January 14, 2019








NA SALEH ALLY
NILIFURAHI sana kuona viongozi mbalimbali wa Serikali wakijitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu ya Tanzania ikiwa katika michuano migumu ya kimataifa.

Viongozi walijitokeza wakati Simba ikicheza mechi yake ya kwanza ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ilikuwa mechi ngumu dhidi ya JS Saoura ya Algeria.

Waarabu wanajulikana, hakuna ambaye hakwenda uwanjani bila ya hofu hata kama ni kidogo. Viongozi wengi wa Serikali kujitokeza, maana yake wana hofu lakini wanaiamini Simba.

Simba ilikuwa dimbani kwa sababu ya mashabiki na wanachama wake. Lakini uhalisia ni kwa sababu ya taifa, timu ya Tanzania dhidi ya timu ya Algeria. Ndio maana wachezaji wa Saoura na mashabiki wao walikuwa wana bendera ya taifa lao la Algeria, wanajua kwamba wanaiwakilisha nchi yao.

Mgeni rasmi alikuwa Naibu Spika wa Bunge, Tulia Akson. Baadaye nilimuona Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye sote tunamfahamu kwamba ni mwanamichezo na kocha wa soka tena wa kiwango cha juu tu kwa hapa nyumbani Tanzania.

 Mwanamichezo mwingine, Dk Damas Ndumbaro, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Baadhi ya wanasiasa maarufu kama Zitto Kabwe na wengine wengi.

Burudani ile ilikuwa inapatikana kwa neno moja tu, “juhudi”. Tukubali, juhudi hizo zilizoongezewa maarifa zimetokana na Wanasimba wenyewe.

Wamekuwa wakipambana kuhakikisha timu yao inafanya vema na tunajua ugumu unaochangiwa na mambo mengi ikiwemo gharama na kadhalika.

Pamoja na hayo Simba wamekuwa wakiendelea kupambana kuhakikisha wanafanya vema. 

Waendelee kwa kuwa ni jukumu lao. Lakini kwa mara nyingine nalirudisha suala ambalo sijawahi kuchoka kuendelea kulikumbushia.

Serikali kuzisaidia timu zinazokuwa zinacheza michuano ya kimataifa kwa kuwa zinawakilisha nchi yetu.

Nimezungumza sana, mara ya pili nililikazia wakati Yanga wakiwa wanashiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Niliwaeleza umuhimu wa hilo na Serikali inavyoweza kuchagiza.
Kabla ya hapo nilizungumzia mara kadhaa. Huenda bado halijaeleweka nimeamua kurudia kwa mara nyingine tena kwa kuwa michezo ina faida nyingi kwa taifa.

Kwa maana ya afya, burudani lakini ni ajira kubwa sana. Mfano juzi wakati wa hiyo mechi zitakuwa zimezalishwa ajira zaidi ya 1000 kwa siku moja. Watu wamefaidika sana, wamefurahi sana na afya imeimarishwa, sote tunajua.

Viongozi wa Serikali wamekuwa pale uwanjani kuonyesha wako tayari kuunga mkono michezo, maana yake wanaweza kuunga mkono kwa kutenga bajeti maalum kwa timu ambazo zinaingia katika michuano ya kimataifa kama hiyo.

Tukumbuke timu hizo zinazoshiriki michuano ya kimataifa, pia zinalipa kodi kutokana na hayo mapato yanayopatikana. Vipi Serikali bado haielewi kuzisaidia?

Mara kadhaa nimetoa mfano huu na ningependa kuurudia. Nchi ndogo kabisa ya Rwanda ambayo ukubwa wake ni mkoa mmoja tu, idadi yao hata robo ya kwetu haifikii, imekuwa ikizihudumia timu zake zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Rwanda wamekuwa wakitoa nauli kwa kila timu inayosafiri katika michuano hiyo. Inalipa nauli ya ndege kwa nchi yoyote wanayokwenda kama sehemu ya kuonyesha Serikali inajali na inaunga mkono.

Kama hata Rwanda wanaweza, na imewasaidia kuongeza hamasa na ubora. Sisi ni Tanzania, tunashindwa nini. Tafadhali Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk Harrison Mwakyembe ambaye pia ulishuhudia mechi hiyo uwanjani, lifanyie kazi hili.

Linaweza kuendelea hadi hapo baadaye. Lakini tayari kutakuwa na msaada wa hamasa. Tukumbuke kwa sasa barani Afrika inajulikana ni Simba kutoka Tanzania.

Mkiamua inawezekana, acha wawakilishi wajue kwamba Serikali nayo ina chake na wanapaswa kuongeza juhudi zaidi. Hili, limo ndani ya uwezo wenu, kama mkiamua.




6 COMMENTS:

  1. Katika siku ambayo Saleh umezungmza vitu vya maana basi ni katika makala yako haya. Nnaimani kabisa hata serikali inatakiwa kuonesha uzendo kwa wananchi wake ili kuinua morali ya uzalendo kwa wananchi wake sio maneno matupu tu.

    ReplyDelete
  2. Hongera salehe kwahili ,nikambo lamaana sana ingawa siamini sana kama viongozi waliokwenda pale taiga walikwenda kiserikali kwakutambua kuwa timu inawakilisha taifa,ninaimani waliokwenda walikwenda kwakuwa namapenzi na club,ninamaana niwanachama namashabiki was simba,wanapaswa kulizingatia ulilolishauri ili ionekane sasa niviongozi wataifa sio mashabiki was club

    ReplyDelete
  3. ndiyo maana ukaitwa Jembe uko vizuri hilo ni jambo maana na pia hata mashabiki tufikie wakati katika mashindano haya tuone klabu inayoshiriki ni kama timu ya taifa kwakuwa inawakilisha nchi kwakuwa timu moja ikifanya vizuri na kutwaa ubingwa inaweza kusaidia kuongeza idadi ya klabu za kushiriki michuano hiyo kwa msimu unaofuata.

    ReplyDelete
  4. ndiyo maana ukaitwa Jembe uko vizuri hilo ni jambo maana na pia hata mashabiki tufikie wakati katika mashindano haya tuone klabu inayoshiriki ni kama timu ya taifa kwakuwa inawakilisha nchi kwakuwa timu moja ikifanya vizuri na kutwaa ubingwa inaweza kusaidia kuongeza idadi ya klabu za kushiriki michuano hiyo kwa msimu unaofuata.

    ReplyDelete
  5. Saleh: miongoni mwa siku hujapuganya pamoja na leo. Ila usisahau kwamba PAUL KAGAME, ni mpenzi mkubwa wa soka anayefanya kwa vitendo. Viongozi wetu, ni mashabiki tu! Siyo watekelezaji. Lakini ufike wakati muzisaidie timu ambazo kwa namna moja ama nyingine zina liwakilisha,taifa letu pendwa la TANZANIA jifunzeni.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic