February 16, 2019


DAR ES SALAAM: Imevuja! Uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Mivumoni, Madale jijini Dar, imekataa kuupa mtaa jina la staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ baada ya msanii huyo kuomba.

Jirani anayeishi karibu na nyumba ya Diamond aliyeomba hifadhi ya jina aliliambia Amani kuwa, kwa nyakati tofauti, Diamond amewahi kuomba Serikali impe idhini ya kuweka bango lenye jina la Diamond katika mtaa unaoelekea nyumbani kwake, lakini alikataliwa.

Jirani huyo alisema, Diamond hakufurahishwa na kitendo hicho kwani lengo lake lilikuwa ni kuona anaenziwa na wakazi wa eneo hilo kwa kitendo cha mtaa kupewa jina lake.

“Diamond si unajua tena alikuwa anaamini yeye ni staa hivyo mtaa ule utakuwa ni wake, lakini viongozi wa Serikali ya mtaa wakamuwekea ngumu na kupotezea kabisa na umaarufu wake wakaweka kando,” alisema jirani huyo.

Ili kujiridhisha na ishu hiyo, mapema wiki hii, Amani lilitia timu katika Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Mivumoni na kukutana na mjumbe, Christina Chilumba ambaye alithibitisha kuwa Diamond aliomba apewe mtaa huo, lakini ilishindikana kumpa.

Alisema kuwa, wakati Diamond anaomba, wajumbe wa mtaa huo, walikuwa tayari wameshafanya mchakato wa kuupa jina la mwenyekiti wao ambaye ni Deodatus Kamugisha.

“Hatukumpa kwa sababu tulikuwa tayari sisi tumeshafanya mchakato wa kumpa mwenyekiti wetu na ndiyo maana hadi sasa unaitwa Mtaa wa Kamugisha,” alisema Chilumba.

Kwa upande wake, mwenyekiti Kamugisha alipotafutwa na Amani kuhusiana na jambo hilo, alieleza kuwa anachokifahamu ni kwamba wajumbe ndiyo walimpa mtaa huo jina lake wakati yeye alipokuwa hayupo.

“Walinipa wakati mimi nikiwa najiunguza sikuwepo kwa takriban miaka mitatu, hilo ndilo ninaloweza kukuambia kuhusu huo mtaa ambao wameupa jina langu,” alisema Kamugisha.

Alipotafutwa Diamond kuhusiana na jambo hilo simu yake iliita bila kupokelewa ndipo akatafutwa meneja wake, Hamis Taletale ‘BabuTale’ ambaye alisema hawezi kuliongelea suala hilo kwa kuwa lipo nje ya masuala yake ya muziki.

“Lingekuwa linahusiana na shoo au muziki wake hapo ningeweza kulisemea, lakini kwa ishu ya mtaa kwa kweli siwezi kusema chochote,” alisema Tale.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic