December 23, 2019


Hatimaye Yanga kwa mara nyingine tena imemsajili kiungo fundi aliyeichezea timu hiyo kabla ya kujiunga na Simba na baadaye kurejea kuitumikia klabu ya kwao Rwanda, AS Kigali.

Niyonzima alitambulishwa na Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Mhandsi Hersi Said, baada ya Mnyarwanda huyo kusaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo jana mjini Kigali, Rwanda.

Huku baadhi ya mashabiki wakibeza uwezo wa kiungo huyu mnyumbulifu, Niyonzima ambaye kwa sasa ni nahodha wa AS Kigali, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaeleza anakuja kupambana.

Niyonzima ni miongoni mwa wachezaji wapya ambao wamekamilisha kutia saini ya kujiunga na Yanga katika dirisha hili dogo, wengine wakiwa ni mshambuliaji Tariq Seif aliyekuwa akicheza soka la kulipwa nchini Misri, beki wa kushoto kutoka JKT Tanzania, Adeyun Saleh Ahmad pamoja na straika Ditram Nchimbi aliyekuwa akiichezea Polisi Tanzania kwa mkopo akitokea Azam FC.

“Nafahamu nilipoondoka mashabiki wa Yanga hawakupenda, lakini maslahi ndiyo yaliyoniondoa siyo kingine, nilikwenda huko sikuwa na upepo nao mzuri na ndiyo maana mkataba wangu ulivyoisha niliamua kuondoka.

“Ninarejea tena Yanga ikiwa ni klabu iliyonilea, kunikuza na kunifikisha hapa nilipo, hivyo ninakuja kwenye timu ninayoipenda, naahidi kuipambania kwa kipindi chote nitakachokuwapo hapo,” alisema Niyonzima maarufu kama Fabregas.

Yanga inatajiwa kushuka Uwanja wa Uhuru leo kuikaribisha Iringa United kwenye mechi ya kuwania Kombe la Shirikisho la Soka nchini (TFF) maarufu kama FA Cup.

Bingwa wa michuano hiyo, hupata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic