March 23, 2019


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kambi ya wachezaji wa timu ya Taifa na kuwaeleza kwamba Serikali na wananchi wanamatumaini makubwa kwa timu yao, hivyo wahakikishe wanapata ushindi katika mechi yao dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa maendeleo makubwa yanayoendelea kupatikana katika soka nchini.

Waziri Mkuu ametembelea kambi hiyo leo (Jumamosi, Machi 23, 2019) jijini Dar es Salaam na amewaeleza kuwa Serikali inaimani nao na kwamba wasiwe na wasiwasi kwa sababu hawana tofauti yoyote na wachezaji wa timu nyingine duniani.

“Macho yote ya Watanzania yameelekezwa katika mechi ya kesho na Serikali inamatumaini makubwa na timu ya Taifa, hivyo waelewe kwamba kesho ni siku muhimu sana. Lengo letu ni kufikia hatua ambayo mataifa mengine yamefikia”.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kamati yake itatoa sh. milioni 10 kwa kila mchezaji wa timu hiyo iwapo timu itafuzu kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON).

Makonda amesema Watanzania wanachokijua kwa sasa ni kwamba AFCON 2019 ni zamu yao, hivyo amewaomba wachezaji wa timu ya Taifa wahakikishe wanawapa furaha kwa kuifunga timu ya Taifa ya Uganda na kwamba wananchi wengi wamehamasika kwenda kuwashangilia.

Nae, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangala ameahidi kuwapeleka katika mbuga ya wanyama kwa ajili ya mapumziko iwapo wachezaji hao wataibuka na ushindi katika mechi yao dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda hapo kesho.

Dkt. Kigwangala amesema Serikali ipo pamoja na wanamichezo, ambapo amewataka wachezaji hao wa timu ya Taifa wakapigane kweli kweli kwa ajili ya Taifa lao. “Kesho muingie uwanjani kama askari wa nchi. Mkapiganie ushindi wa Taifa letu”.

Awali, Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samata amesema,”Ninafuraha si kwa sababu ya ukubwa wa mechi ya kesho bali ni kwa sababu naona kesho nakwenda kuongoza nchi. Tupo tayari kuliletea Taifa ushindi”.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

1 COMMENTS:

  1. Was kiifunga Uganda halafu wasifuzu hawana 10ml@ player? Au hapo inakuwaje?
    Mi nauliza tu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic