SIMBA YAIMALIZA YANGA IRINGA
IRINGA - YANGA jana iliumbuka mjini hapa baada ya kuambulia kipigo cha bao 1-0 lakini wote waliohusika na kipigo hicho waliwahi kung’ara na Simba.
Mfungaji wa bao pekee Haruna Shamte aliwahi kung’ara na Simba misimu kadhaa lakini hata kocha wao, Selemani Matola ni mwanachama hai wa klabu hiyo na mchezaji wa zamani wa timu hiyo ya Msimbazi. Matokeo hayo yanazidi kuipunguza kasi Yanga na kuwaongezea nguvu wapinzani wao, Simba ambao wana viporo vingi.
Yanga imetimiza michezo 28 wakati Simba imecheza mechi 20 na kuanzia wiki ijayo itaanza kuhangaika na viporo vyao.
Lipuli ambao wamepanda hadi nafasi ya nne wakiwa na pointi 44 walijipatia bao lao katika dakika ya 19 lililofungwa na Haruna Shamte ambaye alifunga moja kwa moja akiwa anapiga kona shuti ambalo lilimshinda kipa wa Yanga, Klaus Kindoki, bao ambalo lilidumu hadi dakika ya 90.
Yanga ambao kwa sasa wapo chini ya kocha msaidizi Mzambia, Noel Mwandila bado wanashika nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 67 huku Azam ikifuatia kwa pointi 56. Katika mchezo huo wa jana, Yanga ilijitahidi kufurukuta ili kurudisha mabao lakini ilionekana kuzidiwa ujanja na Lipuli ya kocha Matola.
Nafasi ya wazi ambayo Yanga waliipata kwenye mchezo wa jana ni dakika ya 57, Deus Kaseke alishindwa kufunga akiwa amebaki na kipa wa Lipuli ambaye jana hakuwa na kashikashi nyingi licha ya Yanga kutimia.
Mwandila ambaye awali alikuwa kocha wa viungo, alijaribu kufanya mabadiliko katika dakika ya 53 kwa kumtoa Thaban Kamusoko na kumuingiza Amissi Tambwe na Haruna Moshi ‘Boban’ alichukua nafasi ya Jafari Mohamed dakika ya 82 lakini hawakuweza kubadilisha ubao wa matokeo.
Katika mechi zingine za jana, Mbeya City ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Mbao FC, Coastal Union 0-0 Alliance, Kagera Sugar 2-1 Mtibwa, Biashara United 1-0 Lyon.
Nimefurahi sana timu yangu ya nyumbani kufaya vema
ReplyDeleteKweli Simba Jana iliifunga Yanga Mara mbili!labda pigo LA tatu kwa matopeni FC ni kuwa ubingwa wasahau na Simba inazidi kuwa Tajiri
ReplyDelete