September 15, 2019





NA SALEH ALLY
MAFANIKIO kwa klabu yanapimwa kutokana na kile walichokipata kutoka katika mashindano mbalimbali, yaani walituzwa kipi, hapa unazungumzia makombe.


Kunaweza kukawa na mengi kama kipimo cha mafanikio, mfano uwezo wa kifedha, umiliki wa mali na kadhalika.


Kwa kuwa timu inamilikiwa na klabu, mwisho inatoa ujumuisho wa mafanikio makubwa kwa kile ambacho inashinda. Lakini hili linawezekana limeshindikana kwa Klabu ya Southampton ya England, au yenyewe imeamua kuchagua aina yake ya mafanikio ambayo inajitegemea.


Southampton imekuwa moja ya timu zinazopanda na kushuka, hawana mafanikio makubwa England au Ulaya. Lakini unapozungumzia wachezaji wanaopata mafanikio zaidi, wengi wanatokea kwao na wakati mwingine kwa mkupuo.


Mfano Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu uliopita, wakati inazikutanisha Liverpool na Tottenham, kila upande kulikuwa na nyota kutoka Southampton.
Kidogo Tottenham, Wanyama hakuwa vizuri sana lakini beki ya Liverpool ilikuwa inamtegemea Virgil van Dijk wakati katika ushambulizi alikuwa ni Sadio Mane ambaye pia anatokea Liverpool.


Southampton imekuwa moja ya klabu ambazo haziwezi kuzungumza hata kidogo kwamba zina ndoto ya kucheza katika Ligi ya Mabingwa kwa kuwa ubingwa wa England au kuingia Top Four ya Premier League inaonekana ni “mbingu na ardhi”.


Mane na Van Dijk wamehusika kuipa Liverpool ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, angalia msimu mmoja kabla mchezaji mwingine wa zamani wa Southampton, Gareth Bale alikuwa ameisaidia Real Madrid kubeba ubingwa wa Ulaya mara tatu mfululizo.


Hii maana yake, kwa misimu minne mfululizo, wachezaji wa zamani wa Southampton wamekuwa chachu katika klabu mbili tofauti katika kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.


Hao ni baadhi lakini kuna nyota wengi sana ambao wamepata mafanikio makubwa katika timu nyingine baada ya kuondoka Southampton ambayo unaweza kusema ni moja ya klabu zinazouza hasa wachezaji wa uhakika.


Wachezaji wangekuwa bidhaa, basi Southampton imefanikiwa sana na ndiyo maana kama ungeniambia nitoe maoni yangu ya ishu ya Mbwana Samatta kama siku moja kama atatua England, basi Southampton ndiyo sehemu sahihi kwake.


Nasema hivyo kwa kuwa naona wengi wamefikia mafanikio makubwa baada ya kuwa wameuzwa na klabu hiyo kwenda nyingine na tayari imejijengea hali ya kuaminika kutokana na suala hilo.


Mfano unamkumbuka Theo Walcott aliyetamba na Arsenal na sasa anakipiga Everton FC, Adam Lallana ambaye alikuwa katika benchi fainali ya Ligi ya Mabingwa upande wa Liverpool lakini Peter Crouch, licha ya kwamba alicheza klabu nyingi kama Stoke City lakini Southampton ilikuwa msingi wake.

Jiulize vipi Southampton wanashindwa angalau kufika mbali katika Ligi Kuu England pekee. Hapa kuna jambo la kujifunza kuhusiana na utaratibu wa kimaisha na klabu zimekuwa zikiupitia, kwamba hauwezi kupata kila kitu.


Kwamba kama unataka sana mafanikio ya makombe, mara nyingi hauwezi kuwa mzuri katika suala la utengenezaji wa wachezaji kwa kuwa ukuzaji wa wachezaji unahitaji subira.


Klabu zinazohitaji mafanikio makubwa pamoja na kukuza wachezaji, hazina muda mwingi wa subira, badala yake zinataka kupata zinachotaka, hivyo inafanya zilazimike kununua wachezaji wenye uwezo wa juu kuisaidia. Hapa ndiyo timu za aina ya Southampton.


Kwamba wao wanaweza kuwa na subira, kuwa na wachezaji wanaokua na bahati mbaya au nzuri, wakikua basi wanajitokeza wenye uwezo zaidi na kuwanunua.


Inakuwa bahati mbaya kwa kuwa wao wanashindwa kuwa na makali zaidi ya kupiga hatua, lakini bahati nzuri kwa kuwa wanaingiza fedha nyingi ndiyo maana licha ya kutokuwa na makombe mengi lakini Southampton ni moja ya timu zinazojiweza vizuri kabisa kiuchumi.


Kama hiyo haitoshi, kwao kusema wanataka kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kama leo ilivyokuwa kwa akina Wanyama na Mane, si kitu kinachowezekana kwao hata kwa kutamka.


Hii inatokana na utamaduni ambao wamejijengea wao na inaonekana mafanikio namba moja ni kubaki katika ligi Kuu England, jambo ambalo kwa klabu nyingine nyingi kama Liverpool, Arsenal, Manchester United, Chelsea na nyingine, si jambo la kuzungumza kwao kwa kuwa wana uhakika wa kubaki Premier League na wanachoangalia ni ubingwa au nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na kama wakiteleza kabisa basi washiriki Europa League, hii ndiyo bahati mbaya yao.


Rekodi zinaonyesha katika fedha nyingi ambazo walitoa kumnunua mchezaji ni pauni milioni 19.2 wakati walipomsajili Guido Carrillo akitokea AS Monaco.



Zaidi ya hapo, Southampton wamekuwa wakipokea tu kwa kuuza wachezaji mbalimbali. Rekodi yao ya mauzo ya juu inashikiliwa na Van Dijk ambaye walimuuza kwa kitita cha pauni milioni 75 na kuweka rekodi ya usajili kwa mabeki England na sasa beki huyo wa kati, ndiye bora bora Ulaya akiwa amewashinda Lionel Messi aliyeshika nafasi ya pili na Cristiano Ronaldo aliyechukua ya tatu baada ya kuwa ameingia naye tatu bora.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic