March 15, 2019



LICHA ya ushabiki ambao tunao ni jukumu letu kuipa sapoti timu ya Simba ambayo inawakilisha nchi kwenye michuano mikubwa ambayo ni Ligi ya Mabingwa Afrika, si suala la kubeza.

Kushindwa kupata matokeo haina maana kwamba hakuna uwezo bali ni hesabu tu ambazo zinatakiwa zifanywe kwa sasa ili kuvunja rekodi ambazo zimewekwa hasa kwa timu ya Simba ikiwa ni kwa manufaa ya Taifa.

Kama walifanikiwa kuvunja rekodi ya kufuzu hatua ya makundi ambayo iliwekwa mwaka 2013 kwa nini hii isivunjwe tena Uwanja wa nyumbani? Itakuwa ajabu kama mashabiki watakata tamaa na wachezaji nao wakikata tamaa.

Kila kitu ni mipango na hesabu kali hasa kwenye ulimwengu wa mpira ambao hauna mwenyewe hasa linapofika suala la matokeo Uwanjani. Kikubwa Simba kwa sasa watulize akili zao kwanza kabla ya kukurupuka kufanya maamuzi.

Kundi D nalo limekuwa gumu kwa timu kupata nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali kila timu ina nafasi ya kushinda na kupenya hatua ya robo fainali endapo hesabu zitakubali hasa kwenye mchezo wa mwisho.

Kila timu imepania kupata matokeo kwenye Uwanja wa nyumbani hali ambayo inafanya ugumu kuwa mkubwa kwa kila timu mpaka sasa.

Ikumbukwe kwamba ni Al Ahly pekee ambao walipata sare dhidi ya JS Saoura ugenini hivyo inamaanisha ushindani ni mkubwa na hesabu ni ngumu ugenini.

Kesho jumamosi ndio kete ya mwisho ya Simba inarushwa pale Uwanja wa Taifa, sasa kikubwa ambacho kinatakiwa kufanywa kwanza ni nguvu ya mashabiki kujitokeza kwa wingi Uwanjani kushangilia timu yao.

Hatua ya robo fainali ni hatua muhimu kwa Simba na Taifa kiujumla hivyo ni wakati wa kuweka kando itikadi za ushabiki na kuwa kitu kimoja.

Nakumbuka mara ya mwisho kipindi hicho nacheza tulipata fursa ya kutinga hatua ya robo fainali ila muda umekwenda sana mpaka sasa hakuna aliyetinga hatua hiyo hivyo Taifa kuna kitu linahitaji kuona.

AS Vita sio timu nyepesi kwa sasbabu tumeona namna ilivyowapa taabu waarabu wale Al Ahly nyumbani pia Simba wanakumbukumbu ya kupoteza kwa ufungwa mabao 5-0.

Mipango sahihi na madhubuti inapaswa ifanywe ili kuona ni namna gani mashabiki na Taifa kwa ujumla linatolewa kimasomaso kutokana na ushindani ulivyo na shauku ilivyo kubwa.

Ili kulipa deni la ahadi yenu na mpango wa kushinda mechi za nyumbani muda ni sasa ambapo mkifanikiwa kupata matokeo basi njia yenu ya kusonga mbele inafunguka.

Uzuri ni kwamba baada ya kupenya hatua hii hapo kuna pointi ambazo mtaongezewa hali itakayosaidia Taifa hapo baadaye kuongeza timu nyingine kwenye michuano ya kimataifa.

Hili suala sio la kulichukulia kiwepesi kwani ni jambo kubwa na zito kwa wachezaji na mashabiki kwa ujumla kulitimiza.
Wahenga walisema penye nia pana njia hivyo mkiwa na imani na mkawa na nia moja inawezekana kupenya hatua hii kwa ushindi ambao mtaupata nyumbani.

Inabidi mkubali kwenda na falsafa ya kundi lenu D ambalo mpo kwa sasa hakuna timu ambayo imekubali kufungwa nyumbani sasa kama itatokea mkawa wa kwanza itakuwa ni ajabu na funzo pia.

Ushindi wa aina yoyote ile ndio unaotakiwa kwa Simba kwa sasa kutinga hatua inayofuata ambayo kila Mtanzania na shabiki wa Simba anapenda kufika kwa sasa.

Upande wa wachezaji wanapaswa wacheze wakiwa ni timu na washirikiane kila mmoja atumie nguvu na akili binafsi kutimiza jukumu lake Uwanjani kwa uaminifu mkubwa.

Hii itasaidia kupata matokeo chanya kwenye Uwanja wa nyumbani na itasaidia kurejesha tabasamu kwa mashabiki ambalo lilianza kupotea hasa baada ya vipigo vya kutosha ugenini.

Kwa upande wa viongozi wasiliguse benchi la ufundi waache lifanye kazi kwa ufasaha na weledi kwani kila mmoja anatambua majukumu yake hali ambayo itafanya kama kutatokea makosa ya kiufundi wao wawajibike katika hili.

Niwakumbushe kwamba Simba mnacheza na timu kubwa na ngumu hivyo hampaswi kuwa na kiburi mkijivunia mpo nyumbani kwa hali ilivyo kwa sasa kila timu hesabu zake ni kushinda ilikutinga hatua ya robo fainali kutokana na ukubwa wa michuano hii.

Macho na masikio ya watanzania kwa sasa ni kuona Simba ikiwanyanyua mikono juu kushangilia ushindi wa nyumbani utakaowapeleka mbele kwenye michuano hii ya kimataifa.

Mashabiki msisahau mkifika Uwanjani iwe kazi yenu kuu moja tu ambayo italeta hamasa kwa wachezaji kucheza kwa ari na morali kubwa kama ambavyo ilikuwa kwa mechi zilizopita.

Mkubuke kwamba kwenye mchezo mgumu dhidi ya Al Ahly nguvu yenu ilihusika na timu ikapata matokeo chanya hali ambayo iliwafanya muwe na tabasamu.

Sasa tabasamu lingine limejificha kwa AS Vita kinachotakiwa kimoja tu kushangilia mwanzo mwisho ili kuongeza lile joto la mchezo kwa Simba.

Makelele ya shangwe yatawafanya wachezaji wa Simba watambue kwamba wana kazi ngumu ya kufanya kutafuta matokeo Uwanjani hali itakayosaidia kuendelea kupambana.

Kwa upande wa wachezaji msijisahau wala kukata tamaa ni dua za Taifa kuona mnapenya hatua hii ambayo kama mgechanga karata zenu mapema hasa kwenye michuano ya kimataifa tungekuwa na unafuu angalau ila kwa kuwa kundi bado lipo huru kazi ni kwenu.

Wachezaji 11 mnatazamwa na watu wote Tanzania mmebeba furaha za watanzania mnapaswa mfanye kazi kwelikweli.

Kama mlikuwa hamjashtuka hawa wapinzani wenu wanawatambua vizuri kwa kuwa wanaishi sana hapa Tanzania pia hata wachezaji wengi tunao ambao wanatoka Congo.

Nakumbuka kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera alinukiliwa akisema kwamba atavujisha siri zenu na namna ambavyo mlivyo hii inamaanisha kwamba mbinu zenu zimevuja.

Mnachotakiwa kufanya ni kupambana mwanzo mwisho kwani isiwape taabu suala hilo la mbinu kuvuja mpira ni mbinu na juhudi Uwanjani.

Nina amini kila kitu kitawezekana kila la kheri Simba fanyeni kazi kwa manufaa ya Taifa ili kubeba pointi zitakazokuwa akiba kwetu hapo baadaye kuongeza timu nyingine hapo baadaye.

Kutoka Championi

1 COMMENTS:

  1. Simba will enjoy both, overwhelming well wishers as well as few bed wishers, but it should well be understood that our local team is representing Tanzania

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic