SAFARI ya
kumtafuta bingwa mpya ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara tayari imeanza ambapo ule
uhondo ambao ulikuwa kimya kwa muda umerudi kwa kishindo.
Ubingwa kwa
sasa upo mikononi mwa Simba ambao hawana kingine mkononi cha kufanya zaidi ya
kuutetea baada ya safari yao kimataifa kuishia uwanja wa Taifa hatua ya awali.
Miongoni mwa
timu ambazo zimeanza kunogesha utamu wa ligi ni zile ambazo zimepanda daraja
kwenye michezo yao ya kwanza wamepata ushindi mbele ya watangulizi wao ndani ya
ligi.
Polisi
Tanzania ipo chini ya kocha mpya Suleman Matola haikufanya hiyana mbele ya
Coastal Union kwa kufungua pazia kwa ushindi wa bao 1-0 mbele ya Coastal Union
‘Wagosi wa Kaya’, pia Namungo iliyo
chini ya kocha wao wa muda mrefu Hitimana Thiery ilishinda mabao 2-1 dhidi ya
Ndanda. Matola ana mengi ya kuzungumza juu ya ligi na mipango yake huyu hapa anafunguka:-
“Naona
vijana wameamua kulipa fadhila kwa mashabiki kwa kuwapa zawadi yao ya kwanza
kwa kupata ushindi wa bao 1-0 mbele ya wapinzani wetu Coastal Union, ni mchezo
wetu wa kwanza tumeufungua vema.
Nini kilichojificha kwenye mwanzo huu
wa ushindi?
“Kwanza tulikuwa
nyumbani na mashabiki wetu pia hilo ni jambo la kwanza, pili mbali ya kuwa
nyumbani tulifanya maandalizi ya umakini kwa kila hatua ambayo tulikuwa
tunafanya, tulijitahidi kutafuta makosa yetu na kuyafanyia kazi jambo ambalo
limetupa mafanikio.
“Imani yetu
kubaki kwenye mwendelezo huu ambao tumeanza nao utatupa wakati mzuri kuleta
ushindani wa kweli hapo baadaye.
Unadhani wachezaji wako wanaweza
kuendelea kukupa ushindi?
“Ni kitu muhimu, ninawaamini wachezaji wangu wote ambao uongozi umewasajili
wananipa furaha ya kuwa nao kutokana na utulivu walionao wakiwa kwenye mafunzo
hata ndani ya uwanja wanafanya kile ambacho wameelekezwa pia wanajiongeza kwa
kutumia vipaji walivyonavyo.
Malengo makubwa ya timu yapoje?
“Kwa sasa
sina malengo makubwa ndani ya timu zaidi ya kupata ushindi kwenye mechi ambazo
tunacheza, tunahitaji kuleta ushindani mkubwa na kufanya kweli ndani ya ligi
ikiwa ni msimu wetu mpya kushiriki.
“Hatujataka
kukimbilia kuwaza kutwaa ubingwa muda huu ila tunafikiria namna ya kuwa na
kikosi bora chenye ushindani ambacho kitapata matokeo chanya nje ya uwanja wetu
wa Ushirika pamoja na ndani ya uwanja wetu.
Kwa nini hujafikiria ubingwa?
“Kwa sasa
timu inajijenga ikomae iwe bora na yenye ushindani wa kweli, hapo hesabu kubwa
itakuwa ni kwenye matokeo chanya, endapo timu inapata matokeo chanya nini
kitatokea inakuwa kwenye nafasi nzuri.
“Ubingwa ni
matokeo ya kufanya vizuri sasa hapo ikitokea tukafanya vizuri kwenye michezo
yetu yote tuna nafasi ya kufanya makubwa na kuushangaza ulimwengu, ila kwanza
tunahitaji pointi tatu.
Kipi ambacho kinakupa hofu ukiwa na
timu?
“Kupoteza ni
kitu ambacho kinanipa hofu hasa ukizingatia msimu huu ushindani ni mkubwa na
kila timu inahitaji matokeo chanya, jambo hilo linanifanya niwape mbinu mpya na
kali wachezaji wangu waweze kujiamini na kutafuta matokeo kwenye michezo yote
na sio kujisahau kwani mwanzo ambao tumeanza nao ni mzuri.
Unaiona timu yako ikimaliza nafasi ya
ngapi kwenye ligi?
“Hapo kwa
namna kikosi kilivyo na tunavyopambana kujenga timu naiona ikiwa ndani ya 10
bora na hicho ndicho tunachohitaji kwani ikiwa chini ya hapo itakuwa hatari
kwetu.
“Kanuni
zimebadilika na timu nne zitashuka daraja tukizubaa nasi tutakuwa kwenye kundi
hilo ambalo hatulihitaji kabisa.
Utofauti wa msimu huu na uliopita upo
wapi?
“Kwa sasa
ligi inaanza ikiwa tayari imepata mdhamini mkuu, tayari ni moja ya tofauti kubwa
hii inamaanisha kwamba ushindani kwa msimu huu utakuwa mkubwa na ligi itakuwa
ngumu tofauti na msimu uliopita, hakutakuwa na sababu kwa timu kuchelewa kwenye
vituo na maandalizi yatakwenda vizuri hii inaleta picha kwamba kwa timu
itakayozubaa inaachwa jumla.
“Pia nipo
kwenye makazi mapya msimu huu tofauti na msimu uliopita nilikuwa Lipuli sasa
nipo Polisi Tanzania maisha yanaendelea.
Timu ipi ambayo inakutisha?
“Timu zote
ni bora kutokana na namna zilivyofanya sajili zao, ila kwangu mimi bado sijaona
timu ya kunitisha, ukiangalia Simba, Yanga, Azam hata Namungo zote zina
wachezaji wazuri kama ilivyo kwangu tukikutana nazo lazima nizipe changamoto.
“Natambua
kwamba namna ya kuzifunga hizi timu zote ni maandalizi pamoja na kujiamini
hicho ndicho ambacho nimewaambia wachezaji wangu na ninazidi kuwaambia
hatupaswi kuiogopa timu tuna uwezo mkubwa na tutafanya makubwa tukikutana nazo
lazima zifungwe tu,” anamalizia Matola
0 COMMENTS:
Post a Comment