Kocha Mkuu wa Mbao FC, Amri Said amesema kama uongozi hautafuata masharti yake ni heri abwage manyanga na kuendelea na hamsini zake kuliko kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Said amesema hayupo tayari kufanya kazi na Kocha Msaidizi Ally Bushiri ambaye alikuwa kocha wa Njombe Mji kutokana na kutoshirikishwa katika usajili wake pamoja na uongozi kukiuka makubaliano.
"Uongozi niliuweka wazi kwamba nipo tayari kuwa kocha msaidizi endapo watamleta kocha ambaye amenizidi elimu ili nijifunze zaidi na sio kumleta kocha ambaye nipo naye sawa kwenye leseni jambo ambalo sio sawa.
"Kwa kuwa Bushiri ni kocha ambaye tupo sawa kwenye elimu ya ukocha wote tuna leseni B ni bora niwakabidhi funguo za ofisi wao wanipe stahiki zangu niwe huru kwenye mambo yangu," alisema.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mbao FC, Solly Njash amesema kuwa mwalimu ana hoja ya msingi hivyo uongozi utajadili namna ya kuweza kuweka usawa masuala yanayoihusu timu ili waweze kusonga mbele.
0 COMMENTS:
Post a Comment