapi na amecheza vipi? Wanaosema hivyo unawaamini vipi kiuwezo wa kumjua mchezaji aliyekwisha?

Wakati Simba waliaminishwa amekwisha, viongozi baadhi wakataka kuonyesha hafai na mpira wake ndio basi tena, benchi la ufundi la timu ya taifa ya Rwanda, Amavubi tena linaloongozwa na kocha kutoka nje ya Afrika likaona anaweza kuwa msaada. Likamchukua na kumtumia na tukaona akifanya vizuri licha ya kwamba hakuwa na nafasi ya kucheza katika kikosi chake upande wa klabu.
 

Kweli kipaji cha Niyonzima kinaweza kwisha ndani ya wiki moja au mwezi tu? Baada ya hapo asiwe bora wala msaada na Simba?

Hapo ndio ule wakati nilikuwa nausema kwamba unapaswa kufanyiwa kazi. Kufikiri, kudadavua na ikiwezekana kupata majibu sahihi.

Kama tutapishana sawa, ninaamini tofauti kuhusiana na Niyonzima, kwamba ni mchezaji bora kabisa,a nahitajika Simba na anaweza kuwa msaada mkubwa sana kuliko wengi tunavyoamini kwa kuwa ana kipaji cha juu kabisa, mzoefu kuliko wengi Simba.

Uzoefu wa Niyonzima ni kuanzia soka la Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati lakini bara lote la Afrika kwa kuwa ameshiriki michuano karibu yote akiwa na klabu za Rwanda, Yanga hapa Tanzania na pia timu yake ya taifa ya Rwanda.

Lazima tukubali kwamba alipofikia hapo, kuna tatizo na haliwezi likawa linamhusisha peke yake. Lingekuwa tatizo ni yeye tu, basi viongozi wangekuwa na uwezo wa kulitatua na kubadilisha mambo.

Kwa kuwa tatizo linaendelea maana yake kuna viongozi wanahusika. Nasema wanahusika kwa kuwa wameshindwa kutatua tatizo lake na leo tunamuona tena katika kikosi cha Simba baada ya Kocha Patrick Aussems kumuona akiichezea Rwanda na kusisitiza arudishwe.


Uongozi uliopita ulishindwa kutatua tatizo la Niyonzima arudi kucheza na kuisaidia timu yake. Lakini inawezekana Niyonzima naye ameshindwa kutatua tatizo hilo ndio maana liandelea tu.

Niliwahi kusikia kuna kiongozi alikuwa hampendi Niyonzima na alichangia kumvuruga na huenda ilikuwa kwa makusudi. Kwa sasa hata kama yupo si bosi tena kama ilivyokuwa zamani na hawezi kuwa uamuzi wa kulazimisha mambo yaende anavyotaka yeye kwa kuwa ana mabosi wake pia.

Hivyo ni nafasi kwa Niyonzima kurejea tena, uongozi ulimalize suala lake na kumuachia kazi Aussems kama atampa nafasi.

Binafsi ninaamini Niyonzima akirejea na kuanza kucheza, wengi walioamini ni mwisho wake hawatazungumza tena. Walioona hana nafasi hawatarudia tena kwa kuwa ni mchezaji wa aina yake na uwezo wake hauna mjadala kwa kipindi hiki.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic