September 19, 2019








Na Saleh Ally

MIAKA sita iliyopita nilikuwa nchini Ujerumani na baadhi ya vijana kadhaa, wengi wakiwa kutoka jijini Mwanza ambao walisafirishwa na kituo kimoja kwa ajili ya michuano maalum.

Vijana hao walichanganyika na vijana wachache wa Dar es Salaam kuunda timu ya Tanzania ambayo ilishiriki katika michuano hiyo maalum.



Katika michuano hiyo, kikosi cha wachezaji Watanzania kilipata nafasi ya kubeba ubingwa na wahusika, wakamshawishi mmiliki wa kituo hicho kwa baadhi ya vijana kurejea Ujerumani kwa mafunzo maalum, nilikuwa pale kwa mara nyingine.


Wakati huo, vijana waliorejea ni pamoja na aliyeonekana kuwa nyota kuliko wengine, huyu ni Said Hamis Ndemla. Alikuwa kivutio kikubwa na baadhi ya wadau wa soka katika eneo la mji wa Freiburg, walimtabiria makubwa.


Pamoja na Ndemla, mwingine aliyepewa nafasi kubwa alikuwa ni Miraji Athumani maarufu kama Sheva, kutokana na kasi yake kubwa, krosi alizokuwa akipiga.


Historia inakuwa tamu kwa kuwa vijana wote hao ambao walirejea mara ya pili nami nikaongozana nao, sasa wanacheza au waliwahi kucheza Ligi Kuu Bara.

 

Wengine ni Frank Sekule ambaye sasa yuko Biashara Mara, Caros Protus aliwahi kucheza Toto ya Mwanza, Rajab Rashid alitoka Ndanda akatua Stand United na Japhet Makalay ambaye amekuwa nyota wa Kagera Sugar, baadaye alifuatia Mudathir Yahaya ambaye hata hivyo, alirejea mapema baada ya kukataa kusoma.

Kawaida yalikuwa mafunzo ya soka uwanjani lakini baada ya hapo walisoma ikiwa ni pamoja na kujifunza kujitegemea kwa kufanya kazi kadhaa za nyumbani.


Wote hawa walikuwa vijana wa Kitanzania waliokoga nyoyo za Wajerumani wengi na mwisho wa mafunzo hayo maalum Wajerumani hao waliamua Miraji Sheva na Sekule, wabaki Ujerumani na huko wangetafutiwa timu nzuri kwa ajili ya kuchezea, wangelipwa mshahara na kupewa makazi na baada ya hapo wataendelea na shule wakipata mafunzo ya lugha ya Kijerumani.

 

Vijana hao hawakukubaliana na suala hili, waliona wamekaa nje ya Tanzania kwa mwezi mzima, hivyo walitaka kurejea. Pamoja na juhudi za Wajerumani hao kuwataka wabaki ikiwa ni pamoja kuniomba niwashawishi iwe  hivyo, ilishindikana, tukarejea.


Baadaye nilipata taarifa kwa kuwa karibu wote kasoro Mudathir walikuwa katika timu ya vijana ya Simba, kiongozi wakati ule aliwaahidi kuwasajili timu kubwa na kuwapa mshahara mkubwa na kwa kuwa Jonas Mkude na Ramadhani Singano, tayari walianza kulipwa mshahara, nao wakawa na hamu ya kurejea nyumbani.


Tokea tumerejea, Miran Sheva amecheza timu tatu za Ligi Kuu Bara hadi sasa. Mara baada ya kurejea kweli alisajiliwa Simba kubwa chini ya Mfaransa, Patrick Liewig, hata hivyo mambo yake hayakuwa mazuri. Aliamua kusafiri hadi Mwanza kuanza upya akijiunga na Toto African ambayo baada ya muda mambo yake hayakwenda vizuri, akaondoka na kwenda kujiunga na Mwadui FC ya Shinyanga alipoonyesha cheche zake kabla ya kurejea tena na kusajiliwa na Simba ambayo kwa maana ya mabadiliko ya kiwango, iko juu sana ukilinganisha na ile ya wakati wa Liewig.


Pamoja na kusajiliwa akiwa katika Simba bora kabisa, Sheva bado ameweza kupata nafasi ya kucheza. Kama haitoshi, pamoja na kucheza amekuwa nyota na msaada kwa Simba.


Wakati Sheva anakwenda Toto, rafiki yake Ndemla alikuwa Simba, Sheva alipohamia Mwadui FC, Ndemla alikuwa Simba na sasa wote wapo Simba huku Sheva akiwa nyota na tegemeo zaidi huenda kuliko Ndemla.

Maana Sheva sasa ana uhakika wa namba zaidi ya Ndemla na Kocha Patrick Aussems, anamuamini Sheva zaidi ya Ndemla kwa maana ya mchezaji anayetakiwa. Si kwamba Aussems hampendi Ndemla badala yake hajawa tegemeo namba moja katika namba anazocheza. Hii naiita simu ambayo Sheva amempigia Ndemla, mchezaji ambaye mimi namuona ni lulu ambayo imejificha “mavumbini”.

Ndemla ana kipaji cha juu, ninaamini Sheva na wenzake wanamtambua. Ndemla hana makuu, ana nidhamu ya juu na kijana anayeipenda kazi yake lakini ameshindwa kuyaondoa mapenzi ya Simba angalau kwa muda ili akapambane na kutengeneza ‘msuli’ wake ili kuweza kupambana na “wenye namba” hapo baadaye.


Nasema Sheva amempigia simu Ndemla kumkumbusha, kwamba wakati mwingine anaweza kuondoka kwa ajili ya Simba. Yaani aende sehemu ambayo atakuwa anacheza kwa lengo la kukuza kiwango chake zaidi kwa kuwa atapata “match fitness”, jambo ambalo analikosa Simba kwa kuwa ni chaguo la pili.


Sheva angeweza kubaki Simba halafu akaendelea kuwa chaguo la pili. Lakini kuondoka kwake kumempa nafasi ya kucheza zaidi na zaidi na leo amekuwa chaguo la kwanza hata kuliko nyota wake Ndemla ambaye bado ninaamini Simba hawajampa nafasi ya kutosha kwa kuwa alichonacho ni kikubwa.


Inawezekana Ndemla anaipenda Simba na ana haki lakini anapaswa kujipenda zaidi yeye na moja ya msaada mkubwa kwake ni kusikiliza simu ya Sheva kuwa anatakiwa kutoka nje ya Simba angalau kwa misimu miwili tu.


Kama Ndemla atapata timu nzuri inayoshiriki Ligi Kuu Bara na katika mechi 38 za msimu, angalau acheze hata mechi 25, basi bila shaka msimu mmoja au miwili atakuwa habari nyingine, gumzo la nchi na taifa na anayewaniwa kusajiliwa na klabu kubwa nyingi ikiwemo Simba.


Bado ninaamini hivyo kuwa Ndemla anapaswa kuondoka Simba hata kwa muda ili aende sehemu anayoweza kucheza tena na tena ili aachie alichonacho kwa faida yake na klabu yake na taifa letu kwa kuwa kipaji chake ni zawadi kutoka kwa Mungu na amekuwa akikitumia “vibaya”.

 

 

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic