YANGA YAJIBU MAPIGO, YATAJA MWEZI WATAKAOKAMILISHA UJENZI WA UWANJA WAO
Wakati watani zao wa jadi Simba wakiwa wanaelekea mwishoni kukamilisha ujenzi wa viwanja vyao vya mazoezi Bunju, Dar es Salaam, uongozi wa Yanga nao unaendelea na ujenzi wa kiwanja cha Kaunda kilichopo makao makuu ya klabu Jangwani jijini humo.
Yanga inaendelea na ujenzi wa uwanja huo ambao utakuwa maalum kwa ajili ya mazoezi ya timu, na hivi sasa wapo kwenye hatua ya kusawazisha udongo kabla ya zoezi la uwekaji nyasi kufuatia.
Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela, amesema tayari ujenzi unaendelea huku akiahidi mpaka kufikia raundi ya pili ya msimu wa Ligi Kuu Bara ambayo itakuwa ni mwezi Februari, unaweza kuwa umekamilika.
"Tunaendelea na ujenzi wa uwanja wetu wa Kaunda ambao hivi sasa upo kwenye hatua ya kusawazazishiwa udongo, kuna greda mbili ambazo zinafanya kazi hiyo.
"Baada ya kusawazisha udongo huo, zoezi litakalofuata ni kuweka udongo mwingine ambao ni wa rutuba kisha upandaji wa nyasi utafuatia, na mpaka kufikia raundi ya pili ya ligi unaweza kuwa umekamilika," alisema Mwakalebela.
Mbali na Kaunda, Mwakalebela pia amefunguka juu ya ujenzi wa uwanja uliopo Kigamboni kwa kusema suala hilo tayari limeshafikishwa katika kamati husika na mchakato unaendelea vizuri.
Kiongozi huyo ameeleza Injinia atakayesimamia mchakato huo yupo huku akiwaahidi mashabiki na wanachama wa Yanga waendelee kuwa na subira kwa kuwa kila kitu kinaenda sawa juu ya ujenzi wa uwanja huo.
"Kuhusiana na suala la ujenzi wa uwanja wetu kule Kigamboni tayari mchakato unaendelea na upo kwenye kamati husika.
"Injinia atakayehusika na suala zima yupo, kwa hiyo wanachama na mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi kwani mikakati inaendelea," alisema Mwakalebela.
Imeandaliwa na George Mganga
0 COMMENTS:
Post a Comment