January 12, 2019


JEUNESSE Sportive de la Saoura, wengi wanaifahamu kwa jina la JS Saoura au JSS kwa kifupi, hii ndiyo timu ambayo leo Jumamosi kwa mara ya kwanza itaingia kwenye Dimba la Taifa jijini Dar kuvaana na Simba SC.

JS Saoura ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Algeria, ilianzishwa Septemba, 2008 katika Mji wa Méridja, Algeria na imekuwa ikitumia jezi za rangi ya kijani na njano. Inatumia Uwanja wa Stade 20 Août 1955 ambao una uwezo wa kubeba mashabiki 20,000.

Klabu hii iliwachukua misimu minne tu hadi kupanda ligi kuu na wakiwa huko bado walionekana wachovu kwani walikuwa wakimaliza ligi wakiwa nafasi ya tisa mara mbili na 11 mara moja, lakini baada ya hapo wanakimbiza.

USHIRIKI WAO KIMATAIFA

Baada ya kuzoea mazingira, kuanzia msimu wa 2015/16 wakafanikiwa kufanya maajabu baada ya kuamliza ligi wakiwa nafasi ya pili na kupata nafasi kwa mara ya kwanza kushiriki michuano ya kimataifa chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), lakini waliondolewa katika hatua ya awali.

Baada ya hapo, wakafanikiwa tena kurejea kimataifa msimu huu baada ya kufanya vyema kwenye ligi na kumaliza nafasi ya pili 2017/18 na wamejiwekea rekodi ya kutinga Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.

WALIVYOTINGA HATUA YA MAKUNDI

JSS nao walianzia hatua ya awali kabisa kama ilivyo kwa Simba kwenye michuano hii. Mchezo wao wa kwanza waliiondosha Sporting Gagnoa ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 2-0.

Baada ya hapo ikipata ushindi wa jumla wa mabao 2-1 mbele ya Ittihad Tanger ya Morocco, hivyo utaona namna ambavyo safari yao pia haikuwa rahisi kama ilivyokuwa kwa Simba.

Kitakwimu jamaa hawa kwenye michuano ya kimataifa bado ni wageni ukilinganisha na Simba ambao wamekuwa wakishiriki mara kwa mara, mara ya mwisho Simba walifanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mwaka 2003.

Saoura, haya ni mafanikio yao ya kwanza kwenye michuano ya kimataifa kwa kufanikiwa kutinga hatua ya makundi.

WANA BEKI KONKI, WASHAMBULIAJI KAWAIDA
Kama ilivyo ubora wa kipa wa Simba, Aishi Manula, pia Saoura wana kipa bora ambaye ameruhusu mabao saba tu katika michezo 16. Huyo ni Abderaouf Natèche, 36, na ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kikosini humo na ana thamani ya Sh mil 921.

Kwa upande wa safu yao ya ushambuliaji, inaonekana wazi kwamba bado haina kasi ukilinganisha na Simba. Pale Saoura anayeongoza kwa mabao ni Mohamed El Amine Hammia, Moustapha Djallit na Mohamed El Hadi Boulaouidet ambao kila mmoja ana mabao matatu.

Kwa upande wa Simba, anayeongoza kwa mabao ni Emmanuel Okwi na Meddie Kagere ambao kila mmoja ana mabao saba, hii ni kwenye ligi pekee.

HUWAFUNGI KWAO, UGENINI WANAJILINDA SANA
Ukiangalia hata katika hatua ya awali wakiwa wanasaka tiketi ya kwenda makundi, Saoura walikuwa wakicheza kwa kujilinda sana ugenini.


Matokeo yao katika michezo yao ya mwanzo, walishinda mechi zote za nyumbani na ugenini wakatoka suluhu moja na kuchapwa moja.

Pia ukifuatilia hata kwenye ligi, nyumbani wamecheza mechi nane na wameshinda nne na sare nne hawajafungwa mchezo hata mmoja. Ugenini katika michezo nane, wameshinda mmoja, sare nne na kuchapwa mawili, wamefunga bao moja na kufungwa mawili.

Kocha Nabil Neghiz amekuwa akipenda kutumia mfumo wa kushambulia zaidi wa 4-3-3 nyumbani na ugenini anajaza mabeki na viungo huku mbele akiacha mshambuliaji mmoja tu yaani 4-5-1.

Wakati Simba ikiwa na wachezaji kumi wa kimataifa, wapinzani wao, Saoura wanao nyota wanne tu kutoka nje ya Algeria. Nyota hao ni mshambuliaji kutoka Guinea, Saidouba Camara, Msenegal, Elhadji Konate ambaye ni beki, winga wa kulia, Ziri Hammar na Mshambuliaji Mtanzania, Thomas Ulimwengu.

BENCHI LA UFUNDI LIMEJAZA WAZAWA

Kuanzia Kocha Mkuu, Nabil Neghiz, 51, Kocha Msaidizi, Mohamed Belhafiane na yule wa makipa, Hassan Belhadji wote ni wazaliwa wa Algeria.

Saoura imekuwa na Neghiz tangu Machi 8, mwaka jana ambapo aliteuliwa kuwa kocha mkuu huku msaidizi wake akiwa ndiye mkongwe zaidi kikosi humo kwani yumo tangu mwaka 2012. Kocha wa makipa naye alianza kazi Julai, mwaka jana.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic