Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kikao chake Februari 9, 2019 chini ya Mwenyekiti wake Wakili Kiomoni Kibamba ilipitia mashauri 15 yaliyowasilishwa mbele yake na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, na kufanya uamuzi ufuatao;
Mtunza Vifaa (Kit Man) wa Ruvu Shooting, Augustine Palangwa amepewa Onyo kwa kosa la kuzungumza na mwamuzi bila utaratibu katika mechi dhidi ya Yanga iliyofanyika Desemba 16, 2018 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Ibara ya 10(a) ya Kanuni za Nidhamu za TFF.
Kwa kosa la kutoa lugha ya matusi dhidi ya mwamuzi, Kamati haikumpata na hatia kwa sababu baada ya kupitia maelezo ya mlalamikaji na ripoti zote, kosa hilo limeshindwa kuthibitishwa kwa sababu ripoti za kamishna na mwamuzi zimetofautiana kuhusu tukio hilo.
Kamati imeridhia ombi la Yanga la kuahirisha kusikiliza shauri dhidi ya Abdallah Shaibu kwa vile wakati anapata mwito wa kuhudhuria akiwa mkoani.
Sasa shauri dhidi yake litasikilizwa katika kikao kijacho, na Kamati haitapokea udhuru wowote isipokuwa kama atakuwa na majukumu katika timu ya Taifa.
Bodi ya Ligi imemlalamikia mchezaji huyo kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Coastal Union katika mechi iliyozikutanisha timu Februari 3, 2019 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Kiongozi wa Arusha FC, Hassan Issa amepewa Onyo na kutozwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kutiwa hatiani kwa kutaka kumpiga Mwamuzi katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Arusha United SC iliyofanyika Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Ibara za 10(a) na 15(2) za Kanuni za Nidhamu za TFF.
Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, na faini ilipwe ndani ya siku 30.
Bw. Dennis Shemtoi ambaye pia ni Kiongozi wa Arusha FC naye amepewa Onyo na kutozwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kutiwa hatiani kwa kutaka kumpiga Mwamuzi katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Arusha United SC iliyofanyika Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Ibara za 10(a) na 15(2) za Kanuni za Nidhamu za TFF.
Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, na faini ilipwe ndani ya siku 30 kwa mujibu wa Ibara ya 15(3) ya Kanuni za Nidhamu za TFF.
Kiongozi wa Arusha FC, Bw. Amasha Masenga amepewa Onyo na faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Ibara za 10(a) na 15(2) za Kanuni za Nidhamu za TFF.
Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, faini ilipwe ndani ya siku 30.
Bw. Masenga alilalamikiwa na Bodi ya Ligi kwa kutoa lugha chafu kwenye kikao cha maandalizi ya mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya timu ya Dodoma FC.
Meneja wa Kumuyange FC, Josephat Sinzo amepewa adhabu ya Onyo na faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Ibara za 10(a) na 15(2) za Kanuni za Nidhamu za TFF.
Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, faini ilipwe ndani ya siku 30.
Alilalamikiwa na Bodi ya Ligi kuwa Novemba 11, 2018 katika mehi namba 14 ya Kundi B Ligi Daraja la Pili aliwatolea lugha chafu Msimamizi wa kituo Bw. Mrisho Bukuku pamoja na Mwamuzi.
Mchezaji Dastani D Lipinga wa Mgambo Shooting amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 38(7) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja, faini ilipwe ndani ya siku 30.
0 COMMENTS:
Post a Comment