ALIYEWAUMIZA YANGA CAF AWATABIRIA MAKUBWA KIMATAIFA
Licha ya kuiondoa timu yake ya zamani ya Yanga, Kocha Mkuu wa Zesco United ya Zambia, George Lwandamina, amekiri kiwango kikubwa kilichoonyesha na timu hiyo huku akiitabiria makubwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Kocha huyo aliyewahi kuifundisha timu hiyo, aliitoa kauli hiyo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa pili wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika alipokutana na Yanga.
Timu hizo zilivaana kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndola nchini Zambia ambao ulimalizika kwa Yanga kufungwa mabao 2-1 na kujikuta ikiangukia Shirikisho.
Lwandamina alisema kuwa hakutarajia kukutana na upinzani aliokuta Yanga baada ya timu hiyo kuonyesha kiwango kikubwa katika michezo miwili, wa ugenini uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 kabla ya kurudiana kwao na kushinda 2-1.
Lwandamina alisema alifanya kazi ya ziada kuwapa mbinu viungo wake vyumbani wakati wa mapumziko baada ya kuzidiwa kwenye nafasi hiyo ya kiungo ya Yanga iliyokuwa inachezwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Abdulaziz Makame wakisaidiana na Deus Kaseke na Pappy Tshishimbi.
Aliongeza kuwa kama timu hiyo ikiendelea hivyo, basi itafanya makubwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
“Kwangu ilikuwa zaidi ya vita kati ya timu mbili imara zilipokutana, namaanisha Yanga na Zesco, kiukweli tulikutana na kibarua kigumu na haikuwa rahisi kuwaondoa katika michuano hii.
“Yanga ina wachezaji wote wapya, lakini nakuhakikishia kuwa kama wakiendelea kukaa pamoja zaidi ya msimu mmoja, basi Yanga itakuja kuwa timu tishio zaidi kwa klabu zote za Kusini mwa Afrika.
“Mwanzoni hatukutegemea kupata upinzani wa namna hii hasa kipindi cha kwanza cha mchezo huu baada ya Yanga kumiliki safu ya kiungo kwa asilimia 100 kabla ya kwenda mapumziko na kuwapa maelekezo ambayo yalitusaidia kwa kiasi kidogo kumiliki na sisi mpira,” alisema Lwandamina.
0 COMMENTS:
Post a Comment