September 29, 2019


Kuna mpango mzito wa kummaliza kimuziki staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’, Risasi Jumamosi limeunasa!

Yote hayo yanakuja mwezi mmoja baada ya Harmonize au Harmo kudaiwa kujitoa rasmi kwenye lebo ya muziki ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyomkuza kimuziki.

VYANZO VYANENA

Kwa mujibu wa vyanzo ambavyo ni watu wa karibu wa Harmo, nyuma ya pazia kuna mambo mengi mabaya na hujuma zinazofanywa na kikundi kinachojiita Team Wasafi kinacholenga kummaliza kisanaa, lakini mwenyewe ameamua kukomaa na hakamatiki.

“Kuna mpango mchafu unaendelea kuhakikisha Harmonize anashuka au kuzima nyota na kupotea kabisa kwenye ramani ya sanaa kama ilivyotokea juzikati f’lani kikundi hicho kilikuwa kinamponda.

“Nadhani ulishuhudia siku ile pale kwenye Uwanja wa Taifa (Dar), wakati wa Tamasha la Jamafest.

“Kama ulifuatilia vizuri kuna kundi lilikuwa likimshangilia Diamond (Bosi wa Lebo ya Wasafi) huku likiimba kwamba Konde Boy (Harmonize) kafulia.

“Ule ni mpango kabambe ambao umesukwa ili kumwangusha Harmonize, lakini timu ya Konde Boy (Harmonize) imeshashtukia mchezo mzima, hivyo ni kusonga mbele tu.

KUSONGA MBELE KIVIPI?

“Kinachofanyika ni kuhakikisha Harmonize anaendelea kufanya kolabo na wanamuziki wakubwa kama Skales, Burna Boy, Tekno, Wiz Kid na Davido wa Nigeria na Sarkodie wa Ghana ambazo zipo njiani na wanamuziki wakubwa wa Marekani kama Tyga na wengine.

“Mbali na kolabo pia kuhakikisha anafunika kila shoo anayopata hasa zile kubwa za nje ya nchi kama Ulaya, Dubai, Marekani na kwingine kote ili kuendelea ‘kujiuza’ zaidi.

“Lakini mbali na shughuli za kimuziki, anataka kujikita kwenye shughuli za kijamii kwa kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha maendeleo.

HARMO, JPM NA KIGWANGALLAH

“Harmonize ameapa kuunga mkono jitihada zozote za kimaendeleo zinazofanywa na Rais Dk John Pombe Magufuli (JPM) ili kuleta hamasa kwa kile anachokifanya kiongozi huyo.

“Kuhusu hilo ameamua kuendelea na mkakati wake aliouanza miezi kadhaa iliyopita ya kugawa vitambulisho vya machinga kwa wafanyabiashara maeneo mbalimbali jijini Dar, na kwa kuanzia aligawa vitambulisho 200 bure wakati uhalisia wa kupata kitambulisho hicho mtu anapaswa kulipia kiasi cha shilingi 20,000 lakini yeye anatoa bure.

“Hii yote anafanya kwa sababu anataka kuwa karibu na jamii ambayo ndiyo mashabiki wake.

“Pia Harmo ana kampeni nyingine ya kuhamasisha utalii nchini, ndiyo maana yupo karibu na Hamis Kigwangallah (Waziri wa Maliasili na Utalii).

KUGAWA CHAKULA

“Kubwa kuliko ni ujio wa mradi wake mpya wa mgahawa wake alioupa jina la Konde Boy ambao utakuwa unagawa chakula bure kwa watu wasiokuwa na uwezo sehemu mbalimbali.

Kuhusu hilo Harmo anasema; “Kidogo na kingi Mungu ndiye hutoa na yeye ndiye kamuumba maskini na tajiri!”

“Hata hapa nilipo ni kwa neema zake, sitakula na kusaza ikiwa kuna wengine kula yao ni ya shida, nitagawana nao.”

MENEJA ANASEMAJE?

Risasi Jumamosi lilizungumza na meneja wa Harmonize, Beauty Mmary ‘Mjerumani’ ili kuweza kumsikia kama anazo taarifa za mpango huo wa msanii wake kumalizwa ambapo alikuwa na haya ya kusema;

“Hatujapata tatizo lolote so far. Tumeona hiyo video (mashabiki wakimzomea Harmonize) lakini tumeichukulia tu kama mashabiki lakini hatujapata mashambulizi yale ya moja kwa moja. Mashabiki kufanya vile sisi tunaichukulia positive, inatupa changamoto ya kufanya vizuri zaidi,” alisema meneja huyo.

KOLABO ZA HARMONIZE

Kwa muda mfupi Harmonize amefanya kolabo na wanamuziki wa nje ya Bongo kama Marina kutoka Rwanda, Yemi Alade wa Nigeria, Eddy Kenzo kutoka Uganda, Emma Nyra kutoka Nigeria, Willy Paul kutoka Kenya, IYO, OmoAkin na Burna Boy kutoka Nigeria.

CHANZO: RISASI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic