MCHUNGAJI YAMKUTA BAADA YA KUSEMA ANA DAWA YA UKIMWI
MAHAKAMA nchini Zimbabwe imemlima faini ya dola $700 (Tsh Milioni 1.6) mchungaji mmoja mashuhuri nchini Zimbabwe baada ya kumkuta na hatia ya kudanganya kuwa ana dawa ya miti-shamba inayotibu ukimwi.
Walter Magaya awali alikiri mashtaka ya kuvunja Sheria Udhibiti wa Dawa ya nchi hiyo kwa kuuza dawa ambazo hajithibitishwa. Polisi walimkamata mwezi Novemba 2018, na kuzuia dawa hizo ambazo alisema zinawatibu watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.
Zimbabwe ni nchi ya sita ya Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuwa na maambukizi ya kasi ya virusi vya ukimwi. Takribani watu milioni 1.3 walikuwa wanaishi na ukimwi nchini humo mwa 2016 kulingana na taarifa zilizokusanywa na Umoja wa Mataifa.
Mchungaji huyo ambaye hujiita mtume ana miaka 35 na miongoni mwa viongozi vijana wenye haiba ya kuvutia ambao wameibuka nchini humo tangu mdororo wa uchumi uliposhika kasi. Mwandishi wa shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) jijini Harare, Shingai Nyoka, anaripoti kuwa wachungaji hao wamekuwa wakiahidi kuwatibu wagonjwa kimiujiza na pia kutajirisha watu kwa kutumia muujiza.
Mwezi Oktoba mwaka jana, mchungaji huyo aliwaambia wafuasi wa kanisa lake kuwa dawa hiyo iitwayo Aguma, ina nguvu za kimiujiza zinazoweza kuangamiza virusi vya ukimwi kwa siku 14.
“Dawa hii ni asilimia 100 ya asili. Nasema hivyo kwa kuwa tumegundua haina madhara kwa afya kabisa,” alinukuliwa akisema hivyo na vyombo vya habari vya Zimbabwe. Serikali ya Zimbabwe ilisema kuwa kauli hiyo ni uhalifu na polisi wakavamia ofisi zake.
Hati ya mashtaka dhidi yake ilidai kuwa Magaya “aliteketeza baadhi ya vidhibiti kwa kuvimwaga chooni na kuyachoma moto makontena ofisini kwake muda mfupi kabla ya kukamatwa. Hata hivyo, baadhi ya vidhibiti vilinaswa.”
Wakili wa mchungaji huyo, Everson Chatambudza, ameiambia mahakama kuwa mteja wake aliamini kuwa dawa hiyo ilikuwa ya asili na nzuri lakini amekiri kuvunja sheria kwa kuisambaza bila kupata kibali cha wizara ya afya.
“Kulikuwa na jitihada kwa upande wa mshatakiwa kufuata sheria. Siku tatu kabla ya kuizindua aliiandikia barua wizara kuhusu ugunduzi wake… lakini kwa bahati mbaya hakupata majibu yoyote,” amenukuliwa mwanasheria huyo na gazeti la serikali la Herald. Magaya mwaka jana pia alizindua rangi ya midomo (lipstiki) ambayo alidai inatibu shinikizo la damu.
0 COMMENTS:
Post a Comment