September 18, 2019



SHUKRANI kubwa kwa mashabiki wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa kuipa sapoti timu ya Taifa wakati ikitimiza majukumu ya Taifa.

Sapoti ya mashabiki inapaswa iendelee siku zote bila kuchuja hata siku moja kwa timu yetu ya Taifa ambayo kwa sasa inajiaanda na michuano ya Chan.

Ikumbukwe kuwa mbele ya Burundi uwanja wa Taifa kulikuwa na ushindani mkubwa  na kila mmoja aliona namna ambavyo timu zote zilikuwa zinatafuta matokeo mwanzo mwisho katika hatua ya kutafuta tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar.

Ushindi wa mabao 3-0 ambayo yamepatikana kwa njia ya penalti sio wa kubeza kwani mashabiki mchango wao umeonekana kwa kiasi kikubwa bila kuficha.

Licha ya kuchezwa dakika 120 bado mashabiki walikuwa na moto wa kuendelea kushangilia bila kukata tamaa na mwisho wa siku mshindi akapatikana kwani morali na presha ya ushindi ilikuwa kubwa.

Ushindi wa ndani ya dakika 90 wa bao 1-1 unatoa picha kwamba kwenye soka hakuna mwalimu ambaye anahitaji kushindwa haijalishi anacheza mazingira gani ni nafasi na somo kwa wachezaji kutambua kwamba soka la sasa limebadilika.

Ushindani umekuwa mkubwa na kila mmoja hana hofu ya kupambana na mpinzani jambo ambalo ni somo tosha kwa wachezaji na mashabiki kutambua kwamba wanapaswa kuingia uwanjani bila matokeo mfukoni mpaka pale mwamuzi atakapomaliza pambano.

Mshindi wa kweli anapatikana ndani ya uwanja licha ya tambo kuruhusiwa bado ni jambo la kusubiri matokeo ndiyo kanuni za mpira zinataka.

Wachezahji kazi yenu imeandikwa kwenye historia kwani haikuwa rahisi haijalishi ni ushindi wa aina gani bado nafasi ambayo mmefikia pongezi mnastahili.

Kile ambacho mliwaahidi watanzania kuwapa ushindi na matokeo chanya mmekitimiza kwa kushirikiana kutokana na ukweli kwamba mliweka tofauti zenu pembeni na kutanguliza maslahi ya Taifa.

Kila siku na kila saa mnapaswa mfanye hivyo bila kujali mnacheza nyumbani ama ugenini kama wapinzani waliweza kuwafunga nyumbani basi nanyi ni haki yenu kushinda wakati mwingine mkiwa ugenini.

Burundi pia nao wanapaswa pongenzi kwa kuonyesha ushindani wa kweli na kuona kwamba wanaweza kuleta ugumu kwenye ardhi ya Bongo huu ni mpira wanastahili kile walichokipata.

Naona kwamba mashabiki mnazidi kuongezeka kwenye mechi za Taifa na hamasa yenu inazidi kuwa kubwa huo ni moyo wa uzalendo usife mapema bali uishi siku zote kwa ajili ya manufaa ya Taifa letu.

Uwepo wa mashabiki unanogesha shindano lolote na kuongeza umakini kwa wachezaji ingawa muda mwingine zile zomeazomea zinawapoteza kwenye ramani ni kitu kinachostahili pongezi.

Mashabiki tumeona wameungana wote hakukuwa na kusema mimi shabiki wa Lipuli ama Mbeya City wote kazi ilikuwa moja kuishangilia timu ya Taifa jambo la busara na mnastahili pongezi.

Hakuna neno zuri kwenu kwa sasa zaidi ya kusema mnapaswa pongezi zile za dhati kwa kuwa nanyi mna mioyo ya dhati kwa ajili ya Taifa.

Kujitokeza kwenu uwanjani ni funzo kwa wachezaji kutambua kwamba wanapendwa na wanaheshimiwa na mashabiki wanapaswa wasipoteze thamani yenu kwa kuishusha kiwepesi wakiwa ndani ya uwanja.

Thamani yenu itapandishwa na wachezaji kwa kupata matokeo chanya ndani ya uwanja kwa kushinda na sio kutafuta sababu za kuanza kuomba msamaha ilihali wanakuwa wapo nyumbani.

Wanasema kuwa linaloisha ni dogo kuliko linalokuja hivyo hatua inayofuata ya hatua ya makundi sio ya kuibeza hata kidogo.
Moto mkali na ushindani mkubwa unakuja ni muda wa kubadili gia kutoka kwenye hatua ya kwanza mpaka hatua ya pili ambayo nayo ni ya kutafuta ushindi.

Hakuna cha kuwaambia wachezaji kwa sasa kwa kuwa kazi ya kwanza wameikamilisha kwa uzuri ni wakati wa kujipanga upya kuanza na safari nyingine ambayo ni ya moto kuliko iliyopita.

Nidhamu na kuwa na shauku ya kupeperusha bendera ya Taifa ni silaha ambayo itawabeba watanzania na kutafuta ushindi kwenye mechi zote zinazofuata mpaka kieleweke kwa kupenya hatua ya makundi mpaka kwenda nchini Qatar kucheza Kombe la Dunia.

Hatua hiyo ni tamu na itatufanya Taifa letu lizidi kupeperusha bendera kwenye anga za kimataifa na kuwafanya wale ambao walikuwa hawaitambui Tanzania kuijua vema kenye ulimwengu wa soka.

Kitu kizuri ni kwamba kila kitu kwa sasa kinawezekana kwani sapoti kutoka Serikalini ni ya kutosha pia sapoti ya mashabiki ipo kwa timu ya Taifa.

Nini tena mnataka hapo wachezaji? Hakuna mnachotakiwa kufanya kwa sasa zaidi ya kutafuta matokeo ndani ya uwanja na kupambana kwa juhudi mwanzo mwisho.

Tanzania ina vipaji vingi na wengi wanapenda kuona timu inafanya vizuri na wakati wa kufanya vizuri ni sasa kwa kuwatoa kimasomaso mashabiki kwenye michuano ya kimataifa.

Msijishau kwamba bado kuna kazi kwa ajili ya kucheza na Sudan kwa ajili ya kufuzu michuano ya Chan jukumu hilo lipo mikononi mwenu wachezaji na Taifa linaamini mnaweza kufikia malengo makubwa kwa wakati.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic