May 4, 2019


UCHAGUZI wa Klabu ya Yanga ni moja ya mambo gumzo katika soka hapa nchini na tayari wagombea kadhaa wameanza kujinadi kutaka kupata nafasi za uongozi wa juu, au ujumbe. 

Wanachama wa Yanga, wanapata nafasi ya kufuatilia kampeni hizo kupitia vyombo mbalimbali vya habari, wagombea wakipambana kuhakikisha wanawashawishi ili kupewa dhamana ya kuiongoza Yanga.

Lazima tukubaliane, Yanga ni moja ya lulu la taifa letu licha ya kwamba imekuwa haitumiki vizuri au kuingia kwenye hali ya kuyumba mara kwa mara katokana na muenendo usio sahihi.

Najua Kitanzania, kuambiana ukweli ni kama kuonekana. Watu tunaamini kutoelezana ukweli ndio kuheshimiana na kupendana, jambo ambalo limetuangusha katika mambo mengi sana.

Yanga inaangushwa na Wanayanga wenyewe, hakuna anayeweza kubisha kwa kuwa hakuna anayeweza kutoka nje ya klabu hiyo kongwe akaikwamisha kama atakuwa Yanga wenyewe watakuwa pamoja na wameunda umoja thabiti unaoweza kuifanya klabu hiyo “isivamiwe” na wasiopenda kuiona inaendelea.

Nasema wanaoiangusha Yanga ni Wanayanga wenyewe kwa kuwa miongoni mwao, wengi ni wale wanaojali au kupigania maslahi yao binafsi badala ya klabu na timu yao.

Mfano kwa sasa kwenye uchanguzi wa ambao umepangwa kufanyika Mei 5 jijini Dar es Salaam, wako ambao wanafaidika na uchaguzi huo kwa maana ya maslahi.

Nasema maslahi kwa kuwa watashiriki katika kampeni za kuwanadi wagombea na kadhalika. Wako wanaozunguka kuwanadi wagombea ambao wanajua kuwa hawana faida na Yanga.

Watawapigania kuhakikisha wanaingia na kuwa viongozi lakini wanajua kwamba hawana faida na klabu hiyo.

Hapa kinachotokea, huenda kwa kuwa mgombea atakuwa na fedha nyingi na anaweza kushinda kutokana na ushawishi wa watu hao ambao watafaidika.

Kama hiyo haitoshi, wako ambao wanaweza kuwachagua kutokana na maneno tu. Huenda wasiwe na nia mbaya lakini kutokana na kuvutiwa na maneno ambayo naweza kusema ni kawaida wakati mwingine katika jambo la kampeni.

Pamoja na hivyo, wanapaswa kupima na wajue kwamba kama wanachagua, basi ni kwa ajili ya maslahi ya klabu hiyo ambayo imepitia maumivu kwa muda mrefu sasa baada ya kuondoka kwa aliyekuwa mwenyekiti wao, Yusuf Manji. 

Yanga imechoshwa na maumivu, haihitaji tena watu wa kuiumiza. Yanga inataka kuingia kwenye ahueni na maisha mazuri kama klabu nyingine zinavyoishi na haiwezi kuwa hivyo hadi ipate watu sahihi. Watu sahihi watachaguliwa na wanachama na wao ndio waamuzi wa mwisho.

Hivyo chagueni kuipa Yanga ahueni na baadaye maisha bora au mshadadie matumbo yenu au umakini duni ili muendelee kuitesa na nyie muwe mbele kwa unafiki kupiga kelele kuwa inaonewa au kudhulumiwa.

Wenye maneno mengi wako wengi, nani mtekelezaji, wapi kumbukumbu inaonyesha alifanya vema na kweli wana hadhi ya kuwa sehemu ya uongozi wa klabu ya Yanga?

Yanga ni kubwa, wanaotaka kuiongoza wana nia kweli ya kuibadilisha? Au wanaitaka Yanga wapite na kwenda mbele kisiasa wakiitumia kama njia pekee ya kuwasaidia wao na si wao kuisaidia klabu?

Wana Yanga muwe kipimo cha kinachotokea mbele yenu ili mje muwe kipimo sahihi cha maisha ya baadaye ya Yanga.

Narudia kauli yangu ya mwanzo, walio nje ya Yanga ni vigumu sana kuiangusha klabu hiyo kama ilivyo kwa wale walio ndani yake.

Hivyo wakiwa makini na upendo wao ukawa ni wa dhati, basi Yanga itaondoka katika machungu inayopitia kama kuwa klabu inayoendeshwa kwa michango ya mashabiki hadi kuwa inayojitegemea na baadaye ikiwezekana, tajiri na yenye mafanikio zaidi. rungu, liko mikononi mwenu.

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic