May 19, 2019


UONGOZI wa Yanga umepanga kutumia mamilioni ya fedha watakayopata katika mauzo ya mshambuliaji Mkongomani, Heritier Makambo kwa ajili ya kufanya usajili mkubwa wa wachezaji wanaowahitaji kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu klabu hiyo imuuze mshambuliaji huyo mwenye mabao 16 kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Bara asaini mkataba wa miaka mitatu ya kuichezea Horoya SC ya nchini Guinea.

Miongoni mwa wachezaji ambao Yanga inawahitaji kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chao ni mshambuliaji wa Gor Mahia ya nchini Kenya, Jacques Tuyisenge, kipa wa Bandari, Farouk Shikala na beki wa AS Vita ya DR Congo, Litombo Bangara.

Mwenyekiti Mkuu wa timu hiyo, Mshindo Msolla amesema kuwa klabu hiyo itanufaika kupitia mauzo mazuri watakayoyapata kupitia kwa mshambuliaji wao Makambo.

Msolla alisema, mezani kwake ana ofa nne kutoka nchi tofauti zote zikimuhitaji Makambo kwa ajili ya kumsajili na siyo majaribio baada ya kuvutiwa na kiwango kikubwa ambacho mshambuliaji huyo amekionyesha tangu ajiunge na Yanga msimu huu.

Aliongeza kuwa, kuuzwa kwa Makambo klabu hiyo itanufaika kwa wao kupata fedha zitakazotosha kusajili wachezaji wengine zaidi ya mmoja watakaoendana na hadhi ya Yanga iliyopanga kusukwa upya.

“Taarifa nyingi zimezagaa kuwa Makambo amesaini mkataba wa miaka mitatu Horoya, kama uogozi gozi hatulifahamu hilo, tunatambua amekwenda huko kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya.

“Tofauti na Horoya, zipo klabu nyingine nne kutoka nchi tofauti za Afrika ambazo zimeleta ofa zao mezani, hivyo tunachoangalia hivi sasa maslahi pekee kwa ile itakayotoa ofa nzuri.

“Kama mnavyofahamu timu yetu inavyojiendesha hivi sasa kupitia mashabiki wake kwa kuichangia timu yao, hivyo kwa fedha hizo zitakazopatikana kutokana na mauzo ya Makambo yatatusaidia kutuongezea fedha za usajili,” alisema Msolla ambaye ndiye kiongozi msomi zaidi kwenye ngazi ya klabu za Ligi Kuu Bara.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic