Na Saleh Ally
KWA kijana wa Kiafrika mwenye ndoto ya kucheza soka barani Ulaya, soka la ushindani na mafanikio anapaswa kuamini kwamba anaweza.
Aamini hivi kuwa lazima kupambana na baada ya hapo anapaswa kujifunza kwamba mafanikio ni jambo la kupambana ukiwa na malengo unayotaka kuyatimiza.
Mafanikio si jambo la kutafuta kama unavyotafuta kitu gizani, lazima uwe ni mwenye nia na juhudi na mwenye nia ya kushinda ili kukusaidia kile unachotaka kukifikia.
Kutokana na timu nne za England kupata nafasi ya kucheza fainali za michuano yote miwili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League, sasa ule ubishi wa ligi bora ya soka duniani, umefukiwa.
Hakuna ubishi tena na unaona katika timu hizo, nyota waliozisaidia timu hizo, wanatokea barani Afrika. Arsenal imekwenda Europa League ikiwa inamtegemea Pierre-Emerick Aubameyang na sasa itacheza fainali dhidi ya Chelsea.
Upande wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Liverpool nao wametinga fainali wakiwategemea Sadio Mane na Mohamed Salah na hawa watatu ndio wafungaji bora wa Ligi Kuu England ambayo ni bora zaidi duniani.
Unapokuwa mfungaji bora kutoka ligi bora maana yake wewe ni mshambuliaji bora zaidi. Kumbuka Aubameyang kutoka Gabon, Salah wa Misri na Mane raia wa Senegal ndio wafungaji bora wa ligi hiyo kwa wakati mmoja.
Salah, Mane na Aubameyang kila mmoja amefunga mabao 22. Hivyo ndio wachezaji waliokabidhiwa kiatu cha dhahabu kutokana na kuibuka na ufungaji bora kwa msimu wa 2018/19.
Kumbuka huu unakuwa ni msimu wa pili wachezaji kutoka Afrika wanakuwa bora kwa ufungaji wa mabao katika Ligi Kuu England, msimu uliopita alikuwa ni Salah akifunga mabao 32 akiwaburuza Harry Kane na Sergio Aguero.
Safari hii, Waafrika wamepangana katika nafasi moja wachezaji watatu wakionyesha katika masuala ya ufungaji mabao, Afrika iko juu zaidi kuliko sehemu nyingine yoyote.
Hii maana yake ni hivi; thamani ya wachezaji wa Afrika imepanda sana na hasa unapozungumzia wafungaji na hii ni baada ya mabao 66 kufungwa na wachezaji watatu pekee katika ligi moja.
Kama unacheza soka Afrika na unatamani kwenda Ulaya au unacheza Ulaya na ungetamani kufanya vizuri zaidi, basi nafasi ipo na inawezekana kabisa.
Mfano mzuri kwamba wachezaji kutoka Afrika ni wazuri na wana uwezo wa kufunga, angalia mshambuliaji Mbwana Samatta, Mtanzania anayekipiga katika kikosi cha KRC Genk, ameibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Kama haitoshi, Samatta ameisaidia timu yake kubeba ubingwa wa Ubelgiji ikiwa na mchezo mmoja mkononi. Hili ni jambo jingine unaweza kujifunza na likakupa changamoto kwamba si kweli kwamba haiwezekani badala yake kila kitu cha mafanikio kwa Ulaya kinawezekana kwa Afrika.
Kama kinawezekana, kipi cha kufanya? Hapo ndipo unaweza kuangalia njia sahihi za kupita na kwa wachezaji wa Kitanzania, huu ndio wakati mwafaka wa kuanza kutazama mbali zaidi.
Salah na Mane ni miongoni mwa wachezaji wanaokwenda kucheza michuano ya Kombe la Mataifa Afrika maarufu kama Afcon. Wanatua Afcon wakiwa na jumla ya mabao 44 kwa wao wawili tu kutoka katika Ligi Kuu England.
Hii inaonyesha thamani ya wachezaji wa Kiafrika kuwa mastaa wa kweli katika ligi bora kama hiyo ya England, maana yake Afrika ina ubora na unapaswa kuendelea kukuzwa na kutumiwa.
Wako wengi wenye ubora wa namna hiyo ambao wamebaki Afrika wakiamini hawawezi kuamka. Lakini mafanikio haya ya mabao 66, yanaweza kuwa changamoto ya kuwaamsha wasimame tena na kujipigania upya.
Wachezaji wengi wa Afrika wana uwezo wa juu sana. Wamekuwa wakishindwa kujiendeleza au kuendelea kwa kuwa wanaamini ukiwa Mwafrika ni vigumu.
Kweli haiwezi kawa rahisi tu, hata Salah, Mane na Aubameyang wana historia waliyoipitia ambako walitakiwa kuwa wavumilivu na kuendelea kujituma zaidi ili kufikia malengo.
Wako wameishia njiani kwa kukatishwa tamaa, huenda hata akina Salah wangeweza kukata tamaa. Angalia maisha yake yalivyokuwa Chelsea, lakini aliendelea kupambana hadi alipoinuka akiwa AS Roma kabla ya kusimama kabisa na Liverpool.
Niamini, kama wewe ni Mwafrika na una kipaji, Usikate tamaa. Lakini kumbuka, Uafrika pekee hauwezi kuwa kigezo cha wewe kuinuka badala yake pambana kufikia malengo yako kwa kuwa inawezekana.
TAKWIMU:
AUBAMEYANG:
Mechi: 49
Ushindi: 27
Kupoteza: 15
Mabao: 49
*Kwa misimu miwili, ule wa 2017/18 alioingia katikati ya msimu, Aubameyang alifunga mabao 10 katika Premier League ukiwa ni msimu wake wa kwanza, msimu huu amefunga mabao 22.
MANE:
Mechi: 159
Ushindi: 90
Kupoteza: 32
Mabao: 66
*Ana misimu mitano sasa EPL, miwili ya Southampton aliyojiunga nayo msimu wa 2014/15 na Liverpool mitatu tokea 2016/17 na hajawahi kufunga chini ya mabao 10 kwa msimu. Msimu uliopita alifunga 10 na huu amefunga 22.
SALAH:
Mechi: 87
Ushindi: 58
Kupoteza: 9
Mabao: 56
*Ana misimu minne EPL ingawa hakuwa na misimu mizuri miwili akiwa na Chelsea tokea 2014/15 hadi 2015/16. Lakini 2017/18 alifunga mabao 32 na kuwa mfungaji bora na msimu huu uliomalizika wa 2018/19 amefunga mabao 22 na kuwa mfungaji bora pacha.
0 COMMENTS:
Post a Comment