May 6, 2019


LIGI ya wanawake Tanzania ambayo inakaribia kukamilika msimu huu ilikuwa ina ushindani mkubwa licha ya bingwa kupatikana ambaye ni JKT Queens anapaswa apewe pongezi zake kwa kutetea kombe lake msimu huu.

Mei 19 Ligi ya Wanawake inafika ukingoni hivyo ni mwanzo wa msimu mpya kwa wenye timu ambazo zimepanda watakuwa wameshajua na wale ambao watashuka daraja watakuwa wameshajua mwisho wao ni nini.

Sasa kwa haya yote ambayo yamepita hebu niwaguekie Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wasimamizi wa mpira huu ambao ni mchezo namba moja kwa kupendwa na kufuatiliwa.

Msimu huu licha ya kuwa chini ya udhamini wa bia ya Serengeti, bado tumeona ligi ikisuasua kwa kuwa hakuna ule mwamko na uwekezaji wa kweli katika soka la wanawake.

Matatizo mengi ambayo yamejitokeza msimu huu yanapaswa yatafutiwe dawa mapema ili kupata ligi bora ambayo itatoa wachezaji bora kwa ajili ya timu yetu ya Taifa.

Bado mwendo ni uleule wa kupuuzia mambo unaendelea kwani wakati ligi inaanza tulishauri maboresho kwa miundombinu pamoja na ratiba kuwa rafiki kwa wachezaji pamoja na timu.

Suala la viporo huku kwa kiasi kikubwa mmefanikiwa kwa hilo nawapa hongera licha ya kutokuwa na maandalizi mengi hasa kimataifa hivyo ni wajibu wenu kuangalia ni namna gani timu zetu za Wanawake zinaweza kushiriki kwenye michuano ya kimataifa ili kuongeza uzoefu.

Timu ya Taifa ya wanawake imekuwa ikishindwa kufurukuta inapotoka nje ama michezo ya kimataifa kutokana na kukosa mechi nyingi za kimataifa hili linatakiwa litazamwe kwa ukaribu na umakini kutafuta suluhisho la hili tatizo.

Pia upande wa vitu vya kuboresha ni pamoja na viwanja ambavyo vinatumika kwa watoto hawa wa kike kuwa chini ya viwango hali ambayo inaleta matatizo hasa kulingana na maumbile ya wachezaji wenyewe.

Kwa Dar uwanja mkubwa ambao umekuwa ukitumika kwa michezo mingi ni ule wa Karume, kwa kweli katika hili TFF inapaswa mtazame namna mpya ya kufanya maboresho kwenye uwanja wa Karume maana hali ni mbaya na wachezaji wanacheza kwa taabu.

Hebu fikiria taswira halisi ya mpira ipo hapo na hakuna anayejali kama hakuna kitu kinachotakiwa kufanywa, kapeti muda wake umekwisha hali ambayo ni hatari kwa afya za wachezaji wetu ni muhimu kufanya maboresho hasa kwa ajili ya msimu ujao.

Suala la fedha na maandalizi ya timu nalo linapaswa lipewe kipaumbele kwa kuwa kumekuwa na timu ambazo zinashindwa kufika kwenye vituo vyao kutokana na kukosa fedha za kuwawezesha, tatizo la kuchelewesha kutoa fedha liwe na sababu maalumu na sio inatokea kwa muda mrefu.

Hali hii inafanya wengi kushindwa kupata muda mzuri wa kujiandaa na hata kama wakijiandaa wanashindwa kwenda kwenye vituo kwa wakati kama hili halitachukuliwa kwa ukaribu litagharimu ligi msimu ujao na kufanya ipoteze kabisa mvuto wake.

Uwekezaji kwa watoto pia usifumbiwe macho hii itasaidia kuwa na vijana wenye uwezo mkubwa ambao wanakuzwa tangu wakiwa wadogo hali itakayotufanya tusiwe wasindikizaji kwenye michuano ya kimataifa.

Muda wa mafanikio kwa soka letu la wanawake ni sasa ni wajibu wetu kutoa sapoti ya kutosha kupata matokeo chanya yatakayoleta mabadiliko makubwa hapo baadaye.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic