December 30, 2019




NA SALEH ALLY
MPIRA wa Tanzania kwa sasa tunazungumzia mambo mengi sana ya msingi ili kuhakikisha tunatoka hapa tulipo kwenda mbele zaidi.


Tayari tunajua faida ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na kufikia hatua ya robo fainali kama ambavyo walifanya Simba kabla ya kufeli msimu huu.

Hivyo kama itakuwa Simba, Yanga, Azam FC au timu nyingine itafanikiwa zaidi ni furaha ya changamoto ambayo inatuongoza kufanya mambo mengi sana kwa weledi.

Lazima tupige hatua lakini si kazi nyepesi, kuna mambo mengi sana ya kufanya kama kukuza vijana kwa misingi sahihi, kuendeleza soka la watoto, wanawake na kufanya mpira uwe biashara badala ya furaha ya moyo pekee.

Ndio maana utaona hata katika klabu, sasa hata wale waliokuwa na ngozi ya chuma kupinga uwekezaji sababu ya ushabiki tu wa moyo au sababu ya maslahi yao binafsi, sasa wameanza kubadilika na kukubaliana.

Kama haya ni malengo ya Tanzania kwa ujumla, vipi leo klabu mbili kubwa kama Yanga na Azam FC ziko katika mgogoro mdogo kabisa usiokuwa na sababu za msingi.

Nazungumzia kuhusiana na mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Ditram Nchimbi aliyekuwa Polisi Tanzania kwa mkopo na sasa amesajiliwa na Yanga. Taarifa tulizonazo, Yanga na Azam FC wamemalizana na tayari wanaamini mchezaji huyo atahamia Yanga.

Kiutaratibu, ili aingizwe kwenye mfumo na kuweza kucheza ligi kuu, Azam FC lazima wakubaliane na Polisi Tanzania na mkataba huo uingizwe kwenye mfumo wa wachezaji wa TMS ambao unamruhusu mchezaji kutambulika na Bodi ya Ligi ya yuko timu gani.

Wakati anapelekwa Polisi kwa mkopo, maana lazima hao Polisi watoe fedha kidogo kama walivyosema na wameeleza kuwa mkopo wao na makubaliano yao na Nchimbi ni mwaka mmoja. Sasa haujaisha, kama anataka kuhama lazima kuwe na makubaliano tena kati yake, Azam FC, Nchimbi na hao Polisi.

Ukweli, Yanga wanaweza kuwa wamefuata utaratibu sahihi kwa kuwafuata wamiliki sahihi ambazo ni Azam FC. Lakini wanaingia kwenye ugumu kwa Nchimbi hajamalizana na Polisi ambao bila shaka wataleta ugumu mwishoni.

Katika hali ya kawaida unajiuliza, kama mpira wetu kwa sasa hesabu ni kufika mbali, vipi kuwe na malumbano ya aina hii katika kipindi hiki. Faida yake ni nini hasa?

Kama tunajadili mambo mengi ya msingi, vipi huyu mchezaji anayekwenda timu nyingine baada ya timu yake kukubali kumuuza, imeshindwa vipi kukubaliana na timu ambayo walikubaliana kumchukua kwa mkopo hadi suala hili litambae hewani na kuwa ishu kubwa wakati kuna mengi sana ya msingi ya kufanya kwenda katika maendeleo ya mpira wetu.

Binafsi naona ni mambo yaliyopitwa na wakati na tukubaliane, vyovyote mnavyofikiri, Nchimbi anapaswa kukubali kuwa Polisi Tanzania wamekuwa na msaada mkubwa kwake kuonekana hata kuliko Azam FC hivyo anapaswa kuwaheshimu wakati anaondoka.

Tunapaswa kujifunza suala la uungwana hata kama utakuwa unaondoka sehemu moja kwenda nyingine. Thamani ya pale ulipokuwepo, ndiyo iliyokutengenezea kile ambacho wengine wanakiona.
Polisi Tanzania walitoa nafasi kwa Nchimbi kucheza, akaweza kuifunga Yanga hat trick, ikavutiwa naye. Yes ni mchezaji wa Azam FC, sasa vipi leo aondoke na kushindwa kumalizana na Polisi Tanzania eti hadi wafikie hatua ya kufungua kesi au “kufa” naye kama walivyosema wao.

Tujifunze kwenye kila tatizo, timu hazipaswi kuingia hofu ya kuwachukua wachezaji kwa mambo kama yanayoendelea. Wala wachezaji hawapaswi kuzidharau timu zilizowachukua kwa mkopo hata kama wamiliki wao wamemalizana na wanunuzi.


Kweli Polisi walikuwa na mpango na Nchimbi, makubaliano ni mwaka mmoja, akiondoka kabla, tofauti na makubaliano ni kuwaingiza kwenye mipango mipya ambayo haikuwepo. Basi waheshimuni na Azam FC, Nchimbi katikati na Polisi Tanzania mkae meza moja na mmalize suala hili dogo lisilo na nafasi zama hizi za kufikiria mambo mengi ya msingi kwenda katika mabadiliko.

7 COMMENTS:

  1. ni suala la pande zote kuheshimu mkataba.Unapotaka kumchukua mchezaji ni vizuri kuchunguza je yuko kwenye mkataba.kama yuko kwenye mkataba lazima ufikirie gharama au kitakachotokea endapo huo mkataba utavunjwa.Je Yanga walijua kuwa Nchimbi yuko kwenye mkataba.Hawakuomba kuuangalia mkataba wa Polisi na Nchimbi?Sio swala la Polisi kumalizana na Nchimbi ili aende Yanga.. ni suala la uadilifu..Yale yale ya Pius Buswita yanajirudia.Atakuwa alipitiwa na Shetani wa Yanga

    ReplyDelete
  2. Saleh Ali anaujua ukweli lakini kama kawaida anapita pembeni.Yanga wanajaribu kutumia ubabe. Mchezaji ana mkataba wa mkopo na Polisi walishamalizana na Azam.Vipi Azam wamuuze huku bado yupo kwenye mkopo?Nani analipwa mshahara wa mchezaji?Kwanini timu ikimbilie kumtangaza mchezaji huku hawajamalizana na timu anayoichezea?

    ReplyDelete
  3. hapo kuna kukuza mambo yawe magumu tu kama kulikuwa na makubaliano ya mkopo baina ya Azam na Polisi na Yanga wanataka kumnunua ni sawa Yanga wamefuata utaratibu sasa kosa la Yanga au mchezaji liko wapi? hapo ni wazi Azam ni lazima wawasiliane na wakae na Polisis kujadili hilo suala na kama kuna fidia walipane lakini sio suala la Mchezaji au Yanga msiyafanye mambo kuwa magumu sana pia ni lazima mkumbuke mchezaji akiwa kwa mkopo mmiliki ana uwezo na haki ya kumchukua saa yeyote hata kabla ya mkataba wa mkopo kwisha huku ulaya tunaona hayo mambo yanafanyika bila ya figisu yeyote ile ni makubaliano tu ya mmiliki na timu anayochezea kwa mkopo.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Bro akiwa kwa mkop wa msimu na ukatak kumrejesh katikt lazim mkae mezan ht km ni mali yako

      Delete
  4. hili ni suala dogo sana kimpira ila ukweli ligi ya bongo ina vitu viwili vya kijinga sana. 1. kuna uyanga na usimba kuanzia kwa wamiliki wa vilabu, wachezaji na wadhamini. hawa wote hupenda kuamua mchezaji aende wapi na asiende wapi. 2. kuna tatizo la kupiga pesa bila kufuata utaratibu. hapa hata mikataba ya wachezaji wenye ujuzi mdogo wa mikataba hunyanyaswa sana na hata vipaji vyao kufa huku wakihangaika kusonga mbele. nchimbi kuwa na mkataba na Polisi kiutaratibu hakuzuii timu kumuhitaji, ila pia itategemea mkataba wa mkopo kati ya Azam na Polisi unasemaje kivipengere. Yanga wamewafuata Azam kama wamiliki wakawambia poa tukae mezani na wakaafikiana. Azam wanatakiwa kuwataarifu Polisi juu ya biashara ya Mchezaji wao na sio Yanga. Polisi wanatakiwa kuwasilisha madai ya kifedha au vipengele vilivyokiukwa na Azam kwa Azam kuwaeleza hitaji lao.

    ReplyDelete
  5. Yaaani sijui kama tutaenda mbele kwa hali hii.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic